Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madiwani 16 wawania umeya jiji la Arusha

F7c18804a2b4132d07aad0128918f9fa.jpeg Madiwani 16 wawania umeya jiji la Arusha

Thu, 5 Nov 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

MADIWANI 16 kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) wamechukua fomu, kuomba kugombea umeya wa Jiji la Arusha na wengine wanne wameomba kuwania unaibu meya wa jiji hilo.

Katibu wa CCM Wilaya ya Arusha, Dennis Mwita alisema kuwa kwa kuzingatia agizo la Katibu Mkuu wa chama hicho, Dk Bashiru Ally, jana saa 10 jioni ilikuwa mwisho wa kuchukua na kurudisha fomu hizo na kwamba atatoa majina ya wagombea wote waliojitokeza kuwania nafasi hizo.

Alisema baada ya kumalizika uchukuaji na urudishaji fomu, hatua itayofuata ni vikao vya mapendekezo na uteuzi katika ngazi za chama na bado tarehe ya vikao hivyo haijajulikana.

Katibu wa CCM wa Wilaya ya Longido, Ezekiel Mollel alisema madiwani wawili wamechukua fomu kuwania uenyekiti wa halmashauri ya wilaya hiyo, ambao ni Simon Laizer na Allaice Mushowa.

Halmashauri hiyo inatarajiwa kuongozwa na CCM, kwa kuwa katika Uchaguzi Mkuu madiwani wake wote walipita bila ya kupingwa.

Mkoani Dar es Salaam, madiwani wateule 12 kati ya 14 wa kata zilizopo Manispaa ya Ubungo, wamechukua fomu kuomba CCM iwateue kugombea nia nafasi ya Meya wa Manispaa ya Ubungo na Meya wa jiji hilo.

Katibu wa CCM Wilaya ya Ubungo, Silvester Yaredi akizungumza na gazeti hili kwa simu jana, alisema mpaka jana mchana madiwani wateule 12 walichukua fomu na kati yao 11 wameomba kugombea umeya wa manispaa na mmoja ameomba umeya wa Jiji la Dar es Salaam.

“Mpaka leo mchana (jana) madiwani 12 wamejitokeza kuchukua fomu. Wilaya yetu ina kata 14, hivyo madiwani wateule wa kata 12 wamejitokeza na kati yao mmoja amechukua fomu ya Meya wa Jiji na 11 wa manispaa,” alisema Yaredi.

Chanzo: habarileo.co.tz