Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema kinachotafsiriwa kuwa ni uchawa kwa sasa miongoni mwa makada wa chama hicho, ni njia mojawapo ya wananchi kushukuru kwa maendeleo yanayofanywa katika maeneo yao.
Makalla amesema hali hiyo inaanzia katika ngazi ya familia, ambayo imeguswa na maendeleo yanayofanywa na Serikali ya awamu ya sita.
Makalla ameyasema hayo leo Jumanne Mei 7, 2024 akifanya mahojiano maalumu na waandishi na wahariri wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) alipotembelea ofisi za kampuni hiyo Tabata Relini jijini Dar es Salaam.
"Utamaduni wa kibinadamu, mtu akifanya vizuri anatakiwa ashukuriwe. Ndicho kinachotokea kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kumshukuru, kupongeza ni utamaduni wa kibinadamu, huwezi kuwanyamazisha Watanzania kumshukuru, huwezi kuwaratibu, suala la uchawa huu wa kushukuru hatuwezi kuwafunga midomo wananchi," amesema Makalla.
Hata hivyo, Makalla amesema wanaendelea kuchunguza athari ya suala hilo na atakaa na timu yake kulichunguza kwa kina.