Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Manguya: Aanza safari ya matumaini Newala

46494 Pic+mangu

Wed, 13 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Inawezekana safari mpya ya ‘matumaini’ imeanza na hii ni baada ya mwanzilishi wake Edward Lowassa kurejea CCM huku akifuatwa na wanasiasa wengine waliokihama chama hicho na kwenda upinzani.

Safari ya matumaini ya Lowassa ilizinduliwa Mei 30, 2015 kwenye Uwanja wa Shekhe Amri Abeid mkoani Arusha alikotangaza nia ya kuomba ridhaa ya kugombea urais kwa tiketi ya CCM.

Lakini, safari ya matumaini ilikatishwa na vikao vya CCM baada ya kukata jina la Lowassa na aliamua kwenda Chadema ambako hakuendeleza kauli mbiu yake ya safari ya matumaini badala yake alitaka mabadiliko.

Lowassa amerudi nyumba, kwenye chama cha CCM, pia hajarudi pekee yake wamo waliokumbwa na joto lake la kuhamia upinzani ambao nao wamerejea chama tawala.

Suala kwamba Lowassa amerudi kufanya nini CCM ni siri yake na waliompokea, lakini kwa kijana Juma Manguya aliyelisaka jimbo la Newala kwa karibu muongo mmoja akiwa chama hicho kabla ya kuhamia CUF, kurudi kwake ni kwa lengo la kugombea jimbo la Newala Vijijini.

Akizungumza na Mwananchi, Manguya anasema sasa amerejea CCM kwa kuwa Rais John Magufuli amekirejesha chama katika maadili.

Swali: Kwa kuwa sasa nyakati za uchaguzi zimekaribia, ndiyo umerudi?

Jibu: Wakati huu nimeamua kurejea CCM, sijatangaza kugombea popote, kwanza kwa sababu hakuna jimbo lililo wazi.

Swali: Kwa nini urudi CCM wakati huu?

Jibu: Nimerudi kwa sababu naona Rais John Magufuli amekirejesha chama katika misingi ya uadilifu tofauti na zamani. Hakuna tena ubabaishaji ndani ya chama ambao tulikuwa tukiulalamikia kwa muda mrefu.

Nimerejea ili kushiriki kukijenga chama na kumuunga mkono Rais Magufuli kuwaletea maendeleo wananchi.

Nimerudi kwenye tawi langu la Mtanda wilayani Newala na kuomba kurejea na baada ya kutafakari ombi langu nimerejeshwa.

Swali: Mtu akisema unatafuta madaraka kwa nguvu utasemaje?

Jibu: Si kweli. Mimi niliamua kuacha ajira yangu ya polisi nikajiunga na siasa ili kuwatumikia wananchi. Baada ya kushindwa kura za maoni, niliajiriwa tena na Serikali kupitia Tanesco na huko nimefanya kazi nzuri ya upelelezi kiasi cha baadhi ya maofisa wa shirika kukamatwa na kesi zinaendelea mahakamani.

Nilipokwenda CUF ni kwa sababu hakukuwa na mazingira mazuri ndani ya CCM, lakini sasa nimerudi baada ya mazingira kuboreshwa. Hivyo nimerudi nyumba kuunga mkono juhudi za Rais kuleta maendeleo.

Swali: Wakati huu ukarudi kwenye chama kile kile unachokilalamikia?

Jibu: Hapana, unajua kama wewe unajiona ni mchezaji mzuri na hupangwi kwenye timu, basi unatafuta timu nyingine. Kwa hiyo mimi niliamua kujiunga na CUF na nikapitishwa kuwa mgombea ubunge Newala mjini. Nilikosa kura chache tu kumfikia Mkuchika.

Swali: Baada ya kuingia kwenye siasa mwaka 2010 ulifanikiwa kiasi gani?

Jibu: mwaka 2010 nilifanya vizuri lakini hakukuwa na mifumo ya haki na ndiyo maama sikupitishwa. Nilishika nafasi ya tatu nyuma ya Ajali Akbar Nwangala ambaye ni mbunge wa Newala Vijijini aliyekuwa wa pili na mbunge wa sasa Waziri George Mkuchika aliongoza.

Swali: Baada ya kupoteza nafasi hiyo ulichukua hatua gani kama unaona hukutendewa haki?

Jibu: Sikwenda kushitaki bali niliamua kujikita zaidi kwenye shughuli za uchumi.

Mwaka 2012 niliajiriwa na Shirika la Umeme (Tanesco) Mtwara kama ofisa usalama na mwaka 2014 nilihamia Bukoba Mkoa wa Kagera na nilifanya kazi nzuri, hadi nilipoiacha Agosti 2015 nikarudi tena kwenye siasa.

Swali: Baada ya hapo, ukachukua uamuzi gani kisiasa?

Jibu: Baada ya hapo niliamua kurudi kwenye kazi zangu binafsi. Mimi ni mkulima wa korosho na pia niliamua kuanzisha kampuni yangu ya mafunzo ya udereva inayoitwa Pachoto yenye matawi Mtwara, Dar es Salaam, Dodoma na Mwanza.

Swali: Kwa kuwa wewe ni mkulima wa korosho, unaonaje sakata hili la Serikali kununua korosho za wakulima?

Jibu: Niwaambie tu wakulima kuwa alichokifanya Rais Magufuli ni kitendo cha uzalendo mkubwa. Kuna wakati kiongozi anafanya uamuzi ambao hata kama unawaumiza wananchi lakini unakuja kuleta faida.

Kwa sababu alitaka kuwadhibiti wanunuzi wanunuzi binafsi waliolenga kuwakandamiza wakulima. Ndiyo maana wakulima wengi wmelipwa kwa bei ya Sh3,300 kwa kilo.

Niwaombe wakulima wawe wavumilivu, watalipwa fedha zao hata kama watacheleweshwa lakini watapata katika muda mwafaka wa kuandaa mashamba yao.

Swali: Hebu tueleze ulipotoka kielimu, kazi na siasa.

Jibu: Elimu yangu ni shahada ya uzamili katika maendeleo ya sera niliyoisomea chuo cha Watford cha Uingereza kupitia Chuo kikuu cha Mzumbe.

Kabla ya hapo nilichukua stashahada ya juu (postgraduate diploma) ya uhusiano wa kimataifa katika Kituo cha Diplomasia na Uhusiano wa Kimataifa (CFR) jijini Dar es Salaam.

Shahada ya kwanza ya Sayansi ya siasa na Utawala niliipata Chuo kikuu huria cha Tanzania (OUT). Elimu ya juu ya sekondari niliipata katika Shule ya sekondari ya wavulana ya Songea na kabla ya hapo nilisoma Newala sekondari kidato cha kwanza hadi cha nne.

Kikazi nimefanya Jeshi la Polisi kwa miaka 10 hadi kufikia cheo cha mkaguzi. Niliamua kuacha kwa hiari yangu mwaka 2010 na ndipo nilipoamua kuingia kwenye siasa.



Chanzo: mwananchi.co.tz