TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeonya kuwa msimamizi yeyote atakayesababisha Mahakama itengue matokeo ya uchaguzi, atatakiwa kufidia hasara na gharama za kurudia uchaguzi.
Kamishina wa NEC, Balozi Omari Ramadhani Mapuri pia alisema tume haitasita kumchukulia hatua msimamizi wa uchaguzi, atakayefanya kwa makusudi vitendo vitakavyosababisha uchaguzi kuharibika katika jimbo au kata.
Mapuri alitoa onyo hilo mjini Sumbawanga katika kikao cha NEC na waratibu na wasimamizi wa uchaguzi katika mikoa ya Rukwa, Songwe na Katavi.
Alisema, msimamizi wa uchaguzi ataadhibiwa kwa kuzingatia Kifungu cha 89A cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Sura ya 292.
"Kwa kuzingatia Sheria hiyo ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, tume haitasita kumchukulia hatua msimamizi wa uchaguzi atakayefanya kwa makusudi vitu vitakavyosababisha uchaguzi kuharibika katika jimbo au kata,” alisema Mapuri na kuongeza;
"Msimamizi huyo wa uchaguzi atatakiwa kufidia hasara hiyo kwa mujibu wa Kifungu cha 89 B cha Sheria za Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292,” alisema.
Mwakilishi wa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Amos Akim aliwakumbusha wasimamizi wa uchaguzi kuwaapisha mawakala wa vyama vya siasa ifikapo Oktoba 21
"Oktoba 28 mwaka huu ndio siku ya kupiga kura...vituo vinatakiwa kufunguliwa saa moja asubuhi kama inavyoelezwa na tume...watendaji wa vituo waelezwe kuwahi vituoni mapema ili wafanye maandalizi. Baada ya wapigakura kupiga kura zao wanatakiwa kuondoka vituoni," alisema Akim.
Alisema baada ya kukamilika kwa uboreshaji daftari la kudumu la wapigakura kwa awamu zote mbili, kama ilivyo matakwa ya kisheria, kwa sasa lina wapigakura 29,188,347. Alieleza kuwa kwa nchi nzima kutakuwa na vituo 81,567 vya wapigakura.