Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makonda awaweka matumbo joto mawaziri

MAKONDA SDZC Makonda awaweka matumbo joto mawaziri

Wed, 7 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amewaambia viongozi wa Serikali, wakiwamo mawaziri kuwa si lazima wampende.

Amesema akihitimisha ziara katika mikoa 20 ataanika udhaifu uliopo katika kila sekta. Makonda ameeleza hayo leo Jumanne Februari 6, 2024 alipozungumza na wananchi wa Laela wilayani Sumbawanga, mkoani Rukwa akiwa njiani kuelekea Mkoa wa Songwe.

Makonda ameshafanya ziara katika mikoa 13 na jana ameingia wa 14 ambao ni Songwe. Mingine aliyotembelea ni Dar es Salaam, Pwani, Tanga, Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Tabora, Shinyanga, Singida, Simiyu, Kigoma, Katavi na Rukwa.

"Tutaweka bayana udhaifu wa kila sekta, ili mtu ajitathamini, anafanya kazi yake kama inavyotakiwa? Hatuwezi kuwa tunalipwa mshahara halafu wengine hamfanyi kazi.

"Bahati mbaya wengine wamepewa wizara, badala ya kuhangaika kufanya kazi ya wizara ili kujenga heshima ya Rais (Samia Suluhu Hassan) aliyewaamini wanahangaika kutafuta vyeo na kutengeneza mitandao yao, kucha kutwa kuwalipa watu kuwasifia, wakati kwenye mamlaka yao mambo hayaendi," amesema.

Makonda aliyewahi kuwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam amesema: "Mimi mnichukie sijaja ili mnipende, nimepewa kazi ya kuwasemea wananchi na CCM, nitasema ukweli daima fitina kwangu mwiko, bahati mbaya mimi si muoga."

Januari 28, 2024 akiwa mkoani Shinyanga, Makonda alisema baada ya kuhitimisha ziara atawasilisha orodha ya watendaji wazembe kwa Rais Samia, ili kuchukuliwa hatua.

"Baada ya ziara hii nitakabidhi ripoti na hatua mtaziona, nimekula kiapo nitawapigania wanyonge wa Taifa hili, niwaambie watumishi wote wa Serikali ngazi zote, ukiboronga au kuharibu Makonda hatakutetea utabeba mzigo wako," amesema.

Kabla ya kuanza safari ya kuenda Songwe, Makonda na msafara wake walizuru kaburi la mwanasiasa mkongwe, Dk Chrisant Mzindakaya aliyefariki dunia Juni, 2021 kwa maradhi ya moyo.

Dk Mzindakaya alijizolea sifa na umaarufu katika miaka 1990 kutokana na umahiri wake wa kuibua hoja na tuhuma zilizotikisa kwenye Serikali ya Awamu ya Tatu iliyoongozwa na hayati Benjamin Mkapa na kupachikwa jina la 'mzee wa mabomu'.

Enzi za uhai wake, mwanasiasa huyo aliwahi kushika nafasi mbalimbali ndani ya CCM ikiwemo ubunge wa Kwela aliohudumu kwa miaka 45 kabla ya kustaafu mwaka 2010.

"Tuwaenzi wajane hawa tuwaheshimu na tuwape heshima ileile tuliyokuwa tukiwapa wakati waume zao wapo hai, wazee wakishaondoka na vyeo basi tunawaacha," amesema Makonda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live