Iringa. Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amesema anakereka na baadhi ya watumishi wanaotaja kiwango cha fedha kilichotolewa na Serikali katika mikutano yake, badala ya kueleza namna zilivyotumika kutatua changamoto au kuboresha huduma.
Mbali na hilo, Makonda amewataka viongozi wa dini kuwaombea pia wasaidizi wa Rais akisema baadhi yao ni vimeo wanaokwamisha utatuzi wa kero za wananchi katika maeneo mbalimbali.
Makonda ameeleza hayo jana Alhamisi Februari 8, 2024 wakati akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Mwembetogwa mkoani Iringa katika mwendelezo wa ziara yake ya mikoa 20 ya ‘back 2 back’, awamu pili sehemu ya kwanza.
Tangu kuanza kwa ziara yake Januari 19, 2024 katika mikoa au wilaya mbalimbali aliyopita baadhi ya viongozi na watendaji wa Serikali wakiwemo wakuu wa mikoa na wabunge wamekuwa wakitamka mabilioni yaliyotolewa na Serikali katika maeneo yao, jambo ambalo ni vigumu kwa mwananchi wa kawaida kuelewa kilichofanyika.
"Nakereka sana na kauli ya kwamba yameletwa mabilioni, mabilioni...muonyeshe mwananchi wa kawaida matokeo ya kazi iliyofanywa na hizo fedha ili aone ni mali yake, kutaja idadi ya fedha haisaidii na mwananchi wa kawaida haelewi.”
"Sehemu moja nimeenda wamesema wao wana matrilioni, mwananchi wa kawaida hiyo lugha haelewi, mwambie tulikuwa hatuna mashine ya CT- scan mgonjwa alikuwa analazimika kupelekwa Dar es Salaam endapo akitaka huduma zaidi," amesema Makonda.
Makonda amewataka watendaji wa Serikali kuonyesha wananchi utofauti wa hali ilivyokuwa awali na sasa ikiwemo gharama walizozitumia na hivi sasa watakavyookoa, baada ya Serikali kufanya uwekezaji.
"Muonyeshe namna ya adha ya usumbufu iliyoondolewa badala ya kukaa saa sita hadi saba barabarani kwenda Dar es Salaam, Serikali imejenga uwanja wa ndege utakaorahisisha kutumia muda mchache kufika Dar es Salaam," amesema Makonda.
Katika hatua nyingine, mwenezi huyo mapema leo akiwa wilayani Mufindi amewaomba viongozi wa dini wasiishie kumuombea Rais Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais, Dk Philip Mpango na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa bali washuke hadi kwa wasaidizi wake wa ngazi ya chini.
"Hili mnalifanya sana viongozi wa dini tumlinde Rais wetu lakini kumbukeni wasaidizi wake, maana kuna wasaidizi vimeo wanaopigisha shoti hii nchi.”
"Yaani unaweza kuwa na jambo lako ukamwambia msaidizi wangu, utadhani atalifikisha, lakini kwa sababu halina faida kwake au fedha anayoipata na wewe sio ndugu yake, ataliweka pembeni wala haangaiki nalo ubaki unawaza jambo lako halifanyiwi kazi kumbe kuna wasaidizi vimeo," amesema Makonda.
Makonda amefafanua kuwa ukiona mtendaji anakimbiza faili lako haraka basi lina masilahi, hivyo amerudia kuwaomba viongozi wa dini kuwaombea wasaidizi wa Rais hasa wale wa ngazi ya chini.
"Maombi yanaweza yasiwe mengi, lakini basi wawe tu na hofu ya Mungu ili wamuone kila binadamu wana haki sawa na thamani awe kikongwe au kijana," amesema Makonda.