Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo muhimu kujua uchaguzi mdogo Konde, udiwani kata sita

38f0b0b8e4a4851699e32bc3701284e4 Mambo muhimu kujua uchaguzi mdogo Konde, udiwani kata sita

Thu, 1 Jul 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

KITI cha Ubunge katika Jimbo la Uchaguzi la Konde lililopo katika Wilaya ya Micheweni mkoa wa Kaskazini Pemba kipo wazi kufuatia kifo cha aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Khatib Said Haji.

Mkurugenzi wa Uchaguzi Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Dk Wilson Mahera alitoa taarifa kwa umma kuhusu uwepo wazi wa kiti hicho cha ubunge pamoja na udiwani katika Kata sita za Tanzania Bara.

Kata hizo na halmashauri zake kwenye mabano ni Mbagala Kuu (Manispaa Temeke Dar es Salaam), Ndirigish (Kiteto Manyara), Mitesa (Masasi Mtwara), Gare (Lushoto Tanga), Mchemo (Newala Mtwara) na Chona (Ushetu Shinyanga).

Kwa mujibu wa kifungu cha 37 (3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura 343 inapotokea kiti cha ubunge kuwa wazi Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania humtaarifu kwa njia ya barua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi kumfahamisha juu ya uwepo wa nafasi wazi katika kiti cha ubunge.

Kwa upande wa kiti cha udiwani, waziri mwenye dhamana ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) humtaarifu kwa barua Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi juu ya uwepo wa nafasi wazi za udiwani katika kata husika za Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa Dk. Mahera Tume ilipokea barua hizo na kwamba kwa mujibu wa Kifungu cha 37 (1) (b) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi Sura 343 na Kifungu cha 13 (2) cha Sheria ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa Sura ya 292, maandalizi kwa ajili ya chaguzi hzio ndogo yanaendelea.

Lakini je, ni akina nani watakaopiga kura katika uchaguzi huo mdogo wa ubunge Jimbo la Konde na udiwani katika kata sita za Tanzania Bara ambao kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Uchaguzi utafanyika tarehe 18 Julai mwaka huu wa 2021?

Kuhusu wanaostahili kupiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa madiwani hapana shaka kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi itaratibu na kusimamia uendeshaji wa chaguzi hizo ikitumia Daftari la Kudumu la Wapiga Kura lililotumika wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020..

Hivyo Wapiga Kura watakaohusika ni wale waliojiandikisha katika Daftari la Kudumu la Wapiga Kura, walio na kadi za kupigia kura au vitambulisho mbadala (kwa kadiri ya maelekezo ya Tume) na ambao ni wakazi wa kawaida wa maeneo husika kwenye kata zinazofanya uchaguzi.

Kwa Uchaguzi wa Ubunge katika Jimbo la Konde, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) inaratibu na kusimamia uendeshaji wa uchaguzi huo ingawa daftari litakalotumika wakati wa upigaji kura ni lile la Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC).

Hii ni kutokana na masharti ya Kifungu cha 12 A (1) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi kinachoeleza kuwa kwa madhumuni ya uchaguzi rais na wabunge, Tume ya Taifa ya Uchaguzi itatumia Sheria ya Uchaguzi ya Zanzibar.

Aidha Kifungu cha 12A (2) kinaitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi kuandikisha wapiga kura ambao wana sifa za kumpigia kura Rais wa Jamhuri ya Muungano.

Hivyo kwa tafsiri hiyo wakazi wa jimbo la Konde walioandikishwa kwenye Daftari la Wapiga Kura la Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) watakuwa na haki ya kupiga kura kwa ajili ya kumchagua mbunge wao.

Mbunge wa Jimbo la Uchaguzi la Konde ni miongoni mwa wabunge 50 wa Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa kadiri ya muundo wa wabunge wa aina sita wanaounda bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wakiwemo wabunge wa kuchaguliwa na wananchi.

Katika kuelekea uchaguzi huo mdogo wa Jimbo la Konde, Tume ya Taifa ya Uchaguzi imezialika asasi na taasisi za ndani ya nje kutuma maombi kwa ajili ya utazamaji wa uchaguzi na hii ni katika kutekeleza misingi ya kidemokrasia inayolenga kuwa na uchaguzi wa wazi.

Aidha sambamba na watazamaji wa uchaguzi wa ndani, Tume pia imeruhusu kwa mujibu wa sheria vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi huo kwa kuweka mawakala wa uchaguzi katika vituo vyote vya kupigia kura.

Mawakala wa vyama vya siasa watashiriki katika uchaguzi baada ya kukamilisha taratibu zote ikiwa ni pamoja na kula kiapo na jukumu lao ni kulinda maslahi ya vyama vyao na wagombea, pamoja na kuhakikisha kuwa uchaguzi unafanyika katika hali ya utulivu na amani.

Kwa mujibu wa ratiba ya uchaguzi huo mdogo iliyotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi uteuzi wa wagombea katika uchaguzi huo utafanyika tarehe 27 Juni na kufuatiwa na kipindi cha kampeni kati ya Juni 28 hadi Julai 27, ikiwa ni siku moja kabla ya siku ya kupiga kura, yaani Julai 18 mwaka huu.

Ikumbukwe kuwa vituo vitakavyotumika kupigia kura ni vile vile vilivyotumika kupigia kura wakati wa Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 ambavyo vimo katika mitaa, vitongoji na vijiji katika kata zote za mikoa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Hapana shaka kuwa katika risala ya Mwenyekiti wa Tume itakayotolewa siku moja kabla ya uchaguzi itaelekeza mambo yote muhimu ya kuzingatiwa na wasimamizi wa uchaguzi ili kufanikisha uchaguzi ulio huru na haki.

Mambo hayo ni pamoja na kutoa kipaumbele kwa makundi maalumu ya wapiga kura wenye mahitaji maalumu ya walemavu, wazee, wagonjwa, wajawazito, akina mama wenye watoto wachanga na wanaonyonyesha.

Shime wakazi wa Jimbo la Konde pamoja na kata zitakazofanya uchaguzi wa madiwani Tanzania Bara kujitokeza wakati wa kampeni na hatimaye siku ya uchaguzi ili waweze kupiga kura kwa mustakabali wa maendeleo yao.

Kumbuka kura yako ni sauti yako. Nenda ukapige kura

Chanzo: www.habarileo.co.tz