Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Majibizano ya Spika Ndugai na Rais Samia na fukuto la siasa za 2022 na 2025

Samia 3 3 Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania

Thu, 30 Dec 2021 Chanzo: BBC Swahili

Rais wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na Spika wa Bunge la nchi hiyo, Job Ndugai kwa mara ya kwanza wamejibizana juu ya namna bora ya uendeshaji wa taifa lao.

Kiini cha majibizano hayo ni mikopo inayochukuliwa na serikali kufanya shughuli za maendeleo, jambo ambalo Spika ameonya kuwa huenda ikawa chanzo cha nchi hiyo 'kupigwa mnada'kutokana na madeni yatokanayo na mikopo.

Kupishana kauli huko kwa wakuu hao wa mihimili ya dola umezua mijadala na kuelezwa kuwa ni ishara ya mtifuano mkubwa wa hoja zitokanazo na mitanzamo juu ya namna bora ya uendeshaji wa nchi, njia za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, makundi ya kisiasa kushika hatamu ndani ya chama tawala, CCM, mtikisiko wa siasa za kistaarabu zilizoanza kutamalaki na mwanzo wa kuchokonoa na kuharibu taswira ya nchi kimataifa, msuguano ndani ya Kamati Kuu ya chama tawala, na kuyumba kwa mikakati na ajenda za vyama vyua siasa hasa vya upinzani katika masuala muhimu ya kitaifa.

Duru za kisiasa zimebainisha kuwa matamshi makali ya Spika Ndugai yanashangaza kutokana na taswira aliyoijenga kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita akiwa hajawahi kukinzana na aliyekuwa rais wa nchi hiyo John Magufuli aliyefariki dunia Machi 2021 na kulifanya Bunge kuonekana kukosa nguvu itokanayo na mamlaka yake ya Kikatiba ya kuisimamia na kuishauri serikali. Kwa kipindi hicho cha zaidi ya miaka mitano Bunge lilidhibitiwa na uongozi wa Magufuli kupitia uongozi wa Bunge na kwa kiasi kikubwa kuwafanya wabunge kutokuwa huru vya kutosha kushauri, kukosoa na kupendekeza mambo ya uendeshaji wa taifa hilo. Je, Ndugai na Samia wamesema nini?

Ifahamike chanzo cha mjadala huu ni mkopo uliopokewa na serikali kutoka Shirika la Fedha Duniani (IFM) wa shilingi trilioni 1.3 ambazo zimeelekezwa kutekeleza miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa, vituo vya afya na huduma nyinginezo.

Akizungumza katika Mkutano wa pili wa wana kikundi cha Mikalile Ye Wanyausi wa jamii ya Wagogo jijini Dodoma, Desemba 27, 2021, Job Ndugai alimlenga moja kwa moja Rais Samia kwa kusema,

"Juzi mama ameenda kukopa shilingi trilioni 1.3. Hivi ipi bora, sisi Watanzania kwa miaka 60 ya uhuru kuzidi kukopa tuwe na madeni au tubanane hapa hapa, tujenge wenyewe bila madeni haya makubwa yasiyoeleweka. Ni lini sisi tutafanya wenyewe na kwa namna gani? Tutembeze bakuli ndio heshima? Tukishakopa tunapiga makofi, sisi wa kukopa kila siku? Tukasema pitisha tozo anayetaka asiyetaka, pitisha tozo lazima tuanze kujenga wenyewe, nani atatufanyia,yuko wapi huyo mjomba, tukapitisha. Sasa 2025 mtaamua mkitoa waliopo sawa, waje watakaokuwa kazi yao kwenda kukopa, endapo hiyo nayo ni namna ya kuongoza nchi, hivi sasa deni letu ni Trilioni 70. Hivi ninyi wasomi hiyo ni afya kwa taifa? Kuna siku nchi itapigwa mnada hii,"

Rais Samia alijibu mapigo wakati wa hafla ya utiaji sahihi mkataba wa ujenzi wa reli ya kisasa kwa kipande cha tatu cha Makutupora (Manyoni mkoani Singida) hadi Tabora kwa kusisitiza serikali itakopa kugharamia miradi ya maendeleo. Hafla hiyo iliofanyika jijini Dar es Salaam Desemba 28, 2021.

"Kwa njia yoyote, kwa vyovyote tutakopa. Tutaangalia njia rahisi, njia zitakazotufaa kukopa na fedha hizi hatutazitoa kwenye kodi tunazokusanya ndani, ni lazima tutakopa.

