Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Madai ya wabunge kuchukua mlungula yatawala Kenya

13766 Bunge+pic TanzaniaWeb

Sat, 25 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Wabunge wawili wanataka Bunge la Kitaifa hapa Kenya lifutiliwe mbali kufuatia madai ya baadhi ya wabunge kuhongwa na waliotajwa katika sakata ya sukari yenye sumu.

Mbunge wa Lugari, Ayub Savula na mwenzake wa Matungu, Justus Muruga wanasema Wakenya hawana budi kupewa nafasi ya kuwachagua viongozi mbadala wanaojali masilahi yao.

Matamshi yao yalichochewa na madai kwamba baadhi ya wabunge walihongwa ili kuangusha ripoti kuhusu uagizaji wenye utata mwingi wa sukari yenye sumu.

Wanataka pia madai hayo ya uhongaji yachunguzwe haraka iwezekanavyo.

Spika wa Bunge, Justin Muturi alikuwa amewataka makachero wachunguze madai hayo lakini Katibu wa Bunge, Michael Sialai akasema zoezi hilo halitafanyika kwa sasa.

Wabunge hao wawili wanatoka katika eneo la magharibi mwa Kenya ambapo kilimo cha miwa ni uti wa mgongo wa uchumi. Wanasisitiza kwamba wakulima watashinikizwa kutuma maombi yao kwa Mahakama ya Juu ili Bunge livunjwe mara moja.

Wabunge hao bila shaka hawatafanikiwa katika juhudi hizi za kutaka Bunge livunjwe kwa sababu hii si sababu ya kufanya Bunge lielekee mkondo huo. Kuna njia nyingine za kufuata.

Madai ya kuhongwa kwa wabunge yaliibua hasira miongoni mwa Wakenya wa matabaka mbalimbali. Ripoti hiyo kuhusu uagizaji wa sukari iliisababishia serikali hasara ya Sh10 bilioni za kodi ambazo hazikupitishwa na wabunge ilipofikishwa mbele yao wiki jana.

Kauli ya Mudavadi

Kinara wa chama cha ANC, Musalia Mudavadi ambaye sasa ni sauti ya upinzani baada ya Raila Odinga na Kalonzo Musyoka kujiunga na Rais Uhuru Kenyatta, anasema tabia ya wabunge imesaliti imani ambayo Wakenya walikuwa nayo kama wawakilishi wao bungeni.

“Bunge lilionyesha aibu kwa kukubali kushirikiana na wahalifu,” anasema Mudavadi.

Mudavadi anasema walichofanya wabunge kimewapa ujasiri wahalifu na kusaidia wale wanaokwepa kulipa ushuru. Aliongeza kwamba hatua ya wabunge inakinzana na juhudi za Rais Uhuru za kupambana na ufisadi. “Wabunge wamewatupa wakulima wa miwa katika maisha ya uchochole na kuzika matumaini yoyote ya kufufua sekta ya sukari nchini.”

Ripoti hiyo iliandikwa baada ya wiki tatu za uchunguzi kuhusu ni kina nani walihusika. Pia, ilikuwa imefanyiwa marekebisho baada ya malalamiko kwamba kamati zilizokuwa zinaendesha uchunguzi zilikuwa zimezembea kwenye majukumu yake.

Wabunge walichukua hongo kwa sababu ya ubinafsi, uchoyo na uchu wa kujifaidisha kutokana na matatizo yanayokumba wananchi.

Kwa kukosa kupitishwa kwa ripoti hiyo muhimu, wabunge walitumbukiza nchi kwenye shimo lisilokuwa na tumaini. Hawa ni viongozi wanaofaa kuongoza na uzalendo wanapotekeleza wajibu wao lakini katika suala hili nyeti, waliurusha uzalendo nje ya dirisha na kukumbatia uroho wa hali ya juu.

Mbunge wa Kieni, Kanini Kega ambaye alikuwa mwenyekiti wa Kamati ya Bunge iliyoongoza uchunguzi wa sakata hilo, anamlaumu kiongozi wa waliowengi bungeni, Adan Duale kwa kushindwa kupitishwa kwa ripoti hiyo. Anasema, aliwasihi wabunge wasiipitishe ripoti hiyo kwa madai kwamba kamati haikufanya kazi yake vizuri.

Kiwango cha rushwa

Baadhi ya wabunge wanadaiwa kuhongwa kati ya Ksh10,000 (Sh220,000) huku wengine wakiweka kibindoni Ksh30,000 (660,000).

Ukabila na mirengo ya kisiasa vilichangia katika vitendo hivyo katika Bunge la kitaifa. Kwa kukosa kupitishwa kwa ripoti, walanguzi wa sukari feki walipata ushindi huku wakulima wakisalia katika ufukara.

Wabunge waliokuwa wanagawa hongo kwa wabunge wenzao wanatoka maeneo ya Rift Valley na Kaskazini mashariki mwa Kenya ambako ndiko wanatoka mawaziri wanaotuhumiwa kuhusika kwa uagizaji wa sukari.

