Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Malalamiko ya mawakala yaendelea kutawala

17717 Pic+malalamiko TanzaniaWeb

Mon, 17 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Arusha. Malalamiko ya mawakala wa vyama vya siasa, hasa vya upinzani, kukosa barua za utambulisho ili waingie vituoni kusimamia kura za wagombea wao, yalitawala uchaguzi mdogo katika majimbo ya Ukonga na Monduli uliofanyika jana.

Kutokana na tatizo ambalo liliibuka asubuhi na kutatuliwa saa chache baadaye, mawakala hao walilazimika kubaki nje ya vituo kusubiri barua hizo, wakati viongozi wa vyama vya siasa na wagombea wakifuatilia kwa wasimamizi wa uchaguzi.

Matukio kama hayo yalijitokeza pia katika uchaguzi mdogo wa Kinondoni uliofanyika Februari na kusababisha viongozi wa Chadema na wafuasi wao kuazimia kumfuata msimamizi wa uchaguzi ili kupatiwa barua hizo jambo lililosababisha polisi kutumia nguvu kuwazuia.

Katika tukio hilo, mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji, Akwilina Akwilini alipigwa risasi akiwa kwenye daladala na kupoteza maisha.

Mbali na mawakala hao, pia barua za utambulisho kwa waandishi wa habari waliokuwa wanaripoti uchaguzi huo zilizoombwa tangu Ijumaa, zilipatikana jana Jumapili saa 3:30 asubuhi wakati shughuli za upigaji kura zilianza tangu saa 1:00 asubuhi.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Dk Athumani Kihamia alisema amepokea malalamiko kuhusu mawakala kukosa barua za utambulisho Ukonga na Monduli na kwamba alikuwa akiyafanyia kazi haraka.

Alisema alipata malalamiko hayo kutoka kwa Naibu Katibu Mkuu wa Chadema, John Mnyika na alifuatilia kwa msimamizi wa uchaguzi wa Jimbo la Ukonga na Monduli alikokuwa.

“Hata huku Monduli niliko, lilikuwapo, nimelifanyia kazi mimi mwenyewe na sasa kila kitu kinakwenda sawa. Hata hiyo, Mnyika hajarudi kwangu kwa hiyo ni dhahiri hakuna tena tatizo, maana nilimweleza kama bado kuna shida anijulishe,” alisema Dk Kihamia.

Hata hivyo, baadaye mchana Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage alipotembelea vituo vya uchaguzi vya Jimbo la Ukonga, alikanusha madai kuwa mawakala wamezuiliwa kuingia vituoni huku akikiri kuwapo na idadi ndogo ya wapigakura.

Alisema katika Jimbo la Monduli lenye vituo 256, ni mawakala wanne tu walizuiliwa kuingia vituoni na ni kwa sababu za msingi.

“Walizuiliwa kwa kuwa hawakutambuliwa na msimamizi. Hawakuapishwa walikwenda kwa niaba ya wengine. Hizi habari zinazosambazwa kuwa mawakala wote Monduli wamezuiliwa si za kweli, watu wasisambaze taarifa ambazo hawana uhakika nazo,” alisema.

Mgombea Chadema alia rafu

Mapema asubuhi, mgombea ubunge wa Chadema Jimbo la Ukonga, Asia Msangi aliilalamikia NEC kuhusu mawakala wa chama hicho kuzuiwa kuingia katika vituo vya kupigia kura na kwamba katika vituo vingi, mawakala wake hawakuwa wameruhusiwa kuingia.

“Mpaka sasa (saa 4:45 asubuhi) sijapiga kura ninahangaika na suala la mawakala wangu kwa sababu mpaka sasa hawajaingia vituoni.

“Nimezungumza na msaidizi wa mkurugenzi (msimamizi wa uchaguzi) anasema waingie, kule kwenye vituo wasimamizi wanawazuia kuingia bila barua, yaani ni mkanganyiko ambao naona wazi umetengenezwa makusudi,” alidai Msangi.

Wasimamizi wa uchaguzi kituo cha Pugu Mnadani waliwaondoa mawakala saba wa Chadema, NLD na NCCR ambao hawakuwa na barua za utambulisho.

Mwandishi wa Mwananchi alishuhudia mmoja kati ya mawakala hao, Gabriel Samson akiondolewa na polisi watano waliopo kituoni hapo dakika chache baada ya kufika.

“Askari naomba uniondolee huyu mtu hapa, mwondoe tafadhali, nimesema hatukuhitaji hadi uwe na barua ya mtendaji wa kata,” alisikika akisema mmoja wa wasimamizi wa kituo na polisi wakatekeleza amri hiyo.

