Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madiwani wamkataa Meneja Tarura

Madiwani.webp Madiwani wamkataa Meneja Tarura

Mon, 4 May 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

MADIWANI katika Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi wamemkataa Meneja wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (Tarura),Wilaya ya Mbozi, Mhandisi Naftari Chaula, kwa madai ya kushindwa kutekeleza maagizo yanayotolewa na madiwani hao ikiwamo kushindwa kuwasilisha mpango wa bajeti.

Walidai kuwa tabia ya meneja huyo kushindwa kutekeleza maagizo yao katika vikao halali vya kisheria inaweza kuwachonganisha na wapigakura wao ambao baadhi yao wameshindwa kufanya shughuli zao baada ya madaraja kuvunjika na Tarura kushindwa kwenda kusaidia kurejesha huduma.

Uamuzi huo ulitolewa jana katika kikao cha kawaida cha Baraza la Madiwani wakati wakithibitisha ajenda zilizopangwa kujadiliwa na Diwani wa Kata ya Nyimbili, Tinson Nzunda (CCM), kusimama na kutoa hoja ya kumkataa Meneja Chaula na kuiomba mamlaka zilizomteua zimpangie sehemu nyingine ya kufanya kazi.

Hoja ya diwani huyo iliungwa mkono na baadhi ya madiwani, hali iliyomlazimu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo, Erick Ambakisye, kuwataka madiwani hao kufanya hitimisho la hoja hiyo kwa kuweka maazimio.

Ushauri wa Mwenyekiti ulikubaliwa na kilifika kipengele cha kuwahoji na diwani 22 waliunga mkono hoja ya kumkataa meneja huyo na wengine wanane walipinga kuondolewa kwake.

Awali, Diwani wa Kata ya Ipunga, Button Sinienga, akichangia ajenda kabla ya kuibua hoja ya kukataliwa kwa meneja huyo, alisema hana ushirikiano na ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri na mara kadhaa amekaidi kuwasilisha mpango wa bajeti ya taasisi hiyo kama taratibu na miongozo inavyotaka.

Naye Diwani wa Hezya, Willy Mukondya, alimlalamikia meneja huyo akidai kumdanganya kumpa fedha za ujenzi wa barabara ya Hezya hadi Namwangwa yenye urefu wa kilometa 11 ambayo ni kero ya muda mrefu kwa wananchi wa kata yake.

Akizungumza nje ya ukumbi, Meneja wa Tarura aliyekataliwa, Chaula, alionyesha kushangazwa na taarifa za kukaidi kupeleka mpango wa bajeti kwenye vikao vya halmashauri kwa kuwa alitekeleza agizo hilo kwa kupeleka taarifa hiyo katika ofisi ya Mkuu wa Wilaya, John Palingo na nakala kupeleka kwa Mkurugenzi, akiamini kuwa ingewafikia madiwani hao.

"Barua ya kuitwa kwenye kikao na kuwasilisha mpango wa bajeti ya ofisi yangu nilipata jana (juzi) na haraka mimi na timu yangu tuliandaa taarifa ya bajeti na kuipeleka kwa (DC) Mkuu wa Wilaya na nakala kuipeleka kwa Mkurugenzi, sasa hoja ya mimi kukaidi nashangaa inatoka wapi," alisema.

Katika hatua nyingine Baraza hilo lilitoa siku 14 kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya hiyo, Hanji Godigodi, kutekeleza maagizo manne kinyume na hapo hatua zaidi zitachukuliwa dhidi yake.

Mkurugenzi Godigodi, hata hivyo, aliwaomba radhi madiwani hao na kuahidi kutekeleza maagizo yaliyotolewa ikiwa ni pamoja na umaliziaji wa kituo cha afya Ndolezi kilichojengwa kwa nguvu za wananchi na serikali kuu kutoa Sh. milioni 200 kwa ajili ya umaliziaji.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live