WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa amewaomba wananchi wa Manyara wamchague Mgombea Urais wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Rais John Magufuli ili aendelee kuhudumia wanyonge.
Aidha, aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Manyara, Ester Mahawe, amemuombea kura Magufuli na kutoa mwito kwa wanachama wa CCM wilayani Babati kuachana na makundi yasiyo na tija kwa chama.
Katika mkutano wa uzinduzi wa kampeni za CCM mkoani Manyara uliofanywa na Waziri Mkuu Majaliwa, Ester alisema: "Mimi nilishakubaliana na uamuzi wa chama; ndugu zangu Wanababati acheni maneno na makundi yasiyo na manufaa kwa chama. Mimi nipo tayari kutumwa na chama changu popote; sipend unafiki na makundi yasiyo na maana, tuache nongwa tuendelee kuwapigania wagombea wetu na tuhakikishe wanapita kwa kishindo."
Akizungumza katika mkutano huo uliofanyika katika viwanja vya Kwaraa, Majaliwa aliwatambulisha wagombea ubunge na udiwani kupitia CCM na pia akaitambulisha Ilani mpya ya chama hicho ya 2021 -2025.
Alisema CCM kinafanya kazi kwa kuongozwa na ilani ya uchaguzi ndiyo maana katika miaka mitano inayokwisha, Serikali imetekeleza ilani hiyo kwa kiasi kikubwa hasa katika sekta za elimu, afya, kilimo, na miundombinu.
Kwa mujibu wa Majaliwa, Serikali imeboresha sekta za afya kwa kiasi kikubwa kwakuhakikisha kila kata inakuwa na kituo cha afya na kuviboresha viweze kutoa huduma bora kwa wananchi.
"Tukizungumzia huduma za afya Wanababati mmenufaika kwa kiasi kikubwa, na mkakati tulionao ni kila kijiji kuwa na zahanati; tumejenga vituo vya afya zaidi ya 498 vinavyotoa huduma zote,” alisema.
Akaongeza: “…Tumejenga na tunaendelea kujenga hospitali za wilaya na tulianza na hospitali mpya. Tunataka kuhakikisha kuwa hospitali za kanda zinajengwa ili wanaopewa rufaa wasihangaike kwenda Muhimbili, bali wapate huduma zote karibu na maeneo yao."
Majaliwa alisema kila mwezi Halmashauri ya Mji wa Babati inapatiwa Sh milioni 20 kwa ajili kununua dawa kuhudumia vituo vya afya.
“Babati Vijijini tumeboresha vituo vyake viwili vya afya ambavyo ni Magugu na Nkaiti kwa kuvipatia Sh milioni 400 na sasa uboreshaji umekamilika wananchi wanaendelea kupata huduma,” alisema.
Alisema mwaka 2015 Magufuli aligundua kuwapo watoto wengi wasiokwenda shule kutokana na gharama nyingi na michango iliyokuwa ikiwaumiza wazazi ndiyo maan aliamua kufanya elimu ya kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha sita kuwa bure.
Kwa mujibu wa waziri Mkuu Majaliwa, ili kutekeleza azima hiyo, Serikali imekuwa ikitoa Sh bilioni 24 kila mwezi zinazosambazwa katika shule za msingi na sekondari.
Alisema Serikali katika kutekelezaIilani ya CCM, mwaka huu imetoa zaidi ya Sh milioni 773 kwa mji wa Babati ili kuboresha miundombinu katika shule za msingi Kwaang,' Nangara, Babati, Mutuka, Harambee, Sinai, Daghailoi, Singu na Darajani.
"Kubwa zaidi kitendo kilichofanywa cha kukusanya kodi na kuhakikisha kila sarafu inayokusanywa inaenda kumnufaisha kila mwananchi na fedha zile zilirudi kwa wananchi, kimechochea maendeleo na kuwafurahisha Watanzania…” alisema.
Alisema kwa namna ya pekee, ilani zote za chama hicho zimeweka msisitizo katika utoaji wa huduma bora za jamiii.
Alisema, ilani mpya ya CCM itakayotekelezwa mwaka 2020-2025 imelenga kuboresha uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na taifa kwa kuwa imegusa kila sekta hivyo, wananchi wakichagua wagombea wa CCM, lazima itatekelezwa.
"Utekelezaji wa ilani iliyopita ulikuwa mzuri sana Tumekuja kwenu kuomba ridhaa ili Serikali ya Chama Cha Mapinduzi iendelee kuyatekeleza yaliyobaki. Ilani yetu imeendelea kusisitiza amani kwa wananchi wake na kuhakikisha wanafanya shughuli zao za kila siku bila kubugudhiwa,” alisema.
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Manyara, Simon Lulu aliwahimiza wananchi kuyakumbuka na kuyaona mambo makubwa yenye manufaa kwa umma yaliyofanywa na serikali chini ya Chama Cha Mapinduzi na hivyo, kuiongezea kipindi kingine ili ifanye zaidi.