Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makonda: Mungu nipe hekima nisimuaibishe Rais Samia

Paul Makonda 780x470 Makonda: Mungu nipe hekima nisimuaibishe Rais Samia

Thu, 26 Oct 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Paul Makonda amesema kuteuliwa kushika nafasi hiyo ni kwa mapenzi ya Mungu aliyemfungulia milango akiomba ampe hekima, busara na uvumilivu kukitumikia chama hicho tawala kwa uadilifu.

"Sina maneno mengi nasema asante sana kwa kuwa mtumishi wa wengi, ni matumaini yangu mlango ambao Mungu ameufungua atanipa hekima, busara na uvumilivu na kukitumikia chama kwa uadilifu, uaminifu na mafanikio makubwa ili nisimuabishe Mungu wala Rais aliyeniamini na kuniteua katika nafasi hii," amesema Makonda.

Makonda ameeleza hayo leo Alhamisi Oktoba 26, 2023 katika ofisi ndogo za CCM zilizopo mtaa wa Lumumba jijini Dar es Salaam katika hafla ya kumpokea baada ya kuteuliwa kuwa katibu wa itikadi na uenezi Oktoba 22, 2023.

Baada ya kukabidhiwa vitendea kazi na mtangulizi wake, Sophia Mjema ambaye ameteuliwa kuwa mshauri wa Rais Samia Suluhu Hassan, Makonda alitumia dakika nne kuzungumza akianza kwa kumshukuru Sophia huku akimsifu kuwa ni kati ya viongozi waliomfundisha kazi akiwa mtumishi serikalini

"Kwa bahati nzuri nimekuja kukitumikia chama na wewe unanikabidhi tena kijiti asante sana, kikubwa nashukuru bado naendelea kwenye ulingo wa siasa kumsaidia Rais Samia kwenye nafasi nyingine," amesema.

Ametumia fursa hiyo kuwaomba watumishi wenzake wa chama hicho kumpa Ushirikiano na kumshauri.

"Duniani kote watu wanaishi kwa taarifa na taarifa zinafanya uamuzi, ukiwa na chanzo kibovu utafanya uamuzi mbovu, lakini ukiwa na chanzo kizuri utafanya uamuzi sahihi wakati wote," amesema Makonda akisisitiza kuwa ushirikiano utakifanya CCM kuendelea kuwa na mashiko kwa wananchi.

Alivyowasili

Aliwasili katika ofisi za Lumumba akiwa amepanda bodaboda ikielezwa kuwa alishindwa kufika na gari yake kutokana na msongamano mkubwa wa magari na watu, na kupokewa na umati wa wafuasi na viongozi wa CCM na serikali.

Alipofika alikwenda moja kwa moja ofisini kuwasalimia viongozi mbalimbali waliojitokeza kumlaki ambapo mkuu wa utawala wa CCM, Marko Mhanga alikuwa wa kwanza kumkaribisha na kuwakaribisha viongozi na kisha kumkaribisha Sophia ili akmabidhi ofisi Makonda.

"Nimehudumu kwenye nafasi hii kwa miezi tisa nilikabidhiwa kijiti na Shaka Hamdu Shaka na juzi Oktoba 22, chama kilifanya uteuzi na leo nakukabidhi wewe (Makonda), tuna imani kubwa utatimiza azma ya chama chetu," amesema Sophia.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live