Dar es Salaam. Usiuchukulie poa uchaguzi wa serikali za mitaa kwa sababu unaweza ukaishia jela kwa miezi 12.
Taasisi ya Policy Forum imefanya uchambuzi wa kanuni na kuainisha makosa 13 yanayoweza kusababisha mhusika kuchukuliwa adhabu katika uchaguzi wa serikali za mitaa.
Adhabu zinazotajwa kwenye kanuni hiyo ni kama mtu atathibitika kuwa na hatia atalazimika kulipa faini isiyozidi Sh300,000 au kifungo kisichozidi miezi 12 au vyote kwa pamoja.
Uchaguzi wa serikali za mitaa nchini unatarajia kufanyika Novemba 24.
Kuharibu orodha ya wapigakura au nyaraka zozote zinazohusiana na uchaguzi huo ni kati ya makosa yaliyoainishwa kwenye kanuni za uchaguzi wa serikali za mitaa ngazi ya vijiji na vitongoji ya mwaka 2019.
Kwa mujibu wa kifungu cha 48 cha mamlaka za wilaya, vijiji na mamlaka za miji pamoja na kifungu cha 45 cha mamlaka za wilaya-kitongoji, makosa mengine ni kutoa taarifa za uongo ili kupiga kura na kujiandikisha au kupiga kura zaidi ya mara moja.
Habari zinazohusiana na hii
- Wapinzani ‘watilia shaka’ milioni 19 kujiandikisha uchaguzi Serikali za mitaa
- Maelfu ya wanafunzi hatarini kutoshiriki uchaguzi
- CCM wapuliza kipenga uchaguzi Serikali za mitaa
- VIDEO: Dk Bashiru awasha taa ya 2020
Makosa mengine yaliyoainishwa kwenye kanuni hizo kwa ngazi ya vijiji, mitaa na vitongoji ya mwaka 2019 ni kumzuia msimamizi wa uchaguzi, msimamizi msaidizi wa uchaguzi, msimamizi wa kituo, mjumbe wa kamati ya rufaa au ofisa wa umma aliyeteuliwa kusimamia uchaguzi kutekeleza majukumu yake.
Kanuni hiyo inataja makosa mengine kuwa ni wasimamizi wa uchaguzi kukiuka masharti ya kiapo chao, kupatikana na karatasi za kupiga kura zaidi ya moja kwa nafasi moja inayogombewa na kuvuruga ratiba ya mikutano ya kampeni.
Kanuni hiyo inasema ni kinyume cha kanuni hiyo kwa mtu kukutwa na silaha kinyume cha sheria kwenye eneo la uteuzi wa wagombea, mikutano ya kampeni, eneo la usikilizaji wa rufaa za wagombea, kituo cha kuandikisha wapiga kura au kituo cha kuhesabu kura na kupiga kura.
Kosa jingine ni kutangaza matokeo ya uchaguzi kabla hayajatangazwa na msimamizi au msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa kituo.
Kanuni hizo hazikupita bila maoni ya viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa.
Mkurugenzi wa idara ya kampeni na uchaguzi wa NCCR-Mageuzi, Martin Mng’ong’o amesema kanuni zilizotolewa hazijawabana wala kuwapa uhuru na akabainisha kuwa Tamisemi ilikuwa rafiki kupokea maoni.
“Hata ukiwapigia simu wamekuwa wanatoa ufanunuzi na hata ukiangalia awali tarehe ya kuchukua fomu ilikuwa ni tarehe 29 pekee jambo ambalo liliwafanya kuongeza siku nyingine hadi kufikia Novemba 4, 2019,” alisema.
“Lakini mmeshuhudia kuhusu muda wa uandikishaji tuliokuwa tunaupigia kelele kuwa hautoshi hawakusikia, lakini mwisho wa siku wao wenyewe waliamua kuongeza siku na sehemu nyingine kuonekana kama walilazimika kutumia nguvu.”
Lakini, katibu wa vijana wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, Antony Kantara alisema wananchi wengi wanazijua kanuni hizo na wamekuwa wakizitumia hata kwenye chaguzi zilizopita.
“Ni jukumu la serikali za mitaa na sisi wanasiasa kuendelea kuwakumbusha wananchi na wagombea wetu kuhusu kanuni hizi, lakini wanazifahamu kwa sababu uchaguzi huu si wa kwanza,” alisema Kantara.
Mwenyekiti wa NLD, Oscar Makaidi alisema kanuni hizo zina kasoro na hazitoi haki kwa sababu mapendekezo waliyoyatoa jijini Dodoma katika kikao chao na waziri wa Tamisemi hayakuzingatiwa. “Uchaguzi hauwezi kuwa sawa kwa sababu tayari kanuni zina kasoro, hakuna hatua tunayoweza kuchukua, hakuna mahakama inayoweza kuzuia uchaguzi nchini na moja ya kisingizio kinachoweza kutolewa ni kuwa serikali imeshaingia gharama kuuandaa,” alisema Makaidi.
Kaimu katibu mkuu wa CUF-Bara, Joran Bashange amesema ndani ya kanuni hizo kuna makosa ambayo kwa mtu wa kawaida ni vigumu kuyabaini, na kwamba hakuna tarehe maalumu iliyoandikwa kwa ajili ya kuwaapisha mawakala. “Lakini pia kuna kipengele kinasema msimamizi wa uchaguzi amepewa mamlaka ya kutoa maelekezo kuhusiana na uchaguzi, hiki kinaweza kuleta shida wakati wa uchaguzi na kinaweza pia kutumiwa vibaya.
“Kwa sababu amepewa mamlaka hayo inamaanisha anaweza hata kuwaambia mawakala wengine wakae nje, lakini hadi sasa mapungufu kama yamo yalitakiwa kubadilishwa wakati wa mapendekezo,” alisema.
Naibu katibu mkuu wa Chadema-Zanzibar, Salum Mwalimu alisema yapo mambo ambayo hayako sawa katika kanuni hizo jambo ambalo liliwafanya kuomba ufafanuzi wa ziada kutoka Tamisemi ili kujua misingi wake.
“Tuliomba ufafanuzi kwa sababu hakuna namna tunayoweza kubadilisha kanuni hizo ndiyo maana mara zote tumekuwa tukijiandaa kupambana na mambo magumu,” alisema.