Wakati vigogo wa Chadema Kanda za Victoria, Serengeti, Nyasa na Magharibi wakipigana vikumbo kuchukua na kurejesha fomu za kuwania uongozi, baadhi ya makada wa Kanda ya Kaskazini nao wanajipanga kuingia kwenye kinyang'anyiro hicho.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Chadema, uchaguzi wa kanda nne utafanyika Mei mwaka huu na nafasi zinazogombewa katika uchaguzi huo ni mwenyekiti na makamu mwenyekiti pamoja na mweka hazina wa kanda.
Kwa sasa mchuano wa Kanda za Serengeti, Victoria, Nyasa na Magharibi umepamba moto, baadhi ya vigogo wanaosaka uenyekiti kuchukuliwa fomu za kuwania nafasi hizo na makada wanaowaunga mkono hatua inayofanya uchaguzi huo kuwa na ushindani mkali.
Wakati hayo yakiendelea, Kanda ya Kaskazini inayoongozwa na Godbless Lema nako kumekucha, kwani baadhi ya makada wameelezwa kuinyemelea nafasi hiyo.
Lema ameiongoza kanda hiyo yenye mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Tanga na Manyara kwa kwa miaka mitano.
Miongoni mwa vigogo wanaotajwa kutaka nafasi ya Lema kwa sasa ni pamoja na Gervas Mgonja (Mwenyekiti wa Kamati ya Fedha ya kanda hiyo) na Michael Kilawila (Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro) ambaye pia aliwahi kuwa mwenyekiti wa halmashauri ya Moshi Vijijini.
Leo Jumamosi Aprili 20, 2024 Mwananchi Digital limewatafuta Mgonja na Kilawila ambao walijibu wakati ukifika wataweka mambo hadharani kuhusu kuwania nafasi hiyo inayoshikiliwa na Lema ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya Chadema.
"Kwa sasa siwezi kuzungumza chochote tusubiri chama kitoe utaratibu kama walivyofanya katika kanda nyingine, kisha nitatoa msimama wangu," amesema Mgonja aliyewahi kuwania ubunge wa Same Magharibi katika Uchaguzi Mkuu 2020.
Vivyo hivyo, Mwananchi lilimtafuta Lema kwa mara nyingine kujua msimamo wake kama anatetea nafasi hiyo ambapo amejibu,"Mei 2 nitakuwa na mkutano na waandishi wa habari Arusha na ndipo nitatoa msimamo na mwelekeo wangu wa kisiasa," amesema Lema aliyewahi kuwa mbunge wa Arusha Mjini.
Taarifa zilizopo Mgonja na Kilawila wanatajwa kuwania nafasi ya uenyekiti wa kanda ya Kaskazini, hatua inayosababisha uchaguzi huenda ukawa mgumu kutokana na kila mgombea kuwa na nguvu ya kisiasa.
Kampeni za Sugu, Msigwa mtandaoni
Katika hatua nyingine, wagombea wa uenyekiti wa Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa na Joseph Mbilinyi maarufu kama Sugu, nao wamejipanga kurejesha fomu leo, huku baadhi ya makada wanaowaunga mkono wakianza kuwapigia debe katika mitandao ya kijamii.
Kampeni hizo zinafanywa na watu wa makundi yanayowaunga mkono Sugu na Msigwa wakiambatanisha picha zao na vipaumbele vyao, huku wakiwapigia debe waibuke kidedea.
Mbali na uchaguzi wa kanda, pia kutakuwa na uchaguzi wa kuwapata viongozi wa mabaraza ya mikoa ya Baraza la Wazee (Bazecha), Baraza la Vijana la Chadema (Bavicha) na Baraza la Wanawake la Chadema (Chadema).
Hivi karibuni Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema aliliambia Mwananchi amesema “uchaguzi wetu unafanyika kwa awamu mbalimbali, hivyo kanda hizo ndio awamu ya kwanza ya uchaguzi wa kanda.”
“Baadaye itafuata awamu ya pili ambayo itahusisha kanda nyingine zilizobakia, kisha uchaguzi wa ngazi ya Taifa utafuata baada ya kanda zote kukamilisha uchaguzi," amesema Mrema.