Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maharagande kusaidia wananchi kupata ajira

MAHA Maharagande kusaidia wananchi kupata ajira

Fri, 16 Oct 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Segerea jijini Dar es Salaam kwa tiketi ya ACT Wazalendo, Mbarara Maharagande amesema akiwa mbunge katika jimbo hilo ataorodhesha wadau wote wenye uwezo wa kutoa fursa za ajira, ikiwemo viwanda ili kuwawezesha wananchi kupata ajira.

Maharagande alisema hayo wakati akihutubia wakazi wa Kata ya Kisukuru jijini Dar es Salaam. Alisema wadau hao wakipatikana watasaidia kutoa ajira kwa vijana, wanawake na wazee wenye uwezo wa kujishughulisha ili waweze kujiongezea kimapato.

“Tutaorodhesha wadau wote wenye kuweza kutoa fursa za ajira ikiwemo viwanda vilivyopo ndani ya Jimbo la Segerea na maeneo mengine. Tutashirikiana na vijana waliomaliza elimu ya msingi, sekondari na vyuo kuona namna gani wanavyoweza kupata ajira rasmi na au kujiajiri.

“Kuvitambua vikundi mbalimbali vya ujasiriamali, bodaboda, masoko, mamalishe, wakulima wa bustani ili kuwatafutia mitaji na mikopo nafuu waweze kujiendeleza kiuchumi,”alisema.

Kuhusu elimu, mgombea ubunge huyo alisema atashirikiana na mabaraza ya maendeleo kata na manispaa kuongeza vyumba vya madarasa, madawati, kuzitambua na kusaidiana na wananchi walioanzisha shule za awali kupata vifaa vya kujifunzia na kuwasaidia wanafunzi wenye uhitaji maalumu.

Akizungumzia afya alisema akichaguliwa kuwa mbunge, kwa kushirikiana na viongozi wengine watahakikisha kila kata inakuwa na zahanati, kuzipandisha daraja baadhi yake kuwa vituo vya afya vyenye kutoa huduma stahiki.

Maharagande alisema kwenye miundombinu kwa kushirikiana na viongozi wengine watasimamia kuboresha barabara kwa kutumia fedha za ndani na kutafuta mashirika ya ufadhili kutoka nje ya nchi kama benki ya dunia.

“Pia uanzishwaji wa vituo na njia za daladala katika kata mbalimbali litafanyika. Uboreshaji wa mitaro ya maji na kulipatia ufumbuzi wa kudumu suala la uharibifu unaotokana na mafuriko pembezoni mwa mto Msimbazi.

Chanzo: habarileo.co.tz