Wapenzi na wanachama wa Chadema wameanza kujitokeza kwaajili ya kuhudhuria mkutano wa hadhara wa wa chama hicho.
Mkutano huo unatarajiwa kufanyika kwenye uwanja wa Obwere mjini Shirati leo Machi 14, 2023 pamoja na mambo mengine mengine unalenga kumpokea rasmi aliyekuwa mgombea ubunge Rorya, Ezekiel Wenje aliyekimbilia mchi jirani baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu 2020.
Wapenzi hao wameanza kufika uwanjani hapo baada ya kukatika mvua, huku wengine wakilazimika kwenda Utegi umbali wa zaidi ya kilomita 40 kuwapokea viongozi wa kitaifa wa chama hicho.
Akizungumza uwanjani hapo, Mwenyekiti wa Baraza la wanawake wa Chadema (Bawacha), Angela Lima amesema kuwa maandalizi yote yamekamilika kinachosubiriwa ni viongozi kuwasili uwanjani hapo.
"Msafara utakuwa unaongozwa na mwenyekiti wetu (Freeman) Mbowe na Naibu Katibu mkuu Zanzibar, Salum Mwalimu na viongozi wengine wa kitaifa, kanda na mkoa," amesema
Mwenyekiti huyo pia amelishukuru na kulipongeza Jeshi la Polisi kwa namna ambavo limewapa ushirikiano tangu maandalizi ya mkutano huo hadi sasa.
"Msafara wa viongozi wetu utaiongozwa na polisi na kwakweli hili ni jambo jema kwani tangu tulipopeleka barua polisi kwa ajili ya kutoa taarifa ya mkutano huu wametupa ushirikiano wa kutosha," amesema.
Amesema kuwa anaamini kuwa ushirikiano huo unatokana na maridhiano baina ya chama chake na serikali huku akisema kuwa hali hiyo inawapa wananchi uhuru wa kushiriki mikutano ya hadhara kwa uhuru bila woga.