Dar es Salaam. Mshauri Mkuu wa chama cha upinzani Tanzania cha ACT- Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amewataka Wazanzibari kuhakikisha wanapata vitambulisho vipya vya Mzanzibari mkaazi akisema vina umuhimu mkubwa katika maisha yao.
Amesema kadi hiyo siyo umuhimu katika uchaguzi mkuu bali katika shughuli binafsi za kila siku ikiwamo kutaka kupata kazi au wakati wa kujiunga na vyuo kwa wanafunzi.
“Ukitaka kuuza shamba au kusafiri lazima uwe nacho kitambulisho cha Mzanzibari mkazi. Nasaha na ombi langu kwa Wazanzibari tuache yote tuliyo nayo kila moja ahakikishie anakipata kitambulisho,” alisema Maalim Seif.
Mshauri mkuu huyo ameeleza hayo jana Jumatatu Januari 6,2020 ikiwa ni ujumbe kwa Wazanzibari.
Maalim Seif ambaye amewahi kuwa makamu wa kwanza wa Rais wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa Zanzibar (SUK) alisema kitambulisho pia kwa sababu huwezi kutumia haki ya kupiga kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi mbalimbali bila kuwa na kadi hiyo.
“Ukitaka kuhakikisha tunaiondoa CCM madarakani lazima kwanza uwe na kitambulisho. Acha shughuli zako zote hakikisha unapata kitambulisho, ukikipata rudi uendelee na shughuli zako,” amesema Maalim Seif.
Mwaka 2019 akizindua mchakato huo, Rais wa Zanzibar, Ali Mohamed Shein alisema vitambulisho hivyo vitaiwezesha serikali kuweka na kuhifadhi kumbukumbu za matukio ya watu wote katika daftari la usajili na utambuzi.
Alisema matumizi ya vitambulisho hivyo vitasaidia Serikali, taasisi na watu binafsi kupanga vipaumbele vya utekelezaji wa shughuli mbalimbali zenye mnasaba na huduma za maendeleo ya kijamii.
Kwa mujibu wa Rais Shein, kuwapo kwa mfumo huo wa matumizi ya vitambulisho vipya utasaidia serikali katika kuwatambua watu wanaostahiki kupata haki za msingi, kama ilivyobainishwa katika Katiba ya Zanzibar ya 1984.