Haishiwi mbwembwe au vituko unaweza kutafsiri hivyo, baada ya leo Katibu wa Itikadi wa Chama cha Mapinduzi ( CCM), Paul Makonda kutumia usafiri wa lori la mchanga wakati akiingia kwenye viunga vya wilaya ya Sengerema mkoani Mwanza akitokea Geita.
Hii si mara ya kwanza Makonda kutumia usafiri mbadala wakati akiingia kwenye mkutano au wakati akipokelewa kuingia wilaya mpya. Alianza na bodaboda, bajaji, farasi na baiskeli na leo hii Jumapili ametumia lori la mchanga.
Leo Jumapili Novemba 12, 2023 Makonda aliingia wilayani Sengerema akiwa katika lori la mchanga huku akishika sepetu.
Katika msafara huo aliambatana na wabunge wa Geita Vijijini na Sengerema aliopanda nao katika gari hilo.
Tukio hilo la Makonda liliibua shangwe kwa wananchi wa Sengerema ambapo baadhi yao walionekana wakirekodi tukio hilo kwa kutumia simu janja, Makonda alisindikizwa na waendesha bodaboda wa Sengerema.
Mbunge wa Sengerema, Hamis Tabasamu amesema, "Makonda ameamua kuingia Sengerema kwa tipa la mchanga hii inaonyesha namna anavyojua shida za wananchi. Nawaambia wananchi wa Sengerema tunamshukuru Rais Samia Suluhu Hassan daraja la Kigongo Busisi ujenzi wake unaendelea vyema," amesema Tabasamu.
Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu 'Musukuma' amesema Kanda ya Ziwa hawadanganyiki na wanamuombea Makonda katika utekelezaji wa majukumu yake.
"Tunamkubali Mama ( Rais Samia Suluhu Hassan), huku ndiko atapata kura nyingi. Kanda ya Ziwa tupo salama," amesema Musukuma.