Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mambo manne yaliyoibuka mkutano wa wapinzani Dar

49314 Mkutanopiuc

Fri, 29 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Viongozi wakuu wa vyama vya upinzani juzi jioni walikutana jijini Dar es Salaam kujadili mambo manne, Mwananchi limeelezwa.

Kikao hicho kilifanyika ikiwa ni muda mfupi baada ya Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam kuzuia mkutano wa ndani wa ACT-Wazalendo uliokuwa ufanyike katika ukumbi wa PR wilayani Temeke.

Taarifa za ndani kutoka katika kikao hicho zinaeleza kuwa mambo yaliyojadiliwa ni uwepo wa Tume Huru ya Uchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa 2020, uchaguzi wa serikali za mitaa, ACT-Wazalendo kutishiwa kufutwa na Msajili wa Vyama vya Siasa pamoja na sheria mpya ya vyama vya siasa.

Baadhi ya viongozi walioshiriki mkutano huo ni mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe; katibu mkuu, Dk Vicent Mashinji; naibu katibu mkuu wa chama hicho-Zanzibar, Salum Mwalimu; kiongozi wa ACT, Zitto Kabwe na mwanachama wa chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad.

Hata hivyo, alipoulizwa kuhusu kilichojadiliwa katika kikao hicho Zitto alisema, “tumefanya kikao cha ndani, ni kikao cha kawaida cha vyama 10. Ni kikao cha mahusiano kuhusu masuala mbalimbali.”

Alisema, “kikao hiki ni cha mwendelezo wa kile ambacho vyama vilikutana kujadili muswada (wa Sheria ya Vyama vya Siasa) ambao sasa umesainiwa kuwa sheria. Ni kikao cha kawaida hatukuita wanahabari, ni mwendelezo wa vikao vyetu vya kawaida.”

Related Content

Ingawa kilichojadiliwa na kuzungumzwa hakikuwekwa wazi, lakini taarifa ambazo Mwananchi ilizipata zinaeleza kuwa vigogo hao walijifungia kujadili mambo hayo manne.

Tume huru ya uchaguzi

Kwa nyakati tofauti vyama vya upinzani vimekuwa vikishinikiza kuwepo kwa Tume Huru ya Uchaguzi kwa maelezo kuwa ndio suluhisho la kumaliza mvutano na lawama zinazoibuka wakati wa uchaguzi. Moja kati ya mambo yanayokosolewa ni watendaji wa Serikali wakiwemo wakurugenzi wa manispaa na wilaya kuwa wasimamizi wa uchaguzi na watangazaji wa matokeo huku wajumbe wa Tume ya Uchaguzi (Nec) wakiteuliwa na rais.

Kufutwa kwa ACT

Hoja ya tishio la ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kutishia kuifuta ACT na kuipa siku 14 kuwasilisha maelezo kwa nini isifutiwe usajili ilijadiliwa.

Chama hicho kinadaiwa kufanya vitendo vya uvunjifu wa sheria vya kuchoma moto bendera za CUF baada ya mahakama kutoa hukumu katika kesi namba 23 ya 2016 iliyomtambua Profesa Ibrahim Lipumba kuwa mwenyekiti halali.

Sheria vyama vya siasa

Taarifa zinaeleza kuwa viongozi hao walijadili Sheria ya Vyama vya Siasa ambayo Rais John Magufuli ameisaini na kuchapishwa kwenye gazeti la Serikali la Februari 22.

Tayari Chadema imeshaweka hadharani nia yake ya kuipinga sheria hiyo mahakamani kwa maelezo kuwa ni mbaya kutokana na vifungu vyake kukiuka Katiba, misingi ya utawala bora pamoja na mikataba mbalimbali ya kimataifa.



Chanzo: mwananchi.co.tz