Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maelfu ya wanafunzi hatarini kutoshiriki uchaguzi serikali za mitaa

79915 Uchaguzi+pic

Tue, 15 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar/Mikoani. Wakati maelfu ya wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu na ufundi wakisubiri kukumbana na ’jinamizi’ la kutoshiriki uchaguzi wa Serikali za mitaa, Rais John Magufuli amesema viongozi ambao mikoa yao haitahamasisha watu kujiandikisha watachukuliwa hatua.

Hatihati ya wanafunzi kuchagua viongozi wa mitaa inatokana na uchaguzi huo kufanyika Novemba 24, 2019 kipindi ambacho vyuo vinakuwa vimefunguliwa, wengi hujikuta wamejiandikisha mitaa waliyotoka.

Jambo hilo lilijitokeza hata katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na wa serikali za mitaa wa mwaka 2014.

Ikiwa kasi ya uandikishaji itaendelea kuwa ndogo baadhi ya watendaji watakumbana na mkono wa Magufuli baada ya juzi Waziri wa Tamisemi, Selemani Jafo kuwaweka pabaya wakuu wa mikoa ya Dar es Salaam, Paul Makonda, Anna Mghwira (Kilimanjaro) na Mrisho Gambo (Arusha) baada ya maeneo yao kufanya vibaya katika uandikishaji wa wapiga kura wa uchaguzi huo.

Jafo alimuomba Magufuli kuridhia pendekezo atakalompelekea endapo baada ya zoezi hilo kuisha, baadhi ya mikoa haitofikisha asilimia 50 ya uandikishaji wapiga kura.

Alisema tathmini ya siku mbili Oktoba 8 na 9 Mkoa wa Iringa umeandikisha asilimia 53, Mbeya 34 na Songwe 33 huku Dar es Salaam kwa siku hizo ikiandikisha watu asilimia nane, Kilimanjaro 12 na Arusha 13.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
Uchaguzi wa Serikali za Mitaa 2014 na uchaguzi mkuu wa 2015, wana vyuo waliandikishwa wakiwa vyuoni lakini siku ya kupiga kura wakawa majumbani.

Wakati hali hiyo ikitarajiwa kurejea mwaka huu, baadhi ya Vyama vya Siasa vimeibuka na kuitaka Serikali kuja na mfumo utakaowezesha wanafunzi kuchagua viongozi wa mitaa wakiwa chuoni, kwa Serikali kuunda mitaa katika vyuo wanavyosoma.

Rais wa Serikali ya Wanafunzi Chuo Kikuu Dar es Salaam (Daruso), Hamis Musa alisema, “wanafunzi vyuoni kutoshiriki uchaguzi si mara ya kwanza. Mwaka 2015 ilikuwa hivyo, mfano Novemba 24 wengi tunakuwa vyuoni na wanafunzi wengi wanatoka mikoani ambako wamejiandikisha.”

“UDSM wapo wanafunzi 12,000 na wengi wanaweza wasipige kura. Utaratibu huu wa uchaguzi kufanyika tupo vyuoni unatunyima haki ya msingi.”

Ombeni Daniel, anayetarajia kujiunga na Stashahada ya Mawasiliano ya Umma chuo cha Kumbukumbu ya Stefano Moshi (Smmuco), alisema suala la wao kutopiga kura linahitaji mjadala.

“Hili suala linahitaji mjadala wa kitaifa. Leo naambiwa nijiandikishe lakini wiki ijayo naenda chuo. Afadhali mimi ni hapa Moshi. Kuna wanaoenda Dar, Mwanza na Mbeya,” alidai.

Mwenyekiti wa Shirikisho la Vyuo vya Elimu ya Juu nchini (Tahliso), Peter Niboye alisema wanahimiza wanafunzi kujiandikisha.

“Tupo kwenye mazungumzo na Tamisemi na hivi sasa kama Tahliso tupo Lindi kwenye wiki ya vijana na kesho (leo) tutakuwa na waziri wa Tamisemi tunaweza kupata majibu ya nini cha kufanya kuhusu suala hilo. Wanavyuo popote walipo wajiandikishe kwa wingi wakati huu tunaliweka vizuri suala hili.”

Akizungumzia suala hilo naibu waziri wa Tamisemi, Josephart Kandege alisema kuwa analichukua kama changamoto ambayo inahitaji kufanyiwa kazi kuangalia namna ya kufanya ingawa linachanganya sana.

“Hakuna namna ambayo unaweza kuyafikia makundi yote, kuna ambao watakosa nafasi ya kupiga kura kama hao wanafunzi, nalichukua kama changamoto,” alisema Kandege. Wakati hali ikiwa hivyo, vyama mbalimbali vya siasa vimeanza kuhamasisha watu kujiandikisha ikiwemo ACT-Wazalendo, huku baadhi ya wananchi katika maeneo yao wakitumiwa ujumbe na ofisi za serikali za mitaa wakitakiwa kujiandikisha.

