Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maazimio ya vyama vya upinzani, CUF Lipumba wapinga

33768 Pic+cuf Tanzania Web Photo

Fri, 28 Dec 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Unguja. Katibu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa CUF upande unaomuunga mkono mwenyekiti wa chama hicho, Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa, Khalifa Suleiman amesema chama chao hakiungi mkono maazimio ya vyama sita vya upinzani yaliyotolewa Zanzibar hivi karibuni.

Alieleza msimamo huo wakati akizungumza na Mwananchi mjini Unguja jana na kusema hawaungi mkono azimio la vyama hivyo kutangaza mwaka ujao kuwa vitafanya mikutano ya hadhara iliyokatazwa hata kama havitaruhusiwa.

Alisema kufanya mikutano iliyokatazwa bila kufuata taratibu ni kutaka kuiingiza nchi kwenye machafuko na watakaoathirika ni wananchi jambo ambalo hawakubaliani nalo.

“Maazimio hayo yana lengo la kuwaingiza Watanzania kwenye machafuko, sisi tunaamini katika meza ya mazungumzo, walitakiwa kumuandikia Rais kumueleza malalamiko yao na kuomba kukutana naye ili kujadili suala hili na kupata muafaka badala ya vurugu.”

“Kwa sababu ya kukosa busara na maamuzi sahihi hali kama hiyo iliwahi kutokea 2001 baada ya wanasiasa kuitisha maandamano yaliyokatazwa na Serikali na matokeo yake baadhi ya watu waliuawa, wengine kupata ulemavu wa kudumu na hawajafidiwa hadi leo, huku kwa mara ya kwanza Tanzania ikizalisha wakimbizi waliokimbilia Kenya na Somalia na wala hakuna mafanikio yaliyopatikana zaidi ya hasara,” alisema.

Alisema kwa upande wao wamefanya uchambuzi wa kina na wamejipanga kupeleka hoja zao bungeni kuhusu kuruhusiwa kufanyika kwa mikutano pamoja na marekebisho ya muswada wa vyama vya siasa.

Naye, mjumbe wa Baraza Kuu la CUF Taifa, Mohamed Habib Mnyaa alisema dai la kufanya mikutano ya hadhara si la msingi kwa sasa ikizingatiwa kuna fursa tele za mikutano lakini wahusika hawazitumii.

Alisema tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa mwaka 2015, wabunge na wawakilishi hawajakatazwa kufanya mikutano lakini hadi leo hakuna aliyejitokeza kufanya mikutano jimboni.



Chanzo: mwananchi.co.tz