Katibu wa itikadi na Uenezi Chama cha Mapinduzi CCM Paul Makonda amewataka watendaji wa serikali kujitathmini kama nafasi walizopewa zinafanya yale yaliyokusudiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kumuwakilisha kwenye kuhudumia wananchi.
Kauli hiyo ameitoa leo jijini Dar es salaam Decemba 21,2023 wakati akitoa tathmini ya ziara mbalimbali zilizofanywa na viongozi wa Chama hicho ili kuzungumza na wananchi na kujua changamoto zinazowakabili.
Amesema katika ziara hizo wameweza kuibua kero mbalimbali ambazo wanakutana nazo wananchi katika maeneo yao.
“Hizi ziara tumezifanya kwenye maeneo mbalimbali hapa nchini na tumepata kero nyingi sasa niwaombe watendaji ambao mmewekwa kumsaidia Rais mjitathmini Je? mnafaa kuwepo mlipo na Je? mnatimiza matakwa ya Rais wetu katika kuwahudumia wananchi,” amesema Makonda.
Sambamba na hayo Makonda amewataka watendaji wa shirikia la umeme TANESCO kutoa taarifa ya changamoto ya umeme wakiwa site na sio ofisini ili wananchi waweze kuelewa nini wanachozungumza.
Aidha, Makonda amewataka wananchi kujitokeza kutoa maoni yao kwenye dira ya maendeleo ya mwaka 2025-2050 ili iweze kutoa dira kwa serikali katika kupanga maendeleo na sera zake.