Dar es Salaam. Mwenyekiti wa CCM, Rais John Magufuli amewataka viongozi wa ngazi zote wa chama hicho tawala nchini Tanzania kuisimamia Serikali kwa kuitetea, kutangaza mafanikio iliyoyapata.
Ametoa kauli hiyo leo Ijumaa Januari 24, 2020 jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na viongozi wa CCM wa wilaya, mikoa na jumuiya za chama hicho kutoka mikoa yote nchini.
Amesema miradi mingi ya serikali inafanyika kwenye mikoa na wilaya, kuwataka viongozi hao kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo kwenye maeneo yao na wakiona haiendi vizuri watoe taarifa kwa Katibu Mkuu wa CCM, Dk Bashiru Ally.
Rais Magufuli amewataka wajumbe wa mkutano huo kutangaza mafanikio yaliyofanyika katika kipindi cha miaka minne ya Serikali.
Amesema mambo mengi makubwa ya maendeleo yamefanyika nchini, ni wajibu wao kuwaeleza Watanzania.
"Nitashangaa kama kuna kiongozi wa CCM hatambui mageuzi makubwa yaliyofanyika katika awamu hii. Tumejenga hospitali za wilaya 69, huduma za umeme mpaka vijijini, ujenzi wa reli ya kisasa takribani Sh7 trilioni, mradi wa kufua umeme wa mto Rufiji,” amesema Rais Magufuli.
Habari zinazohusiana na hii
- VIDEO: Viongozi 1,780 wa CCM wahudhuria mkutano ulioitishwa na Magufuli
- Magufuli: Sitaki CCM iwategemee matajiri - VIDEO
- Madiwani watatu wa Chadema Arusha wahamia CCM