Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mapendekezo ya CHADEMA Tume Huru ya Uchaguzi

Chademapxm Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe.

Tue, 21 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimewasilisha mapendekezo kwa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi, kutaka marekebisho ya kanuni za uboreshaji daftari la kudumu la wapigakura ikiwa kuwapo utaratibu wa vyama kufanya kampeni ndani ya magereza.

Maoni hayo ambayo yamewasilishwa kwa Tume, wamependekeza kabla ya kuandikisha wapigakura ambao ni wafungwa na mahabusu, ifanyike sensa ya kujua idadi yao wanaotumikia adhabu ya kifungo kisichozidi miezi sita.

Kadhalika, kimependekeza ifanyike hivyo kwa mahabusu waliopo kwenye magereza yote nchini yakiwamo makuu 12, ya wilaya 68, ya kilimo 46, kambi 40 na vyuo vya mafunzo kwa upande wa Zanzibar.

Pia kuwekwa kwa utaratibu wa vyama vya siasa kuwa na mawakala wa uandikishaji katika  magereza ili kusimamia kazi hiyo ya uandikishaji wa wafungwa na mahabusu.

Kimependekeza kwamba Balozi za Tanzania nje ya nchi ziwe na vituo vya kuandikisha wapigakura ili kuwawezesha Watanzania wanaoishi nje ya nchi kuwa na haki ya kujiandikisha kuwa wapigakura.

"Kama tumeweza kutoa haki hiyo kwa wafungwa na mahabusu, tuwape Watanzania wenzetu wanaoishi nje ya nchi haki hiyo," ni sehemu ya mapendekezo ya chama hicho.

Mapendekezo mengine ni kutaka kuwapo na sifa mahususi za mtu kuteuliwa kuwa mratibu wa uandikishaji ngazi ya mkoa.

Kimetaka Tume iwe na jukumu la kusimamia na kuandikisha wapigakura katika Daftari la Kudumu la Wapigakura kwa ajili ya kura ya maoni na uchaguzi wa serikali za mitaa. 

Aidha, kuwe na utaratibu wa kuitaka Tume kuwasiliana mara kwa mara na wadau wa uchaguzi hasa vyama vya siasa wakati wote wa kuboresha daftari hilo ikiwa ni pamoja na kutambua na kugawa vituo vya uandikishaji wa wapigakura.

Chama hicho kimetaka iongezwe kanuni kuruhusu waandishi wa habari kuwa kati ya wanaoruhusiwa kuingia kwenye vituo vya uandikishaji na kuongeza wigo wa vitambulisho kwa kuongeza kitambulisho cha Mzanzibari Mkaazi.

Kimependekeza pia vyama vya siasa vipewe fursa ya kukagua daftari la awali ili kupeleka mapendekezo yao ya kuboresha daftari.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live