Kama walidhani kutakuwa kuna kusimamishwa miradi ili wapate la kusema, halipo. Kuna jitihada za kutuvunja moyo kwenye mkopo, hakuna nchi isiyokopa, tutakopa tumalize miradi ya maendeleo ili tuendelee kwa sababu ukikopa unajenga sasa kwa haraka na kuharakisha maendeleo na mikopo hii ni ya miaka 20 kwahiyo tutakopa na tutalipa taratibu," alisema Rais Samia

Nini taswira ya majibizano hayo kiuchumi?

Mtaalamu wa masuala ya uchumi, Dkt. Bravious Kahyoza, amemwambia mwandishi wa makala haya, "Sio mgongano mzuri kwa uchumi wa Tanzania unaokua na ambao unatoka kwenye hali ya kusinyaa. Zipo sababu za msingi katika hilo;- kwanza mgongano wa matamshi na aina fulani ya 'vitisho' ya Spika wa Bunge, Job Ndugai inaondosha imani kwenye uchumi wenyewe. Ikumbukwe uchumi wa kileo unategemea sana imani kwa wenye mitaji na imani kwa walaji.

Hali hii inaweza kuongeza wasiwasi juu ya uhalisia wa tarakimu za kiuchumi zilizoko hadharani dhidi ya kile kinachoongelewa na viongozi wawili hawa. Hali hii sio nzuri sana kwa mitaji tunayovutia kutoka nje na kwa ndani inaweza kuwa kichocheo cha kuhamishwa mitaji.

"Jambo lingine ni kusambaa kwa taarifa mbaya juu ya uchumi nje ya uchumi wetu. Katika uchumi hali hiyo tunaita 'Narrative Economics. Kauli za hawa viongozi hadharani zinasambaa duniani na kuleta wasiwasi kwa taasisi za fedha. Miaka kati ya 2012-2017 ilionekana kuwa kampuni zilitumia migogoro ya aina hii kwenye mataifa zaidi ya 8 kubaini ukweli tofauti na taarifa walizokuwa wanapata. Hii inaweza kuhalalisha hoja ya nchi za magharibi kwamba nchi zenye urafiki na China kiuchumi zina kasumba ya kutokutoa takwimu za kweli kuhusu madeni ya taifa." Ni harakati za makundi ya kisiasa na kujipanga?

Ifahamike Spika wa Bunge ni mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM na Mwenyekiti wake ni Samia Suluhu Hassan.

Kamati Kuu ndicho chombo kinachoandaa ajenda za chama tawala na chenye ushawishi wa juu kabisa wa namna ya uendeshaji wa chama na hata nchi. Kwamba viongozi wote wawili wapo katika chombo hicho, hivyo ni jambo la kushangaza wanapokosa kauli moja ya kuzungumzia uendeshaji wa nchi na jambo nyeti la deni la taifa.

Ikiwa hawakuzungumzia ndani ya chombo husika ni dhahiri mgongano huu wa hadharani hauna maslahi kwao binafsi, CCM wala serikali. Ni mgongano unaofedhesha mihimili ya dola na kuibua maswali juu ya uwezo wa uongozi pamoja na cheche za moto wa makundi ndani ya chama kushika hatamu kuelekea uchaguzi wa ndani ya CCM mwaka 2022 na uchaguzi mkuu wa Taifa mwaka 2025.

Duru za kisiasa zinabainisha kuwa upo mgongano wa dhahiri katika ya makundi mawili ya wafuasi wa marehemu Magufuli kwa upande mmoja na kundi la Rais Samia kwa upande wa pili. Kundi hili la pili lina mwelekeo wa kufuata siasa za kistaarabu zaidi licha ya mabaki chembechembe za matumizi ya nguvu.

Uthibitisho wa hilo ulianza kuonekana katika uteuzi wa Makatibu wakuu wa mikoa na wilaya wa CCM ulioonesha wazi mfumo mpya umeshika mkondo.

Taarifa ya chama hicho iliyotolewa na Katibu wa Halmashauri Kuu (NEC), Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka wakat iwa uteuzi, ilijinasibu kuwa walioteuliwa hawakutoka nje ya mfumo wa chama tawala. Hilo lina maana kuwa wapo wanasiasa waliohamia chama hicho katika kipindi cha Magufuli ambao wanajulikana kama 'yatima' au waliokatwa mikia nafasi zao ni ndogo mbele ya uongozi mpya wa Samia ikiinganishwa na hapo awali.

Tafsiri nyingine ya ujumbe uliotolewa ni kwamba uenyekiti wa Samia umejikita katika mfumo uliozoeleka wa CCM tofauti na uenyekiti wa Magufuli ambao ulikuwa unasimika mfumo mpya wa kuwachukua wanasiasa kutoka nje ya chama.

