Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amesema yeye ndiye Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) aliyevunja rekodi kwa kukaa katika nafasi hiyo kwa muda mfupi, lakini ameacha alama isiyofutika.
Mbali na hayo, ametaja maeneo sita atakayoyasimamia katika uongozi wake ambayo ni kuweka misingi ya haki, uwajibikaji, utalii, uchumi, utulivu na usalama na usikilizaji wa kero za wananchi.
Makonda ametoa kauli hiyo leo, Jumatatu ya Aprili 8, 2024 jijini Arusha alipokuwa akikabidhiwa ofisi tangu alipoteuliwa na kuapishwa kuongoza mkoa huo akitoka katika nafasi ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM).
“Kwenye historia, hakuna mwenezi aliyekaa miezi mitano, lakini wakati nina siku 100 katika miezi mitano nimegonga kilomita 11,593, mikoa 23 na tumefanya mambo makubwa ambayo hayatafutika, kwani si muda gani umekaa bali umeacha alama gani kwenye nafasi uliyotoka,” amesema Makonda.
Amesema hata kuwepo kwake mkoani Arusha hataangalia muda gani atakaoutumia katika kuongoza eneo hilo, bali yale atakayoyafanya.
“Nilitakiwa niwe nimesharipoti tangu juzi na leo niwe site. Kila mara kila wakati natamani kwenda kwa kasi zaidi kwa sababu sijui saa wala wakati atakaokuja Yesu kuchukua watu wake,” amesema Makonda.
Makonda amesema katika uongozi wake atafanya mambo sita ambapo suala la kwanza ni kuweka msingi wa haki, huku akisema asipokuwa kiongozi wa kutenda haki, hatokuwa akiwakosesha haki watu wa Arusha pekee, bali yeye pia na uzao wake.
“Wananchi wanaozurumiwa, wanaonyanyaswa, wanaocheleshwa na kuzungushwa kupata haki zao nimekuja kusimama kwa niaba yao, kama mtu yuko Ngaramtoni, Monduli wapi popote alipo iwe Arumeru, ili mradi una haki yako na unajua hii ni haki yangu, sitajali hujasoma, huna pesa, sitajali kama una ndugu mwenye mamlaka nitasimama kwenye nafasi yangu kuhakikisha unapata haki yako,” amesema Makonda.
Amewataka watumishi wa mkoa huo kujua msingi wake wa kwanza katika utendaji ni kutenga haki kwa wananchi, kuendana na azma ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alimtaja kuwa mtu wa kupenda haki.
Uwajibikaji ndiyo jambo la pili alilolitaja, huku akieleza licha ya kupokelewa vizuri ila watageukana muda si mrefu kwa sababu hatijali mtumishi huyo ni mtu gani na amepataje cheo hicho, bali kuhakikisha kila mtu anawajibika kwa nafasi yake.
“Misifikiri huyu alikuwa mwenezi sasa ametoka kwenye uenezi atakuja amepoa, kuna watu wanasema labda atakuwa amejifunza, hakuna nilichojifunza zaidi ya kuwashughulikia wazembe, wavivu na wala rushwa, sina elimu nyingine yeyote, mimi hata nikiwa mkuu wa mkoa kwa siku moja, lakini mtu ajue tu kuwa kuna mwanamume alipita hapa,” amesema Makonda.
Makonda amesema ni vyema kila mtu kwa nafasi aliyonayo kushika majukumu yake kikamilifu, huku akieleza kuwa Mongela alikuwa akitumia akili nyingi kueleza watu mambo, jambo ambalo yeye hana muda huo.
“Niwaombe watumishi wote, mliopo hapa na mlio kwenye ofisi katika sehemu mbalimbali kila mtu ajue wajibu wake na asimame barabara kufanya kazi yake kwa sababu mshahara unaokula ni kodi za wananchi wanaouza mchicha, wanaouza vibanda vyao wanataka wahudumiwe muda wote,” amesema Makonda.
Amesema katika uwajibikaji huo ni vyema wakatanguliza utu na kuona kama wangekuwa ni wao ingekuwaje.
“Kuna wakati kwenye ziara unafika mahali unamsikiliza mtu, unakaa pale ukirudi ndani ya gari unalia unasema Mungu kwanini hawa watu wanafanya hivi, mtu unamwambia njoo kesho, kesho kutwa, faili lako limepotea, mara unaenda kumwita mtaani unamwambia nimeona barua yako ofisini ni nini hiki, ifike mahali kwenye uwajibikaji kila mtu awajibike na usisubiri kusimamiwa na mtu,” amesema Makonda.
Amesema ni vyema watumishi hao kutofikiri kuwa mafanikio yaliyopo ndani ya familia kwa njia za kukandamiza watu, kunyima haki na kupora mali zao kuna baraka na badala yake ni kupanda mbegu mbaya.
“Ndiyo maana familia za watoto wengi wa viongozi hasa viongozi waliokuwa na changamoto za kula rushwa na kunyima haki za watu familia zao huwa hazikai salama, hivyo tuepuka hiyo laana ya kukandamiza haki za watu wengine na kutowajibika,” amesema Makonda.
Suala lingine atakalosimamia ni kuhakikisha mkoa huo unakuwa salama hasa kwa watalii wanaotembelea, jambo litakalokwenda sambamba na watu kufanya biashara usiku kwa usalama.
“Watalii wakija mjini halafu baadaye wanakwenda kulala, halafu hiyo hela tunaipata lini, wametoka kwao hawajaja kulala huku hivyo lazima tuwahakikishie usalama, taa zetu, camera zetu na usafi unaoendana na jiji,” amesema.
Utalii ni jambo la nne atakalosimamia katika mkoa huo kuangazia maeneo matatu ambayo ni utalii wa mikutano kwa wageni kuamua kutumia mkoa huo kufanya mikutano na tayari milango imeshafunguliwa, hivyo ni wakati wa wakazi wa mkoa huo kuandaa malazi kwa ajili ya wageni hao.
“Utalii wa aina ya pili ni watalii wa michezo, tunataka michezo, mechi zote kubwa zinazosifika si tu Arusha hata duniani ije kuchezewa Arusha,” amesema Makonda.
Utalii aina nyingine ni ule uliozoeleka wa watu kwenda mbuga za wanyama, huku akieleza ikiwa nguvu kubwa itawekwa kipato kitaongezeka.
“Tunatamani watu wa Arusha wote wajue faida ya utajiri tulionao na kuusema, kuusimulia na kuueleza popote wanapokuwepo, tungetamani shuleni watu wafundishwe utalii, bodaboda waelewe utalii, ukiingia mapokezi hoteli yoyote muhudumu akuelezee utalii unaopatikanao Arusha,” amesema Makonda.
Uchumi ni jambo la tano atakalosimamia kwa kuangalia sehemu tofauti ikiwemo madini, viwanda, kuongeza thamani ya mazao huku akieleza kuwa katika hilo atakutana na wafanyabiashara wa Arusha, ili wajue nini wanataka kifanyike katika eneo lao.
“Baada ya hapo nitafanya ziara katika wilaya zote, kusikiliza wananchi wanataka nini wana kero gani baada ya hapo tutaweka kila kitu pamoja, tutakaa na chama na kuweka msingi kuwa vipaumbele vyetu na inawezekana yakawa ni haya au yakaibuka mengine zaidi ya haya,” amesema Makonda.