Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mamia wajitokeza kumdhamini JPM

24732 Pic+ccm Mamia wajitokeza kumdhamini JPM

Fri, 19 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MAMIA ya wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Dodoma wamejitokeza kumdhamini mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho katika uchaguzi mkuu, Rais John Magufuli.

Rais Magufuli juzi asubuhi, alichukua fomu ya kutetea nafasi yake na kuipeleka kwa Katibu wa CCM, Mkoa wa Dodoma ili kumsaidia kutafuta wadhamini ndani ya chama.

Miongoni mwa wanachama hao ni pamoja na mamalishe, vijana, wajasiriamali, wanavyuo na waendesha bodaboda.

Akizungumza baada ya kuyapokea makundi hayo, Katibu huyo, Jamila Yusuph, alisema Rais Magufuli, amewakabidhi fomu yake ili kumsaidia kutafuta wadhamini.

Alisema, fomu hiyo inatakiwa kusainiwa na wadhamini 250, hivyo wanachama wanaohitaji kumdhamini, wanatakiwa kufika katika ofisi hiyo ili kupata fursa hiyo.

“Kwa kweli mhweshimiwa Rais, ametushtukiza, hakuna aliyekuwa anafahamu ujio wake, lakini na sisi kama chama lazima tuonyeshe kuwa hatutamwangusha kwa kujitokeza kwa wingi kumdhamini, lakini hata katika uchaguzi kumpigia kura nyingi na mkoa wetu uwe namba moja kwa wingi wa kura za urais,” alisema.

Naye mwakilishi kutoka kundi la machinga, John Ndahani, alisema wana mdhamini Rais Magufuli kutokana na utendaji wake katika kipindi cha miaka mitano ya awamu yake ya kwanza.

Alisema, wamepata mkombozi kwa kuwa katika utawala wake walifanya kazi bila usumbufu tofauti na ilivyokuwa kabla ya utawala wake.

“Katika uongozi wa Magufuli, tumefanya biashara bila usumbufu hakuna mtu aliyetusumbua kutokana na kila mmoja wetu kupatiwa kitambulisho kwa gharama nafuu ya Sh. 20,000 kwa mwaka,” alisema Ndahani.

Naye Hawa Mbogoni, mwakilishi wa kundi la mamalishe alisema mgombea wao, ni mmoja ndani ya chama na ambaye ni Rais Magufuli, na wanapendekeza wanachama wengine wasijitokeze kumpinga.

“Tunapenda Magufuli apite bila kupingwa, ili aitetee nafasi yake mwenyewe bila kupingwa na mwana CCM yeyote, ili amalizie awamu yake ya pili na kutuletea maendeleo zaidi ya haya,” alisema.

Mwakilishi kutoka wanavyuo wa mkoa wa Dodoma Jackson Mathias, alisema kuwa wameamua kumdhamini Rais Magufuli pamoja na kumchangia kiasi kidogo cha fedha kwa ajili ya kulipia fomu yake.

“Sisi katika awamu hii ya Magufuli kama wanachuo tumesoma kwa raha sana kwani mikopo yetu imekuwa ikiingia kwa wakati na hakuna migomo tena sasa tumeona kiasi kidogo cha fedha zetu za chakula tumchangie ili aweze kulipia fomu yake wakati huu anapojipanga kutetea nafasi yake,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live