Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Magari ya matangazo CCM, Chadema mpambano mkali

9893 Pic+magari TanzaniaWeb

Fri, 3 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Mji wa Moshi sasa ni kelele mtindo mmoja, kutokana na CCM na Chadema kushindana kwa magari ya matangazo yanayozunguka katika mitaa ya kata ya Mawenzi kunapofanyika uchaguzi mdogo wa Udiwani.

Wakati gari la matangazo la Chadema likitumia sauti iliyorekodiwa ya mgombea wake, Africana Mlay akiomba kura, wakati CCM wakitumia gari lenye vijana wanaokipiga vijembe Chadema.

Magari hayo yenye bendera za vyama hivyo, yamekuwa yakipita mitaani na muziki mkubwa, yakiporomosha nyimbo maalumu za vyama hivyo huku watangazaji walioko katika magari hayo wakiwaombea kura wagombea wao.

Tukio lililovuta hisia za wananchi lilitokea leo saa 5:50 asubuhi nje ya Hoteli ya Zebra pale gari la matangazo la CCM lilipokutana na msafara wa mgombea wa Chadema na mameneja wake wa kampeni, wakiomba kura nyumba kwa nyumba.

Mgombea huyo aliyekuwa amefuatana na Mbunge wa Viti Maalumu Grace Kiwelu, madiwani na makada wengine wa Chadema, walikuwa wakiomba kura nyumba hadi nyumba na kusambaza vipeperushi vya mgombea wao.

Hata hivyo walivyofika eneo hilo la Hoteli ya Zebra, lilitokea gari la matangazo la CCM na wakati wanapishana na msafara wa viongozi hao wa Chadema, liliendelea kuwapiga vijembe wagombea wa Chadema kuwa ni watu wa kuhamahama, hivyo hawastahili kuchaguliwa.

“Hawa ni watu hawafai kuwachagua. Unamchagua leo kesho anahamia CCM kumuunga mkono Rais Magufuli (John). Ni heri mchague CCM kwani kamwe hawahami hami na kura yenu haitapotea,” alidai mtangazaji.

Pamoja na vijembe hivyo vilivyotokea katikati ya uombaji kura wa nyumba kwa nyumba, si Mlay, Kiwelu wala makada wa Chadema waliojibu mashambulizi hayo bali waliendelea kuomba kura.

Katika uchaguzi huo, CCM imemsimamisha Apaikunda Naburi aliyewahi kuwa diwani wa viti maalumu.

Chanzo: mwananchi.co.tz