Baraza la mawaziri la Magufuli lilitokana na wanasiasa ambao waliingizwa serikalini wakiwa hawana umaarufu wala nguvu ndani ya chama hicho, pamoja na baadhi ya wanasiasa wa upinzani waliohamia na kupewa vyeo mbalimbali ndani ya chama na serikalini. Ni sahihi Rais kumjibu Spika?

Kauli ya Rais Samia imetafsiriwa kujaribu kutoa ufafanuzi juu ya mwenendo wa mkopo na malengo ya serikali yake katika eneo hilo, lakini dhana hiyo inakinzana na kijembe alichorusha cha "kwa wale wanaotuvunja moyo" ikiwa na maana ya kuwalenga wakosoaji wa suala la mikopo akiwemo Spika wa Bunge kuwa ni kuvunja moyo au kukatisha taamaa jitihada za serikali yake.

Kauli ya Spika licha ya kukosoa ilisifia uamuzi wa Bunge kupitisha sheria ya Tozo iliyoanzishwa na serikali ya Samia, ni dhahiri kujibu mapigo kwa namna fulani halikuwa jambo lenye afya.

Upande mwingine baadhi ya viongozi wa chama tawala na serikali wamemwambia mwandishi wa makala haya kuwa "Ndugai, mtu mzima aliteleza", huku wengine wakibainisha kuwa kitendo cha rais kujibu kwa namna ile kinaonesha kuwa "hamhitaji mwanasiasa huyo kuwa Spika wala mjumbe wa ndani ya chama."

Aidha, Rais Samia amefichua kuwa wapo viongozi na wanasiasa ndani ya chama na serikali hawataki afanikiwe katika uongozi wake akiwemo Spika Ndugai, japo hakumtaja kwa jina.

Kwa hiyo, lipo kundi la wanasiasa wafuasi na wapinzani wa Magufuli ndani ya chama na serikali litakalombeba Ndugai ambao kwa nyakati tofauti wamekuwa wakilumbana kwa masuala mbalimbali ikiwemo deni la taifa na mikopo kama ambavyo iliwahi kuzungumzwa bungeni mapema mwaka huu na Mbunge wa Mtama pia Katibu wa zamani wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye. Je upinzani Umelala usingizi?

Ingawaje Bunge limetawaliwa na idadi kubwa ya wabunge kutoka CCM, lakini majukwaa ya kisiasa yameonekana kupwaya kupitia nyenzo mbalimbali kwa sababu wanasiasa kutoka vyama vya upinzani hawapazi sauti zao vya kutosha katika suala la deni la taifa na mikopo.

Sauti za upinzani zimedorora, na kwamba mgongano wa wakuu wa mihimili ya dola inapotokea ilitegemewa kuwa ajenda ya kisiasa. Vyama vya upinzani vinaonekana havina hoja nzito kuhusu masuala ya uchumi dhidi ha serikali.

Wataalamu wa masuala ya kisiasa wanasema mgongano huo unapaswa kuwa ajenda ya upinzani kuwaambia wananchi kuwa namna chama tawala kilivyochoka na kiondolewe kupitia uchaguzi mkuu ujao. Ilitarajiwa wanasiasa wa upinzani wangetumia mwanya huu kama tiketi yao kujiimarisha,kukubalika na kujiongezea umaarufu dhidi ya chama tawala. Upi mustakabali wa yote haya?

Uongozi wa sasa wa Spika umetawaliwa na malalamiko zaidi kuliko kusimamia na kushauri serikali pamoja na kuliongoza Bunge kwa ustadi wa kuwezesha sheria zinapitishwa na kufuatwa. Mkopo uliochukuliwa na serikali ni sehemu ya mapato ya bajeti yaliyojadiliwa katika vikao vya Bunge mnamo mwezi Juni, 2021 na Spika akiwa kiongozi wa mhimili huo.

Swali linaloibuka hapa ni kwa nini Bunge halikupinga jambo hilo ikiwa Spika aliona hatari ya taifa hilo kufikia hatua ya kupigwa mnada sababu ya deni kubwa?

Kwa mantiki hiyo Spika Ndugai naye ameonesha sura isiyoridhisha katika dhana ya mamlaka na uhuru wa Bunge katika kutunga na kupitisha sheria pamoja kuisimamia vilivyo serikali, na zaidi kwa vile ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM ingelikuwa fursa adimu ndani ya Kamati Kuu ya chama kushauriana na Mwenyekiti wake. Si rahisi majibizano haya likawa tukio la kupita, yamebeba maudhui makubwa ya siasa za Tanzania katika miezi au miaka michache ijayo.

Muda utaongea.

Chanzo: BBC Swahili