Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makonda aeleza jinsi alivyompinga Lowassa 2015

Makonda Ampigia Simu Silaa Makonda aeleza jinsi alivyompinga Lowassa 2015

Thu, 25 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Manyara. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa CCM, Paul Makonda amesema hakumuunga mkono Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa katika mchakato wa kura za maoni za kuomba kuteuliwa kuwania urais kupeperusha bendera ya chama hicho, mwaka 2015.

Baada ya Lowassa kuenguliwa katika kinyang’anyiro cha urais ndani ya CCM, alijiunga na Chadema na kupitishwa kuwa mgombea urais katika Uchaguzi Mkuu wa 2015.

Makonda ameeleza hayo jana Januari 24, 2024 alipozungumza na wananchi wa Makuyuni wilayani Monduli mkoani Arusha, katika mwendelezo wa ziara yake mikoa ya Kaskazini.  Amesema alikutana na Lowassa baada ya uchaguzi na kumweleza yaliyotokea.

"Sikumuunga mkono Lowassa, niliwaunga mkono wengine, nilikuwa na msimamo wa kumkataa lakini baada ya uchaguzi, nilikutana naye Ikulu akaniita na kuniambia mwanangu nakupenda, nikipata vijana wengine wa aina yako nitafurahi,” amesimulia.

Amesema Lowassa alimtaja Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe, akisema alikuwa miongoni mwa vijana aliobahatika kuwapata.

"Kilichoniumiza chama chetu kimejaa wanafiki, watu walionekana wapo na mimi, lakini kumbe ni wapelelezi na wachunguzi ambao usiku wanapeleka taarifa kwingine hilo ndilo jambo lililouniumiza," amesema Makonda alichoambiwa na Lowassa.

Makonda amesema Lowassa ambaye pia mbunge wa zamani wa Monduli, alimweleza hata wale watu aliowapenda na kuwapa nafasi walimgeuka na kutoa taarifa za uongo CCM ili achukiwe.

Makonda amesema Lowassa alimwambia: “Nimebeba dhambi za watu wengi, ambazo sitastahili mwanangu amini makosa niliyopewa sio ya kwangu, wengi walionipa makosa hayo wapo na unajua.

"Hata wewe (Makonda) wakati unanikataa ulikuwa na haki ya kunikataa, kwa sababu waliokwambia walikuwa katika nafasi ya kuaminika, hata nikisalimiana nao ni kama tunapendana, lakini ni watu wabaya," amesema.

Kwa mujibu wa Makonda, maneno hayo ya Lowassa yalibadilisha mwenendo wake wa siasa na kuanza kutafakari upya kwamba ndani ya chama hicho, usione mtu anakupa taarifa za fulani ukadhani ni mkweli, bali wengine wanatengenezeana ajali.

"Hao viongozi wapo na Fred (mbunge wa Monduli- mtoto wa Lowassa) anawajua, hata wakati mzee wetu anaumwa wale aliowabeba walishindwa kwenda kumsalimia na wengine wanamuombea mabaya," amesema Makonda.

Amesema hivi sasa anawatizama kwa jicho la pili watu hao akisubiri wamchonganishe na Rais Samia Suluhu Hassan na wananchi atawataja kwa historia yao, akisema ni watu wa makundi wenye lengo la kuwagawa watu.

"Imefika hatua ili upate nafasi lazima ujipendekeze kwenye kundi lenye nguvu, lazima uwe mnafiki, lakini Rais Samia alivyooingia madarakani akasema tabia hii haitaki akawapa nafasi watu wote.

"Rais Samia amegundua tukiendekeza makundi tutalipasua Taifa,ndio maana ameweka adhima yake hata wapinzani anawapa nafasi," amesema Makonda.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live