Alichokisema Magufuli

Jana Magufuli aliwataka viongozi wa mikoa kuwahamasisha wananchi kujiandikisha kwa ajili ya kupiga kura, akiwataka kuchangamka kwa kuwa mwisho wa uandikishaji ni kesho.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa safari za ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) mkoani Katavi, Rais Magufuli alisema, “Jana Waziri alitoa takwimu za baadhi ya mikoa iliyofanya vizuri. Ninafuatilia lakini alitoa baadhi ya mikoa inayoendelea kufanya vibaya. Zoezi likikamilika nitataka Waziri anipe taarifa za mikoa iliyofanya vizuri na iliyofanya vibaya.”

“Nataka niseme hapa hadharani, ile mikoa ambayo watu wao watashindwa kuwahamasisha wananchi kujiandikisha kupiga kura nitawashangaa. Ninajua Watanzania hawatanilaumu kwa hatua nitakazochukua.”

Wadau wanena

Mdau wa elimu, Tegemeael Vujole alisema, “Kuwahamasisha vijana kujiandikisha kwa lengo la kuchagua viongozi kisha unawapeleka kwenye majukumu mengine nje ya makazi wakati wa kupiga kura ni kosa la kimfumo tena la makusudi.”

“Serikali hususani Tamisemi inawajibika kueleza kwa nini kosa hili la kimfumo lijirudie mara kwa mara. Je, wizara inaona ni uchaguzi usio na maana?” Alihoji Vujole.

Mkurugenzi wa Itifaki, Uenezi, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema, alipendekeza kuanzishwa kwa mitaa vyuoni, ili wanafunzi hao waweze kuchagua viongozi huko.

Katibu Mkuu wa Chama cha Kijamii (CCK), Renatus Muabhi alisema suala hilo wamekuwa wakilijadili na kwamba huenda hakuna mipango ya kuwawezesha kupiga kura kwa sababu ya woga.

“Hili suala si uchaguzi wa Serikali za Mitaa tu hata uchaguzi mkuu. Hili kundi (vijana) ndilo lenye fikra ya kutaka mapinduzi na mabadiliko na nataka nikuambie ni kundi haliwezi kuipigia kura CCM.”

“Kijana amefunga chuo anajiandikishia Ubungo lakini wakati wa kupiga kura anakuwa Mbeya. Watapigaje kura? Inawezekana Serikali inayoongozwa na CCM ina sababu zake,” alisema

JPM, Majaliwa wajiandikisha

Jana mkoani Dodoma Rais Magufuli alijiandikisha katika kituo cha Sokoine kilichopo wilaya ya Chamwino huku Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa naye akijiandikisha wilayani Ruangwa. Baada ya kujiandikisha, Rais Magufuli alizungumza na wananchi wa wilaya hiyo na kuwataka kujiandikisha kwa wingi huku Majaliwa akisema kujiandikisha ni zoezi la kitaifa.

Takukuru yaonya

Taasisi ya kuzuia na kupambana na rushwa (Takukuru) mkoani Tanga imewaonya viongozi watakaoamua kujitoa dakika za mwisho kwamba itashughulika nao kwa sababu ni kitendo kinachoashiria kuwapo kwa rushwa.

Kamanda wa Takukuru Mkoa wa Tanga, Christopher Mariba alitoa kauli hiyo alipokuwa akiwasilisha kwa wanahabari taarifa ya utendaji kazi wa taasisi hiyo ya kuanzia Julai hadi Septemba 2019.

Alisema kwamba wakati wa kuelekea uchaguzi wa Serikali za mitaa na Uchaguzi Mkuu wa mwakani, Takukuru imeamua kufanyia kazi mambo matano makubwa ambayo katika chaguzi zilizopita yalionekana kuwa ya kawaida lakini taasisi hiyo imebaini kuwa nyuma yake kuna rushwa.

Tuhuma za vurugu zawaponza wanne

Wakati huo huo, watu wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Tanga wakituhumiwa kufanya vurugu katika uandikishaji wa wapiga kura ikiwamo kubainika kujiandikisha majina yao kwenye kituo zaidi ya kimoja. Taarifa zilizothibitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Tanga, Thobias Mwilapwa ni kwamba watuhumiwa hao walikamatwa juzi katika vituo vya kata ya Ngamiani Kusini na Ngamiani kati.

Msimamizi msaidizi wa uchaguzi wa Wilaya ya Tanga, Ramadhani Posi alisema hadi jana Ijumaa, wakazi 44,615 walijitokeza katika vituo 498 vya kujiandikisha kupiga kura ikiwa ni asilimia 34 ya wakazi 135,892 wanaotarajiwa kujitokeza.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ikungi mkoani Singida, Edward Mpogolo amewataka wananchi wa wilaya hiyo kutumia muda uliobaki kujiandikisha katika daftari la uchaguzi wa Serikali za Mitaa ili waweze kutumia haki yao kuchagua viongozi.

Chanzo: mwananchi.co.tz