Mbunge mmoja alieleza jinsi alivyopewa bahasha yenye fedha na mbunge mmoja kutoka kaskazini mwa Kenya. “Nilikataa kupokea bahasha hiyo,” anasema mbunge wa Kimilili, Didmus Barasa ambaye baadaye alimkabili mbunge huyo mwanamke kwa kujaribu kumuhonga.

Mbali na mbunge huyo mwanamke, wabunge wengine wanne walionekana wakiwaita wenzao wapokee kitita cha fedha kuzuia ripoti isipitishwe, waliweza kuwalipa wabunge wapatao 40 kwa wakati mmoja kutoka Bunge la Kitaifa na Seneti.

Baada ya hapo, jasho lao lilipata matunda kwa sababu ripoti ‘ilikunywa maji’ na kuzamishwa.

Vita dhidi ya ufisadi haviwezi kufua dafu ikiwa viongozi wanaegemea makabila yao badala ya kuweka Kenya mbele.

Mshahara wa wabunge

Wabunge hupokea mshahara wa Sh1 milioni (Sh22 milioni) kila mwezi lakini kwa sababu ya ulafi wao walikubali kuuza haki ya Wakenya ili kuokoa ngozi za wanyanyasaji kwa vipande kidogo vya fedha.

Ni aibu kwamba taasisi kama Bunge ambalo lina jukumu la kuwatetea wananchi, imeamua kula na kunywa na wale watu wanaowanyanyasa.

Sasa, badala ya kuzuia uagizaji wa sukari haramu, milango mingi imefunguliwa kwa waagizaji sukari ambao wanalenga kumaliza sekta ya sukari nchini.

Ripoti hiyo ilifanyiwa marekebisho ili kuipa nguvu na kuziba nyufa zilizoleta tashwishi kuhusu waagizaji na wale walitoa fursa ya kuleta bidhaa hiyo kutoka ughaibuni.

Ripoti hiyo ilikuwa inataka Waziri wa Fedha, Henry Rotich, mwenzake wa Viwanda na Biashara, Adan Mohammed na aliyekuwa Waziri wa Kilimo, Willy Bett watuhumiwe kwa kutumia mamlaka yao kutoa vibali vya kuagiza bidhaa hiyo. Bett sasa ni Balozi wa Kenya nchini India.

Ripoti hiyo iliangushwa ili kuwaokoa mawaziri hao pamoja na mabwanyenye wa sukari. Baadhi ya waagizaji wana ushawishi mkubwa katika serikali. Wadadisi wa masuala ya siasa wanasema, itakuwa vigumu kuufikia mtandao huu wa wafanyabiashara matajiri kwa sababu ya uhusiano wao na wale walio uongozini. “Ukiwagusa, umewaguza viongozi wa ngazi za juu, akasema mdadisi mmoja.

Fedha zilizotumiwa kuwahonga wabunge zilitumwa kupitia kwa mbunge mmoja na mmoja wa watu wanaotuhumiwa kwa sakata hii.

Kuna wanahabari walioonyeshwa bahasha zilizokuwa na noti mpya tayari kusambazwa kwa wabunge kunyonga ripoti. Baadhi za bahasha zilikuwa na Sh30,000 huku zingine zikiwa na Sh10,000. Walikuwa wanapewa kulingana na uzito wa mbunge. Kama wewe ni mbunge usiye na mdomo mkali, ulipokea Sh10,000 lakini ikiwa una kidomo domo, bei yako inapanda na unapokea Sh30,000.

Mbunge wa Usonga, Samuel Atandi alinukuliwa na vyombo vya habari akisema pesa zilikuwa zinagawanywa tangu Jumatano jioni wiki jana kwa lengo moja tu; kuzuia ripoti hiyo isipite.

Hata hivyo, hakusema nani alikuwa anazigawa pesa hizo lakini alisema hakuzipokea kwa sababu maadili yake mema hayangemfanya asaliti Wakenya.

Mawaziri wawili walikuwa wametofautiana kuhusu uhalali na usalama wa sukari hiyo. Waziri wa Usalama wa Nani, Fred Matiangí alisema sukari ilichunguzwa na kupatikana na sumu. Laini Waziri wa Viwanda na Biashara, Adan Mohammed ambaye sasa amehamishwa kwa wizara ya Afrika Mashariki alidai sukari ni salama.

Ripoti ya Bunge pia haingeweza kutoa taarifa ya kudhibitisha ubora wa bidhaa hiyo. Wakenya wamebaki kwenye njia panda. Wengi wameamua kutotumia sukari hadi serikali iwadhibitishie usalama wa bidhaa.

Mudavadi sasa anataka Rais Uhuru aunde tume ya kuchunguza sakata hili la uagizaji wa sukari.

Chanzo: mwananchi.co.tz