Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magufuli aahidi makubwa Kigoma

78e40ca039008b911c2378692e239b97 Magufuli aahidi makubwa Kigoma

Mon, 21 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

RAIS John Magufuli ameagiza itangazwe zabuni ya ujenzi wa barabara ya Uvinza kwenda Malagarasi mkoani Kigoma, itakayojengwa kwa kiwango cha lami.

Ametoa agizo hilo jana Uvinza, akiwa njia kwenda Tabora kuomba kura ili wananchi wamchague Oktoba 28 mwaka huu.

Magufuli alisema barabara hiyo ina urefu wa zaidi ya kilomita 151 na itaanza kujengwa hivi karibuni kwa kuwa fedha zipo.

Alisema serikali ilipata zaidi ya sh bilioni 51 kutoka Mfuko wa Msaada wa Nchi ya Kuwait na Mfuko wa Nchi Zinazotoa Mafuta Kwa Wingi Duniani (OPEC), na kwamba, kilichobaki ni kumtafuta mkandarasi.

‘’Hili sio suala tena, tutatangaza zabuni mwezi ujao wa kumpata mkandarasi kwa ajili ya ujenzi wa hiyo barabara kwa kiwango cha lami, fedha zipo tulipasa kutoka Kuwait na OPEC, pia nakumbuka na kaahadi kangu kahapa Uvinza ka kujenga kilomita moja, tumeanza, nitakamalizia, niliamua kupasua barabara kubwa kisha nimalizie hapa, msije sema nimesahahu, na ndio maana nimesimama hapa” alisema Magufuli.

Kuhusu ahadi ya ujenzi wa kilomita moja ya barabara mjini Uvinza, alisema mkandarasi anaendelea na ujenzi.

Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) mkoani Kigoma, umesema tayari mita 900 za barabara hiyo zimejengwa.

Magufuli aliuliza kujenga kilomita moja kwa kiwango cha lami inagharimu kiasi gani, akajibiwa Sh milioni 500, na akampigia simu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Sulemani Jafo kumuagiza apeleke Sh bilioni tano haraka kwa Tarura Uvinza ili wajenge barabara ya lami ya kilomita 10.

“Kama ndio hivyo, basi tangaza zabuni za kujenga hiyo barabara au fanyeni extension (upanuzi) kwa mkandarasi anayejenga ili ajenge barabara yote, hizo kilometa 10 iwe lami, nitaleta fedha zote hizo bilioni 10, nataka nikija kuweka jiwe la msingi barabara ya Uvinza Malagarasi na hii niikute ina lami” alisema Magufuli.

Akiwa eneo la Nguruka mkoani Kigoma, Magufuli alitoa maagizo kwa Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako ahakikishe kero ya ukosefu wa shule ya sekondari katika kata ya Nguruko, inatatuliwa kabla ya mwaka huu kuisha.

“Hapa kuna kero ya ukosefu wa shule ya sekondari, sasa hili sio la kwangu, ilitakiwa mbunge aliyekuwepo hapa awe ameshughulikia kupitia fedha za Mfuko wa Jimbo, tena Waziri wa Fedha anatoka Kigoma, halafu kunakuwa na tatizo la shule, Profesa Ndalichako hili lizungumzie”alisema Magufuli.

Profesa Ndalichako alisema atalifanyia kazi suala hilo. Alimuagiza Ofisa Elimu Wilaya ya Uvinza, kuwasiliana naye na kusema kama zaidi ya madarasa sita yameshajengwa, kibali kitatolewa haraka ili shule ipate usajili.

Chanzo: habarileo.co.tz