Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Paul Makonda wa Chama cha Mapinduzi (CCM) amewaagiza viongozi wa chama hicho, kuandaa taarifa za utekelezaji wa Ilani ya CCM na kuzipeleka katika ofisi zote za Chadema kabla ya Januari 24,2024 ili kuwaonyesha Serikali inavyotekeleza majukumu yake ya kuwaletea maendeleo.
Makonda ametoa maagizo hayo, leo Jumamosi Januari 20, 2024 akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Lamore wilayani Tanga katika mwendelezo wa ziara yake ya mikoa 20 aliyoipa jina la 'back 2 back' awamu ya kwanza sehemu ya pili.
Amesema lengo la kufanya hivyo ni viongozi wa Chadema kutambua licha ya chama hicho kupanga kufanya maandamano ya amani Januari 24, 2024 basi watambue kazi kubwa inayofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi.
"Tunataka wakitaka kufanya maandamano basi watambue kuna kazi nzuri iliyofanywa na Chama cha Mapinduzi kwa mfano wakisema... oooh hawajaletea maji, nyie (CCM) mnawajibu ni kweli kulikuwa na changamoto, lakini hatua kadhaa zimechukuliwa na maji yanapatikana.
" Wao (Chadema) wakisema, lazima muwaonyeshe na upande wa kilichofanyika na Serikali, viongozi wangu wa chama andaeeni utekelezaji wa chama wapelekeeni ndugu zetu Chadema na vyama vingine vyote iwe ACT- Wazalendo, CUF au NCCR- Mageuzi leo itakuwa mara yangu ya mwisho kuizungumzia Chadema ndio maana nataka muandae taarifa,” amesema Makonda.
Hata hivyo, Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema amesema amesikia kauli ya Makonda akisema taarifa hiyo itawaongezea sababu za wao na wananchi kutaka kuandamana kupinga masuala mbalimbali ikiwemo ugumu wa maisha.
"Wanataka kutuletea taarifa gani za Ilani? za ugumu wa maisha, nauli kupanda maradufu na sukari bei juu au changamoto ya kukatika kwa umeme, tunaamini wanatuongozea sababu za wananchi kuandamana, taarifa yao itatuongezea sababu ya maandamano," amesema Mrema.
Januari 13, 2024 Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe alitangaza vuguvugu la kudai haki litakaoambatana na maandamano ya amani ili kuishinikiza Serikali kuzingatia maoni na mapendekezo ya wadau demokrasia ya vyama vingi kuhusu miswada mitatu.
Miswada hiyo ni Sheria ya Uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani, muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Muswada wa Sheria ya Marekebisho ya Sheria za Vyama vya Siasa wa mwaka 2023.
Katika hatua nyingine, Makonda amesema miongoni mwa majukumu aliyopewa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Samia Suluhu Hassan ni kuhakikisha nakuwa sauti ya wananchi wanyonge sambamba na kuwakagua watendaji wa Serikali wasiotekeleza majukumu yao na kusabanisha mkuu wa nchi kuchukiwa.
"Nimepewa kazi ya kuhangaika na kero za wananchi, sijaja kuuza sura," amesema Makonda.
Baada ya kueleza hayo, Makonda amesema Tanga hasa Hospitali ya Bombo kuna changamoto mbalimbali akimtaka Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dk Japhet Simeo kutoa majibu ya kwa nini wananchi wanaokwenda kupata huduma wanateseka.
Katika majibu yake, Dk Simeo amesema kuanzia Jumatatu hospitali ya Bombo itakuwa na uongozi mpya itakayosaidia kubadilisha safu nzima ya utendaji kazi ya hospitali hiyo.
Hata hivyo, majibu hayo hayakumfurahisha Makonda aliyemhoji tena Dk Simeo siku zote walikuwa wapi kufanya mchakato huo hadi wayafanye Jumatatu mabadiliko hayo.
Dk Simeo alijibu kuwa,"kulikuwa na changamoto zilizojitokeza kuanzia Agosti Septemba, Oktoba kulikuwa na kamati maalumu iliyokuwa ikifanya kazi na kupeleka majibu kwa mkuu wa mkoa Waziri Kindamba hivyo Jumatatu mabadiliko yatafanyika.
Makonda alimuuliza tena swali, Dk Simeo nje ya Bombo akitaja kituo kingine cha afya kinachowatesa wananchi na hajachukua hatua je amfanye nini?
"Ninazo taarifa hapa Tanga, watu wananyanyasika wanateseka, hawapati huduma, wajawazito wanajibiwa vibaya na hospitali vifaa vimeharibika watu wanakosa huduma," amesema Makonda
Akijibu swali hilo, Dk Simeo ana mwaka mmoja wa kuhudumu nafasi hiyo, lakini katika kipindi amefanikiwa kutatua changamoto katika vituo na zanahati 20 vilivyokuwa na usumbufu kati ya 23.
"Mwenezi ndani ya mwezi mmoja hivi vituo vilivyobaki ikiwemo hospitali ya Bombo," amesema Dk Simeo.
Baada ya maelezo hayo, Makonda alimpa nafasi nyingine Dk Simeo akimtaka kushugulikia changamoto ya zahanati, vituo vya afya vilivyobaki ili kuboresha huduma za afya mkoani Tanga.
"Katika maisha kuna nafasi ya pili, nitakuja tena katika taarifa nilizonazo wako baadhi ya watumishi katika zahanati au kituo cha afya hawatoi huduma bali muda wote wapo na simu wanachati, wengine wanauza dawa, nimeyabaini haya kaka (Dk Simeo ) nipo makini simamia hili," amesema Makonda.
Kisha akahamia kwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu ambaye ni mbunge wa Tanga Mjini aliyemtaka aeleza anawasaidia watu wasio na uwezo ambao wanaouguza wagonjwa ambapo ikitokea bahati mbaya wanafariki dunia wanashindwa kugomboa maiti.
"Inafika hatua ndugu hawa wanashindwa kutimiza tendo la kiimani la kuwastiri wa pendwa wao kwa wakati kwa sababu hawana fedha za kugomboa mwili, je kama waziri mwenye dhamana jambo hili umekutanalo na linawakera, unaweza kutueleza mkakati ulionao ili wananchi wapate nafasi ya kuwastiri ndugu zao,"
Akijibu suala hilo, Waziri Ummy amezitaka hospitali zote za Serikali kuacha kuzuia maiti za Watanzania," narudia mara tatu marufuku kuzuia maiti haya ndio maelekezo ya Serikali.”
"Nimeshawaambia hasa kwa Waislamu ukiona hawajachukua maiti ndani ya siku mbili basi mtu huyo hana uwezo, kwa hiyo nawataka waganga wafawidhi kuzingatia mwongozo wa Serikali wa kutozuia maiti, bali waitoe baada ya kuzika taratibu zingine zifuate," amesema Waziri Ummy.
Baada ya maelezo hayo, Makonda akiwa mbioni kuhitimisha hotuba yake alimpongeza Waziri Ummy akisema amefarijika kusikia msimamo huo na kuahidi kulisimamia jambo hilo kwa nguvu zote.