Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Amos Makalla amesema tuhuma zilizotolewa na Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu kuhusu kuwapo kwa fedha 'chafu' zinazoingizwa katika chama chao ili kuwavuruga sio za kweli na zinapaswa kuchunguzwa.
Makalla ameyasema hayo leo Jumanne Mei 7, 2024 akifanya mahojiano maalumu na waandishi na wahariri wa kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) alipotembelea ofisi za kampuni hiyo, Tabata Relini jijini Dar es Salaam.
"Huo ni uongo, uzushi uliotengenezwa na hauna ukweli wowote, na ndio maana tunajitokeza na kulijibu.
"Wanaosema chama chao kinapokea hela chafu, ni kashfa ambazo wenyewe wanajipa, sio kauli ya kuipuuza. Mimi nasema Msajili wa Vyama na Takukuru wakae nao waseme zimetoka wapi, je ni ndani au nje ya nchi. Kwahiyo inabidi wajitathmini wenyewe," amesema Makalla.
Chadema ipo katika uchaguzi wa ndani ngazi ya kanda ambapo baadhi ya maeneo ikiwamo Kanda ya Nyasa, mchuano ni mkali na umehusisha mashabiki wa Peter Msigwa na Joseph Mbilinyi 'Sugu' kuwachukulia fomu na mbwembwe nyinginezo, mambo ambayo hayakuzoeleka hapo kabla.