Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mangula, Lowassa kuunguruma Monduli Agosti 29

13985 Pic+chadema+ccm TanzaniaWeb

Mon, 27 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Makamu mwenyekiti wa CCM Bara, Philip Mangula na Waziri Mkuu mstaafu ambaye pia in Mjumbe wa Kamati kuu Chadema, Edward Lowassa watazindua kampeni za uchaguzi mdogo wa Monduli, Jumatano Agosti 29, 2018.

Wakati Mangula atazindua kampeni za CCM, Monduli mjini, Lowassa atazindua kampeni za Chadema eneo la Mtowambu katika uchaguzi mdogo utakaofanyika Septemba 16.

Akizungumza na Mwananchi Digital leo Agosti 26, 2018 katibu mwenezi wa CCM Mkoa Arusha, Shaaban Mdoe amesema tayari maandalizi ya uzinduzi wa kampeni yamekamilika.

"Makamu mwenyekiti wetu (Philip) Mangula ndiye atazindua kampeni na tunaomba wanaCCM kujitokeza ili kuonyesha umoja na mshikamano wetu," amesema.

Mgombea ubunge wa CCM, Julius Kalanga amesema amejiandaa na wana CCM kutetea jimbo hilo ambalo alijiuzulu akiwa mbunge wa Chadema.

"Tutazindua kampeni Jumatano na nina uhakika wa ushindi kwani CCM ni chama imara ambacho kinakubalika sana Monduli," amesema.

Naye Chadema, mwenyekiti wa Chadema Mkoa Arusha, Aman Golugwa amesema wamejipanga Jumatano Agosti 29 kuzindua kampeni kwa kishindo.

"Tutakuwa na viongozi kadhaa akiwamo Lowassa ambaye ni mbunge mstaafu wa Monduli na tuna uhakika wa ushindi tena Monduli," amesema.

Golugwa amesema chama hicho kinajua michezo michafu ambayo inaendelea kufanywa na CCM, lakini wanataka dunia ijue CCM haikubaliki tena.

"Kuna figisu figisu nyingi hata hizi za wagombea udiwani kupita bila kupingwa lakini wasifikiri Chadema itakufa," amesema.

Katika uchaguzi wa Monduli vyama vinane vinashiriki Chadema wamempitisha kugombea diwani wa Lepurko, Yonas Laizer.

Kata hiyo ndiyo anakotoka Kalanga ambaye pia alikuwa diwani wa kata hiyo hadi mwaka 2015 akiwa CCM na kujiunga na Chadema.

Wagombea wengine katika jimbo hilo ni Omar Kawanga (DP), Feruzi Juma (NRA), Simon Ngilisho (Demokrasia Makini), Fransis Ringo (Aada-Tadea), Elizabeth Salewa (AAFP) na Wilfred Mlay (ACT-Wazalendo).

Chanzo: mwananchi.co.tz