Dar es Salaam. Mshauri mkuu wa chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amesema vyama vya upinzani vitapata ugumu kushinda katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2020 bila kushirikiana.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo leo Jumatano Machi 4, 2020 katika mahojiano yanayofanyika katika ofisi za kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) Tabata Relini jijini Dar es Salaam.
Maalim Seif amesema tayari mazungumzo ya kushirikiana yameanza na vyama vingine.
“Kwa msimamo wa ACT Wazalendo sisi tunaamini tunahitaji ushirikiano. Hatuwezi kwenda kwenye uchaguzi huu chama kimoja. Tuangalie kwenye uchaguzi wa 2015 kuna maeneo tulipoteza kura chache sana kwa sababu tuligawanyika.”
“Vyama ambavyo viko makini kuuungana au kushirikiana ni jambo muhimu sana. Tunahitaji kufanya kazi pamoja. Sisi we have tried to reach out (tumejaribu kufikia) ni mapema mno kusema tumefikia hatua gani. Tumekwenda na response (majibu) siyo mbaya. Tukae tuangalie vipi tunaweza kupata ushirikiano ambao kila mmoja ataridhika,” amesema Maalim Seif.
Katika uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25, 2015, vyama vinne vikiongozwa na Chadema vilishirikiana na kuunda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa). Mbali na Chadema vyama vingine ni NLD, NCCR-Mageuzi na CUF.
Habari zinazohusiana na hii
- LIVE: MAALIM SEIF AKIWA MUBASHARA NDANI YA MWANANCHI KARIBU UTUFUATILIE
- VIDEO: Maalim Seif aweka wazi alichozungumza na Rais Magufuli
- Maalim Seif: Magufuli akutane na wapinzani wote kujadili uchaguzi huru na haki - VIDEO
Idadi hiyo ya kura za rais na kuongezeka kwa wabunge na madiwani kulisababisha Ukawa kuongeza majiji kama ya Dar es Salaam, Mbeya, Arusha; Manispaa na Halmashauri zaidi ya 20.
Mgombea urais wa Chadema aliyeungwa mkono na vyama shiriki vya Ukawa, Edward Lowassa alipata kura milioni 6.07 sawa na asilimia 39 huku Rais John Magufuli wa CCM akipata kura milioni 8.88 sawa na asilimia 58.46.
Hivi karibuni wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti, Chadema kimesema kinathamini ushirikiano na tayari kimeunda kamati ndogo ya kamati kuu ambayo itakuwa na jukumu la kufanya mazungumzo na vyama vitakavyokuwa tayari kushirikiana kwenye uchaguzi huo.
Hoja ya Chadema iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Chaumma, Hashim Rungwe ambaye anasema kilichotokea katika uchaguzi wa serikali za mitaa Novemba 24, 2019 kinawapa shaka kama kutakuwa na uchaguzi mkuu au la.
Naye Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mawasiliano ya Umma wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu amesema wako tayari kushirikiana na vyama vingine makini vya upinzani na kwamba chama hicho kilipitisha uamuzi huo kabla ya uchaguzi wa serikali za mitaa.
Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia alitaja mambo matano ambayo ni kiini cha mkwamo wa kuungana. “Kumekuwa na vurugu tangu 2015, hakuna utulivu wa fikra kwenye vyama na hiyo yote inasababisha kukosekana utulivu wa kisiasa na mambo mengi yanaharibika,” anasema Mbatia.
“Kama conflicts (migogoro) ziko ndani ya vyama, Chadema wenyewe hawaaminiani viongozi wao wanahama hama, atapata wapi muda wa kuzungumzia kuungana na mwingine?” alihoji Mbatia.
“CUF wenyewe kwa wenyewe hawaaminiani. ACT- Wazalendo tunaosema ni chama mbadala lakini wapo kwenye uchaguzi wa ndani halafu ndiyo wajipange tena kwa uchaguzi mkuu,” alisema.
“Tuko njia panda. Kuungana kwa upinzani kuwa na nguvu ya pamoja uchaguzi mkuu 2020 kwa uchambuzi nilioufanya kwa kweli niwe mkweli, tuko njia panda,” alisisitiza.
Naye Katibu Mkuu wa CUF, Khalifa Suleiman amesema, “mpaka sasa hakuna chama kilichokuja kutaka kushirikiana na sisi, tunaendelea na maandalizi ya kuingia kwenye uchaguzi sisi wenyewe.”
Alipoulizwa kwamba haoni kuunganisha nguvu kuna tija kama ilivyokuwa 2015, Suleiman alisema “hakuna faida”.
“Mwaka 1995 na 2015 tumeshirikiana na tumepata viti vingi lakini umeona yaliyotokea. lazima tujue lengo halisi la kushirikiana na lipi,”anasema.