Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mahakama ya mtandao yatajwa kudhibiti rushwa

8447541269aa816265f3751867b905ac.jpeg Mahakama ya mtandao yatajwa kudhibiti rushwa

Thu, 3 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dk Eliezer Feleshi amesema matumizi ya mahakama mtandao yameongeza imani kwa wawekezaji na yameziba mianya ya rushwa.

Akitoa salamu za serikali katika Ufunguzi wa Mwaka wa Shughuli za Kimahakama jijini Dodoma jana, Dk Feleshi alisema mafanikio makubwa yamepatikana nchini ikiwemo kuanza safari ya mahakama ya kimtandao.

"Mahakama kimtandao imeongeza uwazi na ufanisi na hivyo umefanya wananchi na wekezaji kuongeza imani.

Matumizi ya Tehama yameziba mianya na kupunguza urasimu katika utoaji haki," alisema.

Dk Feleshi alisema, mfumo wa mahakama mtandao unaokoa muda na gharama za kusafiri kwenda kusajili mashauri yao mahali zinapopatikana huduma za mahakama na kufanya kwenye mitandao.

Pia alisema mfumo umesaidia katika uhifadhi wa kumbukumbu na hukumu za mashauri kupatikana kwa urahisi kwenye mtandao bila gharama na umeongeza usalama ambao awali wananchi walihofia hata kujitaja hadharani.

Dk Feleshi alisema ofisi ya mwanasheria mkuu na wadau wake wanaendelea kuboresha mifumo ya kielektroniki ili kusomana na ya taasisi nyingine ili kupunguza urasimu kwa wadau.

Mfumo huo umesaidia kwa mwanasheria mkuu wa serikali kuhifadhi kumbukumbu, ushauri wa kisheria, sheria za bunge, kanuni, sheria zilizofanyiwa marekebisho, utafiti na orodha ya wanasheria na hivyo kujua uzoefu na ubobevu wao. Ili kurahisisha na kuongeza kasi utoaji haki, ofisi ya mwanasheria mkuu, ofisi ya mashtaka, mawakili na taasisi nyingine za kisheria zimewasilisha serikalini mpango wa kuanzisha vituo jumuishi.

Dk Feleshi aliomba serikali iwezeshe uwekaji wa miundombinu ili kutokwamisha utendaji wake na kusaidia kupunguza muda na gharama za kwenda mahakamani kusajili mashauri.

Safari ya maboresho kuelekea mahakama mtandao, inatakiwa kushirikisha wadau wote na kuhakikisha ubongo bandia unapoanza kutumika lazima uwekezaji mkubwa katika miundombinu wezeshi uwe umefanyika.

Ili kufanikisha mahakama mtandao wadau wote ikiwemo ofisi ya mwanasheria, ya mashtaka na mawakili zinatakiwa kuwa na vifaa kama ukumbi, vifaa vya kuunganisha skana na vingine ili kuunganika na mitandao mingine.

Kwa vile Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inatakiwa kwenda na kasi ndani ya mhimili wa mahakama ili kupata matunda yanayokusudiwa, Dk Feleshi aliomba kupitia wizara ya fedha na mipango kuongeza bajeti kadiri ya maombi yao kuanzia mwaka wa fedha 2022/23.

Dk Feleshi alisema mapinduzi ya nne ni ya juu kuliko ya kwanza hadi ya tatu.

Mapinduzi ya kwanza ya karne ya 18 ziligunduliwa mashine na kuanza kutumika, huku ya pili yalihusu nishati ya mafuta na umeme ukachangia maendeleo ya kisayansi na uzalishaji. Mapinduzi ya tatu ya miaka ya 1950 yalikuja na vifaa vya Tehama kama kompyuta ikaanza kutumika.

Katika mazingira ya Tanzania mapinduzi ya nne yamefanya wawekezaji wengi kutoka nje kufanya biashara na kuwekeza kwa njia ya mtandao ambao pia unatakiwa kwenda sambamba na utoaji wa haki kwa haraka.

Maboresho hayo ya utoaji haki kimtandao yalianza mwaka 2015/16 ambapo mahakama ilianza matumizi ya Tehama.

Mahakama ya mtandao ilianza 2018, wakati Jaji Mkuu Profesa Ibrahim Juma alipofungua utaratibu wa kufungua mashauri kwa njia ya mtandao na kuweka kanuni za kusajili mashauri kimtandao.

Usajili wa mashauri kwa njia ya mtandao umekuwa ukifanyika kwa wingi zaidi mfano kati ya Januari mwaka jana hadi jana mashauri 5,235 kati ya 5,447 yamefunguliwa kwa njia ya mtandao isipokuwa 212 ndiyo yamefunguliwa kawaida.

Hayo ni mafanikio ya mahakama na nchi kwa ujumla.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live