Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madiwani Kibondo waziba pengo la mwenyekiti aliyetoweka

Thu, 5 Jul 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kibondo. Wakati Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kibondo, Simon Kanguye akiwa hajulikani alipo tangu alipotoweka katika mazingira ya kutatanisha Julai 20 mwaka jana, Phares Nzobona amechaguliwa kuziba pengo lake.

Kanguye alitoweka katika mazingira ya kutatanisha baada ya kuchukuliwa na watu wasiojulikana wakati akitoka ofisini kwake.

Katika kikao chake kilichofanyika jana, Baraza la Madiwani wa halmashauri hiyo lilimchagua Diwani wa Bunyambo (CCM), Phares Nzobona kushika nafasi hiyo kwa kura 20 akimshinda Julius Kihuna wa Chadema aliyepata kura tano. Baraza hilo linaundwa na madiwani 26 CCM ikiwa nao 17 na upinzani tisa.

Akizungumzia taratibu zilizotumika kumchagua, Nzobona alisema uchaguzi ulifanyika baada ya Kanguye kutohudhuria vikao vitatu kwa mujibu wa kanuni. “Kanuni za Serikali za mitaa zinaelekeza kwamba mjumbe wa baraza asipohudhuria vikao vitatu mfululizo bila taarifa anakuwa amepoteza nafasi yake ya udiwani, ndiyo maana halmashauri imefanya uchaguzi kujaza nafasi hiyo,” alisema Nzobona.

Alisema Kanguye hajahudhuria vikao vinne kuanzia Agosti, 2017.

Nzobona alisema kutokana na kubanwa na kanuni madiwani wameamua kufanya uchaguzi wakati taratibu za kiuchunguzi kuhusu alipo zikifanywa na polisi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kigoma, Martin Ottieno aliliambia Mwananchi kuwa wamekuwa wakifuatilia kutoweka kwake, ingawa wananchi wameshindwa kueleza chochote wanachojua kuhusu suala hilo ili iwe rahisi kumpata.

Mteule aomba ushirikiano

Akizungumzia ushindi wake, Nzobona aliwaomba madiwani wenzake, watendaji, wananchi na wadau wa maendeleo kushirikiana naye kutekeleza miradi ya maendeleo.

Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Kibondo, Themeo Ndenza na Sheikh Uled Issa wa Bakwata waliwataka madiwani na viongozi wa Serikali kuzishughulikia na kuzipatia ufumbuzi changamoto zinazowakabili wananchi.

Sheikh Uledi aliwataka pia madiwani kutobaguana wala kutanguliza mbele tofauti za kiitikadi katika suala la maendeleo.

Chanzo: mwananchi.co.tz