Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo moto uchaguzi

9ee4bfe020d9eff8a949c76f5d4a6ae3 Mambo moto uchaguzi

Thu, 27 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

WAKATI harakati za uchaguzi mkuu wa rais, wabunge na madiwani zikiwa zimeanza, wagombea wa nafasi hizo wamemiminika kuwekeana pingamizi huku vimbwanga vya kila aina vikionekana.

Sambamba na hayo viongozi wa dini na Tume ya Taifa ya Uchaguzi(NEC) wametoa neno kwa wagombea.

Pingamizi

Katika pingamizi hadi jana saa 10:00 jioni ambao ndio mwisho wa kupokea, NEC kupitia kwa Mkurugenzi wake, Dk Wilson Charles alisema hakukuwa na chama chochote kilichowasilisha pingamizi ya urais.

Kwa upande wa ofisi ya Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kibamba na Ubungo Mkoani Dar es Salaam imepokea pingamizi sita kutoka kwa wagombea wa vyama vya siasa vilivyoshiriki uchukuaji na urejeshaji wa fomu za uteuzi.

Hayo yalibainishwa na Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kibamba na Ubungo, Beatrice Dominic, alipozungumza na HabariLEO jana ofisini kwake.

Beatrice alisema vyama 17 kati ya 19 ndivyo vilivyorejesha fomu na vyama vingine viwili kikiwemo Chama cha DP na AFP havikurejesha fomu zao.

Msimamizi huyo wa uchaguzi alisema jumla ya pingamizi sita ziliwasilishwa ofisini kwake kati ya juzi na jana na yeye anatakiwa kutoa majibu ya pingamizi hizo ndani ya saa 48.

Kwa mujibu wa Beatrice, vyama vilivyoweka pingamizi ni Chama cha Demokrasia Makini kilichoweka pingamizi dhidi ya NCCR-Mageuzi Ubungo, Ada Tadea Kibamba kimeweka pingamizi dhidi ya ACT-Wazalendo Kibamba, Chama cha Mapinduzi (CCM) Ubungo kimeweka pingamizi dhidi ya ACT-Wazalendo na Chadema Ubungo, CCM Kibamba kimeweka pingamizi dhidi ya ACT-Wazalendo na Chadema Kibamba na CCM Ubungo kimeweka pingamizi dhidi ya NCCR-Mageuzi.

Wakati huohuo, Chadema mkoa wa Katavi imeweka pingamizi katika majimbo matatu ya uchaguzi na Kata 10 mkoani Rukwa.

Aidha, hakuna vyama vya siasa vilivyoweka pingamizi katika majimbo ya uchaguzi ya Nkasi Kaskazini, Nkasi Kusini, Sumbawanga Mjini wala Jimbo la Kwela.

Mkoani Rukwa Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Kwela ,Nyangi Msemakweli amelieleza gazeti hili kuwa hakuna pingamizi kwa wagombea wa ubunge wala wagombea udiwani katika Kata zote 27.

Hivyo wagombea wanne watangazwa kuwa na sifa za kuwania ubunge katika Jimbo la Kwela ambao ni Deus Sangu (CCM), Naftali Ngongo (Chadema) na Jailos Pengo.

Mwingine ni mgombea wa CCK ambaye hakuweza kukumbuka majina yake mara moja.

Naye, Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Sumbawanga Mjini , Jacob Mtalitinya amewatangaza rasmi wagombea ubunge sita kuwa wamekidhi vigezo kutokana na kutowekewa pingamizi.

Wagombea hao ni Aesh Hilaly (CCM) ambaye anatetea nafasi hiyo kwa mara ya tatu , Doris Kafuku (NCCR - Mageuzi) akiwa mwanamke pekee, Shadrack Malila (Chadema), Suleiman Sinani (ACT -Wazalendo),Julius Mizengo (CUF) na Michael Lubava Jimbo la Nkasi Kaskazini Ally Kessy (CCM) anayetetea nafasi hiyo mara ya tatu.

