Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maalim Seif aeleza atakavyorudisha kadi ya CUF

49779 Pic+maalim

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwanachama wa ACT- Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amesema hawajarudisha kadi ya chama chake cha zamani cha CUF, lakini wameweka utaratibu maalumu wa kuirudisha yeye na wenzake.

Machi 18, 2019 Maalim Seif na wenzake walijiunga na ACT- Wazalendo baada ya Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam kukubaliana na uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa wa kumtambua Profesa Ibrahim Lipumba kama mwenyekiti halali.

Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa Waziri Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na baadaye Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, ametoa kauli hiyo leo Jumatatu Aprili mosi, 2019 wakati wa mahojiano katika kipindi cha 360 kinachorushwa na Clouds TV.

“Tumeshadhamiria wote  kila aliyekuwa mwanachama wa CUF bendera zote, Katiba, sare  na kadi tunazikusanya na kumkabidhi kiongozi wa chama (Zitto Kabwe) azikabidhi kwa Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye atajua cha kufanya,” amesema Maalim Seif. 

Mbali na hilo, Maalim Seif amesema uamuzi wake wa kujiunga ACT- Wazalendo haujamshusha umaarufu wake bali upo palepale.

Katika shughuli ya kukabidhiwa kadi iliyofanyika Machi 18, 2019 makao makuu ya ACT-Wazalendo, Maalim Seif alikabidhiwa kadi namba moja huku Juma Duni Haji 'Babu Duni' akikabidhiwa namba kumi.

Babu Duni ndiye alikuwa pekee ambaye alipokabidhiwa kadi mpya, alimpa kadi ya CUF, Zitto huku akimweleza ampelekee Profesa Lipumba.

 



Chanzo: mwananchi.co.tz