Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mashinji atoka jela baada ya CCM kumlipia faini ya Sh30 milioni

98671 Pic+mashinji+jela Mashinji atoka jela baada ya CCM kumlipia faini ya Sh30 milioni

Wed, 11 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chama cha  Mapinduzi (CCM) kimelipa faini ya Sh30 milioni aliyotakiwa kulipa mwanachama wa chama hicho, Dk Vicent Mashinji ili kutoka jela.

Mashinji na viongozi wanane wa  Chadema jana Jumanne Machi 10, 2020 walihukumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kulipa faini ya Sh350 milioni au kwenda jela miezi mitano baada ya kutiwa hatiani  katika mashtaka 12 kati ya 13 yaliyokuwa yakiwakabili.

Kutokana na jana jioni kushindwa kukamilisha taratibu za kulipa fedha hizo, walipelekwa katika gereza la Segerea, huku taratibu za kuwatoa zikifanywa na Chadema walioanza kuchangishana fedha huku CCM kupitia wa Katibu wa Itikadi na Uenezi, Humphrey Polepole wakieleza kuwa watachanga fedha kwa wanachama wake wa Dar es Salaam ili kumtoa Dk Mashinji.

Mwananchi lililopiga kambi katika gereza la Segerea leo Jumatano Machi 11, 2020 kuanzia asubuhi lilishuhudia Polepole akifika katika gereza hilo sambamba na wanachama wengine wa CCM na kuondoka na Dk Mashinji.

Akizungumza baada ya kutoka jela, Dk Mashinji amesema, “ sikutegemea wana CCM watanilipia faini, sikutegemea wangelifanya jambo hili kwa uzito kama huu maana hadi jana familia yangu ilikuwa inaendelea kutafuta fedha ili kunitoa.”

“Ila leo wana CCM Mkoa wa Dar es Salaam wamejiunga kwa pamoja na kunilipia faini, nashukuru nipo chama dume kwa ajili ya kutoa mchango wangu kwa Taifa.”

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Awali katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Polepole alisema baada ya hukumu hiyo kutolewa  jana viongozi na wanachama wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam walianza utaratibu wakutafuta fedha hizo.

Amesema hadi leo asubuhi utaratibu huo ulikuwa umekamilika na walifika mahakamani kwa ajili ya kuelezwa taratibu.

"Tulifika asubuhi kwa ajili ya kupewa utaratibu namna ndugu yetu tutamnusuru na kifungo na utaratibu ni wa kielektroniki baada ya kupewa  namba tumeenda kuweka fedha benki na  kurudi kwa ajili ya kupewa kibali cha kwenda kumtoa gerezani.”

"Tumelipa na kupewa risiti ya mahakama hatua inayofuata ni kwenda kumtoa gerezani kisha kumpeleka kwa familia yake. Ni  mwanachama wetu mpya anaamini utii wa sheria bila shuruti na kufanya kazi kwaajili ya kuleta maendeleo,” amesema Polepole.

Happyness  ambaye ni mke  wake wa Dk Mashinji ameishukuru CCM kwa  namna ilivyojitoa na kuonyesha ushirikiano kwa mumewe.

"Naishukuru CCM kwa umoja na ushirikiano waliouonyesha sikutegemea kama mambo yangeenda haraka hivi na Vicent ni mwanchama  mpya,” amesema Happyness.

Mbali na Mashinji,  washtakiwa wengine ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Katibu mkuu wa chama hicho, John Mnyika; naibu katibu mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu; mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa; Esther Matiko (Tarime Mjini); Halima Mdee (Kawe); Ester Bulaya (Bunda) na John Heche (Tarime Vijijini).

Chanzo: mwananchi.co.tz