Wengine ni January Yamsebo(ACT -Mageuzi), Aida Khenani na Dickson Konga (NCCR -Mageuzi ) Nkasi Kusini Vicent Mbogo (CCM) na Alfred Sokota (Chadema).

Mkoa wa Katavi , Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Katavi, Rhoda Kunchela ametangaza kuweka pingamizi katika majimbo matatu ya uchaguzi kwa nafasi ya ubunge na Kata 10 kwa nafasi ya udiwani kwamba wagombea wa vyama hivyo wameenguliwa bila sababu za msingi.

Vimbwanga

Kwa upande wa vimbwanga vilivyobainika hadi sasa ni pamoja na mmoja wa wagombea kukwapua fomu za mgombea mwenzake na kudumbukia nazo mtoni.

Pamoja na kituko hicho, mgombea ubunge wa Chama cha ACT-Wazalendo Faraji Msagati alilazimika kuvaa vazi la kike la baibui na juba kwa kile kilichodaiwa kukwepa maofisa wa uhamiaji waliopanga kumkamata kabla hajajibu pingamizi alilowekewa.

Vituko vingine ni pamoja na mgombea kunusurika kuporwa begi lenye fomu zake alizokuwa akizirudisha kwa Msimamizi wa Uchaguzi, mgombea kutekwa na watu wasiojulikana pamoja na kitendo cha kughushi barua ya chama ili kupata idhini ya kuomba kupitishwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa mgombea.

Mkoani Rukwa, Jeshi la Polisi linamshikilia kwa mahojiano mkazi wa Majengo Sumbawanga akidaiwa kukwapua fomu za uteuzi za mgombea udiwani kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Emanuel Fungameza.

Fungameza alikuwa akizirejesha fomu hizo juzi asubuhi kwenye Ofisi za Kata ya Senga ambako anagombea nafasi ya udiwani.

Mtuhumiwa huyo baada ya kukwapua fomu hizo alikimbia na kujitosa mtoni na kusababisha zirowe maji. Hata hivyo alinusurika kifo baada ya kupigwa na watu wenye hasira.

Kamanda wa Polisi mkoa wa Rukwa, Justine Masejo hakuwa tayari kuyataja majina ya mtuhumiwa kwa sababu za kiupelelezi.

Mwenyekiti wa Chadema mkoa wa Rukwa, Shadrack Malila akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu alisema mgombea huyo alifanikiwa kuzirejesha fomu hizo katika Ofisi ya Kata Senga na amepitishwa kugombea nafasi ya udiwani.

Akielezea mkasa huo mgombea huyo Fungameza alilieleza gazeti hili kuwa mkasa huo ulitokea juzi saa 3:00 asubuhi wakati akirejesha fomu hizo ambapo akiwa kwenye msafara wake wa pikipiki tatu ambapo pikipiki ya mwisho ndio ilikuwa na mtu wake wa karibu aliyezibeba fomu hizo.

Walipovuka daraja la Senga walikutana na pikipiki kubwa ikiwa na watu wawili. “Tukawapita watu hao ambapo waliigonga pikipiki ya mwisho na kusababisha taharuki ambapo abiria wa pikipiki hiyo alikwapua fomu, dereva wa pikipiki alitimka na pikipiki yake huku aliyekwapua fomu akikimbilia porini"

Wakiwa kwenye msafara walibaini pikipiki ya mwisho iliyokuwa na fomu haionekani na wakaamua kugeuza ndipo waliposikia yowe na mtu akomba msaada.

“Tukakimbia ambako sauti inatokea, mara tukamuona mwanamume anajitosa majini huku wenzetu wawili waliokuwa kwenye pikipiki ya mwisho wawili nao wakijitosa majini na kumdhibiti aliyetunyang’anya fomu ambazo tayari zilirowa. Tukazianika juani na kutoa taarifa polisi,” alisema.

Kutokana na mkasa huyo, aliyekuwa Mstahiki Meya wa Manispaa ya Sumbawanga, Justine Mwaniwasa anatuhumiwa kumtuma mwanamume huyo kunyang'anya fomu hizo.

