Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madiwani wahofia kutupwa nje 2020

Mon, 4 Feb 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Madiwani wa kata mbalimbali za manispaa ya Kigamboni wamelalamikia baadhi ya miradi wanayoipeleka kwenye halmashauri hiyo kutotekelezeka kwa wakati hatua inayowapa wakati mgumu wananchi wao.

Walieleza hayo juzi wakati wa kikao cha baraza la madiwani cha manispaa hiyo kilichokuwa na ajenda mbalimbali ikiwemo kupokea taarifa za utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kata tisa za manispaa hiyo.

Walisema miongoni mwa miradi wanaoilalamika ni kutojengwa kwa mitaro na taa za barabarabi itakayopitisha kuelekea bahari ili kupunguza adha ya nyumba kuzingirwa na maji wanayoipata hasa nyakati za mvua.

“Mheshimiwa mwenyekiti hiki kikao kinachukua muda mrefu, lakini leo (jana) sisi madiwani wote tulipanga tutumie dakika kumi kuwasilisha taarifa zetu za kata ili tuondoke, kwa sababu mambo tunayoyaomba hayatekelezeki kwa wakati. Wananchi huwa wanatuliza mmefikia wapi tunashindwa kuwajibu,” alisema Dotto Msawa ambaye ni diwani Kigamboni.

Msawa alisema wamekuwa wakipeleka maombi ya miradi mbalimbali ambayo inaishia kuwekwa kwenye makaratasi na kupangiwa bajeti lakini utekelezaji wake ni mgumu.

Diwani wa Kimbiji, Bunaya Sanya aliungana na Msawa kwa kusema baadhi ya taarifa wanazoandika kuhusu kero za wananchi hazifanyiwi kazi kwa wakati jambo linalowapa wakati mgumu.

“Kama alivyosema mjumbe mwenzangu tulipanga tutumie dakika 10 halafu tuondoke katika kikao hiki. Tuliamini tukifanya hivi mtajirekebisha maana kuna miradi mingi tangu tukiwa manispaa ya Temeke bado haijatekelezeka hadi leo,” alisema Sanya.

Hata hivyo, mkurugenzi wa manispaa hiyo, Ng’wilabuzu Ludigija aliwatoa hofu kwa kuwaeleza kuwa miradi hiyo inatekelezwa lakini kwa utaratibu maalumu na kulingana na fedha zilizopo.

“Mara nyingi tunatekeleza miradi iliyoandika katika bajeti. Lakini kuna baadhi ya miradi inaletwa katikati ya bajeti jambo ambalo utekelezaji wake unakuwa ni mgumu, ndio maana huwa tunawashauri madiwani wakati kupanga bajeti waandike miradi ya kipaumbele ili ifanyiwe kazi, kuliko kuileta katikati,” alisema Ludigija.

Katika hatua nyingine, madiwani hao akiwamo Isaya Mwita alisema ni wakati muafaka kwa manispaa hiyo kujipanga kwa ajili kutafuta vyanzo vya mapato ili fedha zitakazopatika zitekeleze midai mbalimbali ya maendeleo.

“Mnaweza mkaongea na jiji kuangalia uwezekano wa kuanzisha stendi ya mabasi ya mikoa kusini ili ziwe mbili ile ya Mbagala. Hii inawezekana na itachangia mapato kwa kiasi kikubwa katika manispaa hii changa,”alisema

Ludigija alisema anatambua vyanzo vilivyopo havitoshelezi, lakini bado anaumiza kichwa na watalaamu wake kuangalia namna ya kuongeza vyanzo hivyo ili manispaa hiyo itekeleze majukumu yake kwa ufanisi.



Chanzo: mwananchi.co.tz