Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maoni ya wabunge saa 72 kabla ya bajeti

8814 Pic+maoni TZW

Tue, 12 Jun 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dodoma. Zikiwa zimebaki saa 72, Bajeti Kuu ya Serikali ya mwaka 2018/19 kusomwa, wabunge wameitaka Serikali kuishi kile inachohubiri kwa kupunguza gharama za ada, tozo na kodi ili kuchochea uwekezaji wa Tanzania ya Viwanda.

Pia, wametaka bajeti itakayosomwa Alhamisi wiki hii na Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Philip Mpango kujali utu na ubinadamu kwa kuweka mazingira wezeshi kwa wananchi kupata huduma stahiki kama afya, elimu bora na chakula.

Bajeti hiyo ni ya tatu tangu utawala wa Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli ilipoingia madarakani Novemba 5, 2015.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Mwananchi, baadhi ya wabunge walizungumzia ada, tozo na kodi kuwa kikwazo.

Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya Fedha na Mipango, Halima Mdee alisema changamoto kubwa ni kuwa hakuna ukweli kuhusu uwezo wa kukusanya mapato ya ndani jambo linalokwamisha utekelezaji wake.

“Mdee ambaye ni mbunge wa Kawe (Chadema) alisema, “Waziri Mpango atakuja na Sh17 trilioni, wakati tunaweza kukusanya Sh14 trilioni, tunakwenda na pungufu ya Sh3 trilioni kwa hiyo wasitoe matumaini makubwa ambayo hayapo. Tuna shida kubwa ya deni la Taifa kuwa mzigo na Serikali haitaki kukubali.”

Alisema kunahitajika kujengwa mazingira rafiki kwa walipaji kodi na lazima kuwe na muda wa uwekezaji na si kudaiwa wanapoanza tu biashara.

Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe alisema anatarajia kuona bajeti yenye uhalisia akidai tangu utawala huu uingie madarakani haujawahi kuwa na bajeti halisi. “Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) katika bajeti ya mwaka 2016/17 ilikuwa ya Sh29.5 trilioni lakini kati ya hizo Sh1.5 trilioni hazionekani zilivyotumika,” alisema.

Alisema Serikali imeendelea kuandaa bajeti zisizotekelezeka na kwamba anatarajia kuona kipaumbele kikiwekwa kwa viwanda vya nguo ambavyo vitazalisha kwa wingi na kufungua milango ya kuuza bidhaa nje.

Mazingira ya uwekezaji

Mbunge wa Maswa Magharibi (CCM), Mashimba Ndaki alisema bajeti inapaswa kuja na sera nzuri za kukuza viwanda kwa kupunguza urasimu wa kodi, ada na tozo ili kuwezesha wawekezaji kuwa na mazingira rafiki kuanzia mwanzo wa uwekezaji.

Kilimo

Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Constantine Kanyasu alisema ili bajeti iwe na mtazamo wa uchumi wa viwanda ni lazima kuimarisha kilimo kwa kuweka fedha za kutosha kwenye pembejeo na kuwapo kwa wataalamu.

Kanyasu alishauri kuondoa kodi kwenye zana za kilimo, kuhamasisha kuongeza thamani ya mazao, kuongeza bajeti kwenye vyuo vinavyotoa wataalamu watakaoviendesha viwanda, na kuweka fedha za kutosha kwenye miundombinu inayosaidia kukua kwa viwanda kama vile reli, barabara, maji na umeme.

Mbunge wa Mbinga Mjini (CCM), Sixtus Mapunda alisema inahitajika uwekezaji katika bajeti ya kilimo ikiwamo kuongeza thamani ya mazao na kuyatafutia masoko.

Huduma za jamii

Mbunge wa Vunjo (NCCR-Mageuzi), James Mbatia alisema ili kupata matumaini katika viwanda, suala la utu wa binadamu lipewe kipaumbele.

Mbatia alisema inahitajika bajeti yenye kuonyesha maendeleo ya watu na si ya vitu. “Vyanzo vya mapato vya kodi vya halmashauri virudishwe huko kwani ndiko wananchi waliko lakini halmashauri zikiwa hoi bin taabani usitegemee maendeleo,” alisema Mbatia ambaye ni Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi.

Chanzo: mwananchi.co.tz