Fungameza(Chadema) na Mwanisawa (CCM)wanagombea udiwani katika Kata ya Senga Manispaa ya Sumbawanga.

Alipohojiwa Mwanisawa na gazeti hili kuhusiana na tuhuma hizo alikana akisema zina lengo la kumchafua kisiasa.

Kwa upande wa kituko cha mgombea wa Pangani, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na chama chake cha Act-Wazalendo, mgombea wao wa wa mwanamume aliwekewa pingamizi na mgombea wa CCM Jumaa Aweso na ndipo alipolazimika kuvaa baibui, nikabu na hijabu ili kwenda NEC kuwasilisha majibu ya pingamizi alilowekewa.

Kwa upande wa mkoani Pwani, Polisi mkoani humo wanamshikilia mtu mmoja ambaye jina lake limehifadhiwa kwa tuhuma za kumteka mgombea udiwani kupitia Chadema kata ya Kerege Martin Anney (35).

Kamanda wa polisi mkoani Pwani, Wankyo Nyigesa alisema mtuhumiwa alikuwa na wenzake watatu ambao walikimbia na bado wanatafutwa.

Nyigesa alisema kuwa tukio hilo lilitokea Agosti 22, mwaka huu, saa 2:00 usiku Kitongoji cha Manofu kata ya Kerege wilaya ya Bagamoyo.

"Baada ya tukio hilo tulifanya ufuatiliaji na kufanikiwa kumkamata mtuhumiwa mmoja mwanaume eneo la Janga Mlandizi wilaya ya Kibaha. Pia tulikamata gari aina ya Toyota Rav 4 inayodaiwa kutumiwa na watuhumiwa hao kufanya tukio hilo,” alisema upelelezi unaendelea.

Aidha, polisi mkoani Morogoro, inawashikilia watu watatu, wanaodaiwa kuwa ni wanachama wa Chadema wilaya ya Morogoro kwa tuhuma za kutengeneza barua bandia ya utambulisho kutoka Chama cha Sauti ya Umma (SAU) na kutaka kuchukua fomu ya kugombea ubunge Jimbo la Morogoro Mjini.

Kamanda wa Polisi wa mkoa wa Morogoro , Wilbroad Mutafungwa alisema watu hao walikamatwa juzi baada ya Polisi kupokea taarifa kutoka kwa Msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Morogoro mjini, Sheilla Lukuba mara baada ya kutilia shaka barua ya utambulisho kutoka kwa Edgar Msigwa aliyedai kuwa ni mwanachama wa chama cha SAU .

Alisema walifika katika ofisi za msimamizi huyo na kumhoji mtu huyo na walipokagua barua yake ilibainika ina mapungufu na hata uchunguzi wa Polisi ulibaini kuwa chama hicho hakina ofisi ya wilaya au mkoa Morogoro.

Baada ya kumhoji alikiri kuwa yeye si mwanachama wa SAU bali alipewa barua hiyo na Christian Daniel ambaye ni mratibu wa uchaguzi wa madiwani wa Manispaa ya Morogoro pamoja na dereva wa mgombea ubunge jimbo la Morogoro mjini Devotha Minja kupitia Chadema aliyetambulika kwa jina moja la David.

Watuhumiwa wote watatu wanaendelea kuhojiwa ili kujua sababu za kufanya udanganyifu huo, jambo ambalo linakwenda kinyume na sheria za nchi na linalenga kuhatarisha amani.

“Tunamshikilia huyu ndiye alitumia gari ya mbunge huyo kumbeba Edgar Msigwa ambaye alikuwa na barua ya kughushi kwa hiyo tumemkamata yeye pamoja na gari aliyoitumia,”alisema.

Katika hatua nyingine, Mutafungwa alidhibitisha kukamatwa kwa mtu mmoja ambaye alifanya jaribio ya kupora mkoba wenye fomu za kugombea ubunge wa Jimbo la Morogoro Mjini za Mgombea Chama cha Wananchi (CUF).

