Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madiwani waibuka na hoja 4 walipwe mshahara

3e707816b8633e43f10d9b63a4faa33c.jpeg Madiwani waibuka na hoja 4 walipwe mshahara

Mon, 17 May 2021 Chanzo: www.habarileo.co.tz

MADIWANI wameiomba serikali iwalipe mishahara kila mwezi kupitia Hazina badala ya posho wanazilipwa na halmashauri kwa kuwa kuna ugumu kumsimamia kikamilifu, mtu unategemea akulipe posho ya kujikimu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha mkoani Pwani, Mussa Ndomba, alisema ni wakati mwafaka kwa madiwani kulipwa mishahara ili kuwawezesha kutekeleza majukumu yao.

“Madiwani wana kazi kubwa kwani hata ukusanyaji wa mapato ya halmashauri unasimamiwa na madiwani na wanasimamia kamati zote za halmashauri, kuongoza na kuweka mwelekeo; yote hayo wanaofanya ni madiwani,” alisema Ndomba.

Alisema mbunge bora hutokana na baraza bora la madiwani, na kwamba, diwani anafanya kazi muda wote na ofisi yake ni popote.

“Tunawashukuru wabunge walioibua hoja hiyo ya sisi kulipwa mshahara kwa kila mwezi kwani wameona na kutambua namna tunavyopambana katika kuleta maendeleo na katika vikao vya baraza la madiwani vinapofanyika huingiliana na vya wabunge hivyo madiwani ndio wanaendesha na kusimamia mambo yote kwenye majimbo,” alisema Ndomba.

Akaongeza: “Posho tunazolipwa ni ndogo sana, hivyo ni vema mfumo uangaliwe ili tuweze kulipwa maslahi mazuri na kuleta uwajibikaji na maendeleo yatakuja kwa haraka na wananchi watahudumiwa vizuri.”

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya Sumbawanga, Kalolo Ntila, aliiomba serikali iwalipe madiwani mishahara kila mwezi na posho za kila mwezi kupitia Hazina kwa madai kuwa, baaadhi ya halmashauri zinashindwa kuwalipa kwa madai kuwa vyanzo vya mapato vimechukuliwa na serikali kuu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Kalambo, Daud Sichone alisema madiwani wengi wamekuwa masikini kutokana na maslahi duni.

"Hii posho ya Sh 350,000/- haitoshi tuliomba tuongezewe iwe kati ya Sh 500,000/- hadi 800,000/- lakini majibu ni yaleyale,” alisema Sichone.

Alipendekeza kuwa kwa kuwa baadhi ya halmashauri zinashindwa kuwalipa madiwani posho ya Sh 350,000/- hivyo walipwe kupitia Hazina kwa sababu baadhi ya vyanzo vya mapato vya halmashauri vilirejeshwa serikali kuu.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mji Handeni, Mussa Mkombati alisema huwezi kufanya vizuri katika uwajibikaji wakati unayemsimamia ndiye unategemea akupe posho ya kujikimu.

"Sisi tunamtegemewa kusimamia halmashauri hatuwezi kufanya vizuri wakati kama hatuna hata uhakika wa mishahara yetu, hivyo ipo haja ya serikali kuangalia huu muundo tena," alisema Mkombati.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe, Sadik kallaghe, alisema suala la mishahara kwa madiwani limezungumzwa kwa muda mrefu hivyo ni wakati sasa lifanyiwe kazi.

"Tunahitaji mishahara na sisi madiwani ili tuweze kufanya kazi zetu kwa ufanisi katika kata zetu kwani sisi ndio wenye wananchi na tunajua shida zilizopo wanazokutana nazo," alisema Kallaghe.

Madiwani kadhaa wa Arusha waliomba walipwe mshahara wa kati ya Sh milioni 1.5 na Sh milioni 2 kwa mwezi.

Diwani wa Kata ya Ngarenaro, Isaya Doita na Abraham Mollel wa Kata ya Kimandolu, walisema madiwani wanafanya kazi kubwa kwa kuwa wao ndio wanaoshinda na wananchi na kuhangaika na kero zao za kila siku.

Doita alisema wanalipwa Sh 300,000 kwa mwezi na posho za vikao vya madiwani, lakini hazitoshi kujikimu katika maisha ya madiwani.

"Tofauti bungeni anatakiwa mwakilishi mmoja tu sasa kwa nini wabunge wapate posho nyingi wakati wao kama madiwani wanaohangaika na shida za wananchi wakilipwa posho ndogo kuliko wabunge wanaokaa vikao vya kamati, na mwisho na mwezi kulipwa hela nyingi kama mshahara," alisema.

Mollel alisema ni vema posho za madiwani ziangaliwe upya na pia serikali ione uwezekano wa kuwalipa mishahara ya kila mwezi kwa kuwa wanafanya kazi kama za wabunge.

Diwani wa Kata ya Lulembela, Halmashauri ya Wilaya ya Nyang'hwale mkoani Geita, Deus Lyankando, alisema ni muhimu madiwani walipwe mishahara kwa kuwa kulipwa na wakurugenzi inawanyima uhuru wa kuhoji mambo mengi yasiyoenda sawa.

"Mimi nadhani ni jambo jema kwa sababu rais, wabunge na madiwani wote tunachaguliwa kwa mujibu wa sheria kuitumikia serikali, hivyo si sawa kwa madiwani kutengwa kwenye mfumo wa malipo, hiki ni kitu kinachotuvunja moyo kutekeleza majukumu,”alisema Lyankando.