Akizungumzia kitendo hicho, Samson alidai hiyo ni hujuma.

“Tulipokula viapo tuliambiwa viapo na fomu zote tutazikuta kituoni, leo tunafika kituoni hapa tunaambiwa haturuhusiwi hadi barua na hati za viapo. Tunarudi kwa mtendaji wa kata hayupo ofisini,” alisema Samson akiwa na mawakala wengine sita wa NLD na NCCR Mageuzi.

Hata hivyo, kituoni hapo kulikuwa na mawakala wawili, Elick Mgasha (Sau) na Albert Modest (AAFP) ambao walioonyesha barua zao za utambulisho, wakisema hakukuwa na usumbufu wowote wakati wa kufuatilia barua hizo kwa mtendaji wa kata.

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi kituoni hapo, Mustapha Zayumba alisema hakuna wakala aliyeruhusiwa kuingia kituoni hapo bila barua ya mtendaji wa kata.

“Hata mawakala saba wa CCM tumewaondoa, hawakuwa na barua ya mtendaji wa kata, wameondoka kuzifuata, hakuna wakala anayeonewa hapa ila utaratibu lazima ufuatwe,” alisema Zayumba.

Dakika chache baadaye, lilionekana kundi la mawakala wa CCM waliojikusanya pembeni na walipohojiwa walisema wanafuatilia barua hizo.

Mawakala hao ni Mwajuma Gobel, Salim Said, Nicodem Mganga, Jesca Roma, Upendo Ndomba na Kilopola Mohamed.

Hata hivyo, Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, Msongela Palela alipoulizwa na kwa simu alisema wasimamizi wa vituo vyote wanatakiwa kuwaruhusu mawakala kuingia vituoni bila sharti la kuwa na barua ya mtendaji wa kata.

Aidha, mgombea udiwani wa Kaya, Kata ya Vingunguti (CUF), Mohamed Faki alisema zaidi ya mawakala wake watano hawakuwa wameruhusiwa kuingia kwenye vituo vya kupigia kura kwa kuwa hawatambuliki.

Faki alisema hafahamu kwa nini kitendo hicho kilijitokeza kwa sababu alifuata njia zinazotakiwa kuwapata.

“Tuna barua za mawakala, lakini wakifika katika vituo wanaambiwa hawatambuliki, nimeenda kituo kimoja baada ya kingine tangu saa 12 asubuhi, nahangaika kuwatafutia vituo.

Ilivyokuwa Monduli

Kutokana na tatizo hilo, mawakala wa vyama vya siasa katika vituo mbalimbali vya kupigia kura walichelewa kuingia vituoni Monduli.

John Leshuku, mkazi wa Meserani, Monduli alisema wameshangazwa majina ya mawakala kucheleweshwa vituoni wakati waliapishwa wiki moja kabla ya uchaguzi.

Viongozi wa CCM na Chadema wameeleza tatizo hilo kwa mtazamo tofauti. Wakati CCM wakisema ni dosari za kawaida, Chadema walidai ni hujuma.

Chanzo cha tatizo

Katika ufafanuzi wake, Dk Kihamia alisema tatizo kubwa linatokana na wapinzani wenyewe kutaka kubadili mawakala asubuhi wakati picha zao zinakuwa tayari vituoni.

Alisema kwa Monduli, tatizo Chadema walitaka kubadili mawakala 15 asubuhi akisema hata kama kulikuwa na dharura idadi hiyo ilikuwa kubwa.

“Nilipouliza wakasema waliopangwa wamekamatwa na polisi, nikasema twende kwenye hivyo vituo niwaone hao watu... Tatizo kubwa linatoka kwao na kila tunapofanya semina kuwaelimisha, viongozi wa juu hawaji. Kama mimi nipo, mwenyekiti wa Tume yupo, wao wana majukumu gani makubwa kuliko uchaguzi? Wanawatuma ma-junior (maofisa wadogo) wasiokuwa na uamuzi,” alisema Dk Kihamia.

Alisema uchaguzi ni sheria hivi sasa NEC haifanyi utani na kwamba ameshazungumza na Dk Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chadema ambaye amesema wakati mwingine atahudhuria mwenyewe.

Aidha, alisema kwa kuwa malalamiko hayo yanapitia kwenye vyombo vya habari, anakusudia kufanya semina ili waandishi wajue michakato ya mawakala inavyokwenda na nini chanzo cha malalamiko.

Chanzo: mwananchi.co.tz