Alisema mtuhumiwa huyo alikamatwa na polisi waliokuwa eneo la jengo la Msimamizi wa Uchaguzi wa jimbo hilo baada ya kuarifiwa kufanyika kwa kitendo hicho wakati mgombea akirejesha fomu zake na watuhumiwa wa tukio hilo wameshakamatwa na wanaendelea kuhojiwa.

Baada ya kumkamata mtuhumiwa huyo akiwa na begi hilo, fomu hizo zilitambuliwa na mhusika, Abeid Mlapakolo ambaye baada ya kuzikagua alisindikizwa kwenda kuzirudisha kwa msimamzi wa uchaguzi wa jimbo hilo kwa muda uliopangwa.

Kauli ya NEC

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Uchaguzi(NEC), Dk Wilson Mahera amesema hakuna mgombea wa ngazi yoyote anakatwa kwa matakwa ya mtu.

Dk Mahera ameyasema hayo alipozungumza na waandishi wa habari kuhusiana na tabia ya malalamiko yanayoenea kuwa kuna watu ambao wamekatwa.

Aidha, amevikumbusha vyama vya siasa na wagombea wa ngazi zote kuzingatia maadili ya uchaguzi ambayo yamenza kutumika jana.

Alisema: “kumekuwapo na dhana potofu ya watu wanakatwa, suala la uteuzi huwezi kukata mtu kwa matakwa yako kwa sababu Tume ya Taifa ya Uchaguzi inafanya kazi kwa kuzingatia sheria, taratibu na kanuni.”

“Tumeweka kabisa sifa za wagombea katika ngazi ya urais, ubunge na udiwani lakini pia tumeweka pia masharti ya uteuzi katika ngazi zote, mtu ukiona hajateuliwa ina maana hajatekeleza masharti, kwa hiyo ni vyema kupata sababu za kutoteuliwa.”

“Lakini hii tabia ya watu kuingia kwenye uchaguzi na kabla ya uchaguzi haujafanyika tayari anajiona ni mshindi hii ni tabia mbaya, sheria , taratibu na kanuni zitatumika kuhakikisha aliyeshinda anatangazwa. Hivyo nawasihi Watanzania msiingie kwenye vurugu ambazo hazina msingi.”

Aidha, Dk Mahera ametumia fursa hizo kuvikumbusha vymama vya siasa na wagombea wa ngazi zote kuzingatia maadili ya uchaguzi.

“ Kwa wagombea wote, maadili ya uchaguzi 2020 kwa ajili ya urais, wabunge na diwani maadali yanaanza kutumia rasmi leo(jana), kwahiyo sheria na adhabu zinazotokana na hayo maadili zinaanza kutumia leo kwa hiyo hawana uhuru tena.

“Lakini pia wanapaswa kuzingatia sheria za nchi kwani zipo pia na hazijasimama, zitaendela kuwepo. Ukihamasisha vurugu ujue kuna sheria zitatumika

Aidha, amekemea tabia ya baadhi ya vyombo vya habari kutoa matangazo ya wabunge na madiwani wanaodaiwa kushinda bila kupingwa bila kupewa taarifa hizo na tume.

“Kitendo hiki ni kinyume na sheria za uchaguzi na kina maana ya kupoka uhuru na majukumu ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi.”

“Kwa mujibu wa kifungu cha 40 (2) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, pingamizi linaweza kuwekwa kwa mgombea wa ubunge kama zuio kwa wagombea aliyeteuliwa kuanzia saa 10 kamili jioni siku ya uteuzi maana yake jana (juzi) hadi saa 10 kamili jioni siku inayofuatia baada ya siku ya uteuzi yaani leo(jana), hivyo kutangaza mtu ameshinda inaweza kupeleka uvunjifu wa amani pale ambapo mtu atawekewa pingamizi na asionekane ameshinda.”

Alisema Tume haitasita kuichukulia hatua za kisheria kwa chombo chochote cha habari kitakachoenda kinyume na sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi.

Chanzo: habarileo.co.tz