Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Makada CCM wazidi kujitosa kuutaka uspika

Fomu 2 Pc Data Makada CCM wazidi kujitosa kuutaka uspika

Tue, 11 Jan 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) wameendelea kuchukua fomu za kuomba kuteuliwa kukiwakilisha Chama Cha Mapinduzi (CCM) kugombea nafasi ya Spika wa Bunge la Tanzania.

leo Januari 11, 2022 wamejitokeza baadhi ya wanachama kuendelea kuchukua fomu hizo katika ofisi za makao makuu ya CCM jijini Dodoma na wengine kwenye ofisi ndogo Lumumba jijini Dar es Salaam.

Mbunge wa Ilala, Mussa Zungu amechukua fomu hizo katika ofisi za CCM jijini Dodoma huku aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT), Sofia Simba na akiyewahi kuwa Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye wakichukua katika ofisi ndogo za Dar es Salaam.

Baada ya kuchukua fomu hizo, Zungu amesema amefuata sheria zote za kujaza fomu ya kutaka kugombea nafasi hiyo ili wanachama wenzake wampitishe kwa mujibu wa sheria.

“Kwa mujibu wa Katiba ya nchi yetu na Chama chetu nafasi hii ina utaratibu wa kujazwa, na kuombwa kwake ni kujaza fomu ambapo viongozi wa chama watapitia maombi yangu na kutizama kama ninatosha watatoa majibu” amesema Zungu

Sofia ambaye amechukulia fomu katika ofisi ndogo za chama hicho jijini Dar es Salaam amesema “Ni zamu ya mwanamke kuwa tena Spika wa Bunge la Tanzania'.

Akizungumzia kuhusu kilichosumsukuma kuwania kiti hicho, Sofia amesema ni kutokana na kuwa mwanachama halali wa CCM na nafasi hiyo kuwa wazi hivyo anajiona anaiweza.

"Jingine lililonisukuma nimekuwa bungeni kwa miaka 20 hivyo nina uzoefu na ninaona ni muda wa kumrudisha mwanamke bungeni kukalia kiti hicho kwani wanawake tayari tumeonyesha tunaweza.

"Wanawake tumekuwa moja ya wanaharakati katika nchi hii tangu enzi za baba wa Taifa Mwalimu Nyerere, hivyo nafasi hii imetokea hatuna budi pia kujitokeza kugombea," amesema Sofia.

Pia, akiyewahi kuwa Mbunge wa Arumeru Magharibi, Goodluck Ole Medeye amesema ana nia ya kuuimarisha muhimili wa Bunge katika kutunga sheria na kuwa na ushirikiano mzuri na mihimili mingine huku akisifia mchakato huo ndani ya chama chake.

Ole-Medeye ambaye aliyekuwa Mbunge na Naibu Waziri wa Kilimo kati ya mwaka 2010 hadi 2015 amesema “Nia yangu ya kuchukua fomu ni kuwajulisha Watanzania kuwa nina nia ya kuwatumikia kupitia nafasi, nia yangu ni kuimarisha Muhimili wa Bunge” amesema Ole-Medeye ambaye hii ni mara yake ya pili kuomba nafasi hiyo ndani ya chama chake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live