Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maandalizi ya mapokezi ya Lissu yashika kasi

Lissu Kujaaaa Maandalizi ya mapokezi ya Lissu yashika kasi

Thu, 19 Jan 2023 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Maandalizi ya kumpokea Makamu Mwenyekiti wa Chadema -Bara, Tundu Lissu yameshika kasi huku chama hicho, kikichangisha Sh9 milioni za kufanikisha ujio wake.

Fedha hizo zimechangishwa ndani ya siku mbili na lengo ni kupata Sh10.5 milioni kabla ya Januari 25 mwaka huu,  ambapo Lissu atatua nchini kwa mara ya pili akitokea Ubelgiji anakoishi baada ya kupata kibali cha kuishi nchini humo.

Viongozi na wanachama wa Chadema, wanachangisha fedha hizo ili kufanikisha maandalizi ya kumpokea Lissu,  ambaye baada ya kutua Tanzania atafanya mkutano mkubwa wa hadhara katika eneo litakalowekwa wazi baadaye na uongozi wa chama hicho.

 Lissu aliondoka nchini Septemba 7, 2017 kwenda Nairobi Kenya kwa matibabu baada ya kushambuliwa kwa risasi katika makazi yake eneo la Area D jijini Dodoma,  muda mchache baada ya kutoka bungeni.

Alipatiwa matibabu nchini Kenya hadi Januari 6, 2018 aliposafiri kwenda Ubelgiji kwa ajili ya matibabu zaidi, kadhalika makazi ya uhamishoni. Alirejea Tanzania kwa mara ya kwanza Julai mwaka 2020 kwa ajili ya kushiriki uchaguzi mkuu, akiwania nafasi ya urais.

Novemba 10, 2020 alirejea Ubelgiji baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu, akidai kwamba usalama wa maisha yake upo hatarini.

Januari 13 mwaka huu, akitoa salamu za mwaka mpya, Lissu alieleza kusudio na tarajio lake la kurudi Tanzania Januari 25 na atashukia katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere saa 7:35 mchana.

“Naomba kuwafahamisha kwamba, panapo majaliwa nitakanyaga udongo wa ardhi ya Tanzania kwa mara nyingine tena siku ya Januari 25, saba na dakika 35 mchana,” alisema.

Akilizungumzia hilo, Kaimu Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Baraka Mwago ambao ndio wanaosimamia jukumu la maandalizi ya ujio wake alisema, Maandalizi ya ujio wa Lissu yanaendelea vizuri na kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wanachama na viongozi kutoa fedha kwa ajili ya kufanikisha suala hilo.

“Siku atakayotua atafanya mkutano hadhara katika eneo tutakaloweka wazi baadaye, pia muda utakapofika tutatoa taarifa polisi kuhusu ujio wake,” alisema Mwago.

Mwananchi lilimtafuta Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro ambaye alisema Lissu ni Mtanzania kama wengine wanaorudia nyumbani,” hata akifanya mkutano wa hadhara kuna tatizo gani?

“Mtu yoyote anaruhusiwa kurudi nyumbani na shughuli zinaendelea au sio? Wapo wengi wanaokwenda na kurudi,” alisema Muliro

Aidha, Mwago alisema fedha hizo zimechangwa na viongozi wa Chadema wanaoishi nchini na diaspora wanaoishi Marekani. Hata hivyo, Mwago alisema vikao vya maandalizi ya ujio wa Lissu bado vinaendelea.

 Mratibu wa Chadema Marekani, Liberatus Mwang’ombe alisema wanadaispora wanaoishi nchini humo, wameamua kujitoa kufanikisha maandalizi ya ujio wa Lissu kwa ushikirikiano na Chadema kanda ya Pwani.

Mwang’ombe alisema Chadema kanda ya Pwani waliomba nusu ya bajeti yao ambayo ni Sh10.5milioni. Alisema diaspora waliombwa kuchangia Sh5.25 milioni.

 “Sisi tukajiwekea lengo la kukusanya dola za Marekani 3,000, sawa na Sh.6.9 milioni ili fedha itakayozidi itumike kwa mikutano ya Lissu ya kuzunguka nchi nzima baada ya kufika Tanzania.

 “Fedha hizi hatukufanya hamasa kubwa kama kawaida yetu, lakini wanadaispora wamejitoa kwa

sababu tuna matumaini ya Lissu atakuwa kinara ya kusimamia upatikanaji wa Katiba Mpya akisharikiana na wenzake,” alisema.

Mwang’ombe alisema zaidi ya Sh5 milioni zilizokusanywa zilipatikana ndani ya saa tano kupitia makundi ya ‘club house’ na WhatsApp.

Aliongeza katika harambee hiyo walifanikiwa kupata Dola za Marekani 3,047 sawa na zaidi ya Sh7 milioni na bado watu wanaendelea kutoa kwa sababu michango hiyo itakuwa endelevu ili kumwezesha Lisu kuzunguka nchi nzima kuwashukuru Watanzania kwa kuwaunga mkono kwenye  Uchaguzi Mkuu 2020.

Mwang’ombe aliyegombea ubunge wa Mbarali mkoani Mbeya mwaka 2020,  alisema Lissu akishirikiana na vyama vingine watahakikisha wanapigania Katiba Mpya itakayoleta mazingira mazuri ya demokrasia na hali ya usawa kwa Taifa.

Juzi Ofisa Habari na Mawasiliano wa Chadema Kanda ya Pwani, Gervas Lyenda alisema Lissu atapokelewa na wanachama wa Chadema kisha atahutubia katika mkutano wa hadhara ulioandaliwa kwa ajili yake.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live