Akaongeza; "Tunashughulikia maendeleo makubwa, tunakusanya michango mingi, sasa wewe unatengeneza mamilioni halafu unalipwa posho, ni vyema mchakato uwahishwe, uanze mwaka ujao wa fedha, kama imewezekana kumlipa mtendaji mshahara mzuri kwa nini isiwe hivyo haa kwa diwani!"

Naye Diwani wa Kata ya Nyankumbu katika Halmashauri ya Mji wa Geita, John Mapesa, alisema madiwani hawana mishahara wala fedha za mfuko wa maendeleo, lakini wanashiriki michango mingi, hivyo wanawateseka.

"Mtendaji wa kata analipwa mshahara na posho, diwani hakuna, hata ile heshima inakuwa haipo, na huyu mtu anashughulika na wananchi kwenye shughuli za kila aina, kwa hiyo mimi naona walifanye suala hili, tena walifanye haraka sana, kwa sababu diwani ni kiungo kikubwa mno,” alisema Mapesa.

HabariLEO lilizungumza na Diwani wa Kata ya Chato, iliyopo Halmashauri ya Wilaya ya Chato mkoani Geita, Mange Ludonya aliyesema, mwaka 2018 Umoja wa Madiwani Nchini ulikutana na Rais John Magufuli na kumueleza hoja hiyo na aliahidi kuifanyia kazi.

Diwani wa Kata ya Nyakanga, Wilaya ya Butiama, Shangire Shasha alisema kama ni vigumu wao kulipwa mishahara posho zao zilipwe na serikali kuu na iongezwe angalau ifike Sh milioni moja.

Shasha alisema madiwani wanafanya kazi katika jamii na kila mara wanalazimika kutumia fedha kwa kuzunguka kata nzima kutatua kero zinazowakabili wananchi.

Gazeti hili lilizungumza na Diwani wa Kata ya Kitaji, Halmashauri ya Manispaa ya Musoma, Golden Charles akadai kuwa, halmashauri nyingi hazina vyanzo vya mapato vya kutosha kuziwezesha kukidhi mahitaji ikiwa ni pamoja na kuwalipa posho madiwani.

Diwani wa Kata ya Kyanyari, Wilaya ya Butiama, Mgingi Mhochi alidai kuwa, baadhi ya halmashauri zinashindwa kuwalipa posho madiwani na kusababisha migogoro na madiwani.

Naye Diwani wa Kata ya Songwe kutoka halmashauri ya Kishapu mkoani Shinyanga, Abdul Ngoromole, alisema madiwani wanastahili kulipwa mishahara kwa kuwa wana majukumu mengi yakiwemo ya kusimamia utekelezaji wa miradi.

"Tutafurahi fedha ziwe zinatoka Hazina na bajeti ya mapato ya ndani iliyokuwa inatengwa kwa ajili ya posho za madiwani, vikao vya kamati na posho za ziara zielekezwe kwa malipo ya wenyeviti wa vijiji na vitongoji kwani nao wanafanya kazi ya kuhakikisha maendeleo yanapatikana," alisema Ngoromole.

Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kahama mkoani Shinyanga, Yahaya Ramadhani, alisema madiwani wanastahili kulipwa posho kwa kuwa wanazifahamu kwa ukaribu changamoto zinazowakabili wananchi na wamekuwa wakisimamia utekelezaji wa miradi.

HabariLEO lilizungumza na Diwani wa Viti Maalumu katika Manispaa ya Ilemela, Kuruthumu Abdallah, aliyesema, ni muhimu madiwani walipwe mishahara kwa kuwa wanafanya kazi kwa karibu na wananchi kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Diwani wa Kata ya Pamba katika Jimbo la Nyamagana, Rodick Ngoye ambaye ni Naibu Meya wa Jiji la Mwanza alisema madiwani wanafanya kazi kubwa ikiwemo ya kufahamu mahitaji kwenye mitaa na kwenye Kamati ya Maendeleo ya Kata (WDC) ili kuibua Maendeleo.

“Tuko na wananchi shida zao wanatufikishia tunawatatulia hatuna mfuko vilevile kukaa vikao na kuwafikia wananchi kuwaunga mkono kwenye kazi zao kama tunavyofanya kwa sasa katika ujenzi wa vyumba vya madarasa ni kazi muhimu inayolingana na hitaji la kulipwa,” alisema.

Akaongeza; “Tunafanya kazi kwa karibu na umma hivyo, upo umuhimu taifa lituone na hivyo tulipwe mshahara badala ya posho tu ambayo haikidhi mahitaji," alisema Ngoye.

Katibu Mtendaji wa Jumuiya ya Tawala za Mikoa Tanzania (ALAT), Elirehema Kaaya, aliunga mkono kilio hicho cha madiwani na kuiomba serikali ifikirie kuboresha maslahi yao.

“Nashukuru juzi bungeni Waziri Ummy (Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa) alizungumzia vizuri hoja hii ilipoibuliwa bungeni na kuleta matumaini kwetu,” alisema Kaaya.

Imeandikwa na John Gagarini (Kibaha), Peti Siyame (Sumbawanga), Veronica Mheta (Arusha), Amina Omari (Tanga), Yohana Shida (Geita), Editha Majura (Musoma), Kareny Masasy (Shinyanga), Suleiman Shagata (Mwanza) na Halima Mlacha (Dar es Salaam).

Chanzo: www.habarileo.co.tz