Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makonda awakaanga jukwaani vigogo watatu Mbeya

Makonda 0 Makonda awakaanga jukwaani vigogo watatu Mbeya

Thu, 8 Feb 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Watumishi watatu mkoani Mbeya wamejikuta katika wakati mgumu baada ya Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda kuwabana akitaka watoe ufafanuzi kwa umma kuhusu utendaji wao katika sekta wanazozisimamia.

Watumishi hao wamepata wakati huo, jana Jumatano, Februari 7, 2024 katika mkutano wa hadhara wa Makonda uliofanyika Uwanja wa Ruanda Nzovwe, jijini Mbeya katika mwendelezo wa ziara yake ya mikoa 20 ya ‘back 2 back’.

Watumishi hao ni Ofisa Utumishi Mkoa wa Mbeya, Anna Kimbute, Mganga Mkuu wa mkoa, Dk Elizaberth Nyema na Meneja wa Wakala wa Barabara za Mijini na Vijijini (Tarura) mkoani humo, Albert Kindole wanaodaiwa kushindwa kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.

Kabla ya kueleza hayo, Makonda amesema lengo la ziara yake ni kusimamia changamoto za Watanzania na atasimamia ukweli, ingawa kuna watu hawampendi.

Katika mkutano huo, Makonda alimuita Kimbute na kumhoji juu ya madai ya kuwapo kwa mtandao wa ufisadi ofisini kwake na ofisa huyo alijibu hakuna. Jibu hilo lilimfanya Makonda aulize swali jingine kama hakuna, kwanini watumishi wawili wanataka kuhamishwa?

Swali hilo lilionekana gumu kwa Kimbute ambaye alikaa kimya kidogo. Makonda amesema kuna ofisa utumishi mmoja na mhasibu anayeitwa Haule wanataka kuhamishwa.

Kimbute akajibu kuwa hajui sababu za watumishi hao kutaka kuhamamishwa, inawezekana mamlaka imewaruhusu.

Akaulizwa ni mamlaka ipi iliyowaruhusu? Ya mbingu na nchi? Akamuuliza kwanini wanahama, akimsisitizia Kimbute kusema ukweli bila kuficha kwa sababu anajua kinachoendelea.

"Kwa hiyo wewe bosi wa utumishi wa mkoa hujui, wanahamishwa hujui sababu? Je kikao kilichoketi na kuamuru wahame we unakijua?" amehoji Makonda.

Hata hivyo, ofisa huyo alishindwa kutoa majibu, jambo lililomkera Makonda aliyesema licha ya mtumishi huyo kuratibu shughuli za wafanyakazi, lakini hajui kinachoendelea.

Makonda pia alimuita mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa wa Mkoa wa Mbeya, Ndele Mwaselele ambaye amesema anazo taarifa za kuhamishwa kwa watumishi hao baada ya kupokea malalamiko.

Amesema amepokea malalamiko kutoka kwa Obokela Mwantina. "Huyu binti alikuwa katibu wa afya wa mkoa, zipo tuhuma zilizoletwa ofisi ya chama kwamba kuna genge linaloendelea linalotafuta baadhi ya miradi ya maji, Ukimwi.

"Hilo genge linahamisha watumishi akiwemo Obokela bila sababu, kabla ya hatujaanza kushughulikia suala la Obokela tukapata taarifa za watumishi wengine kutaka kuhamishwa," amesema Mwaselele.

Mwaselele amesema waliwahoji mamlaka husika kwa nini wataka kuwahamisha watumishi hao bila sababu za msingi na kwa nini miradi mitatu yenye tetesi za ufisadi zisiundiwe kamati ya kuchunguzwa.

Baada ya maelezo hayo, Makonda amesema ofisa utumishi huyo anajua kinachoendelea.

"Kila mtu akija akiwa mwaminifu kuanza kuziba mianya wanamuundia zengwe la kumhamisha haraka, nitamwambia  waziri atakuja hapa Mbeya, ili kukomesha mchwa hawa wanaotafuna fedha, mama yangu (Kimbeta) kwa kuwa sauti haitoki kakae utaandika kwa  maandishi watakapokuja kukuhoji," amesema Makonda.

Kisha akamuita Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Dk Nyema aeleze Sh700 milioni za vifaa zipo wapi au zimetumikaje, ambapo alijibiwa fedha hizo zimepelekwa katika vituo vya afya.

Makonda akamuuliza kituo cha afya cha Makongorosi kina vifaa tiba? Akajibiwa kuwa wameagiza vifaa tiba, lakini fedha walizopewa bado hazijashuka chini, jambo ambalo mwenezi huyo alishindwa kumuelewa.

"Yaani mmeshapewa, lakini bado hazijashuka, umesema zimepelekwa kwenye vituo swali hawa wana vifaatiba na wananchi wakienda wanapata huduma?

Dk Nyema akijibu,"huduma za wagonjwa wa nje wanapata, lakini huduma za upasuaji hadi vifaatiba na fedha tulipata tangu Septemba mwaka 2023.”

Kutokana na suala hilo, Makonda akamuliza kama fedha wamepewa Septemba mwaka 2023, vifaatiba viko wapi? Kisha akamuamuru Dk Nyemo kurudi katika eneo lake kuketi.

Hakuishia hapo mwenezi huyo akamuita Kindole kumueleza kuwa barabara nyingi za mtaani katika Jiji la Mbeya ni mbovu, nini mkakati wa taasisi yake katika kushughulikia kabla ya mvua kunyesha.

Katika majibu yake, Kindole amesema barabara nyingi za Jiji la Mbeya bajeti yake imeshatoka na wakandarasi wapo kazini, jambo lililoibua kelele za wananchi waliokuwa katika mkutano huo kuashiria bosi huyo wa Tarura haelezi ukweli.

"Swali langu ni moja umeona hizi kelele zote wewe ukijitathimini unafaa kuwa mtendaji wa kutafuta kura za Rais Samia,” amehoji Makonda.

Kwa mujibu, Kindole amesema takribani kilomita 18 ujenzi wake unaendelea, akisema anaweza kuzitaja endapo Makonda ataridhia, hata hivyo kelele zikaibuka tena za wananchi kuashiria maelezo anayoyatoa bosi huyo wa Tarura mkoa wa Mbeya si ya ukweli.

Kutokana na suala hilo, Makonda amesema atazungumza na Mbunge wa Mbeya Mjini, Dk Tulia Ackson ambaye ni Spika wa Bunge kujua mkakati wa kuzitengeneza barabara za mitaani, ili kulipendezesha jiji hilo.

"Nitafanya mpango wa kuonana na Dk Tulia, pia tutawasiliana na Waziri wa Tamisemi (Mohamed Mchangerwa) ili kuweka mkakati maalumu wa kulifanya Mbeya liwe jiji kweli kweli," amesema Makonda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live