Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Maalim Seif: Yanayotokea ACT Wazalendo tuliyatarajia, yanatujenga, hayaturudishi nyuma

49062 Maalimpic

Thu, 28 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwanachama mpya mwenye kadi namba moja wa  chama cha ACT Wazalendo, Maalim Seif Sharif Hamad amesema yanayotokea sasa dhidi ya chama hicho waliyatarajia na yanawajenga badala ya kuwarudisha nyuma.

Maalim amesema hayo leo akiwa makao makuu ya chama hicho Kijitonyama jijini Dar es Salaam baada ya polisi kuzuia mkutano wao uliokuwa ufanyike kwenye ukumbi wa mikutano wa PR Stadium Temeke jijini Dar es Salaam.

Amesema hashangai hayo kutokea na kila wanavyowadhibiti ndiyo wanawakuza.

“Nawashangaa watu hawa hawajifunzi, kila wanavyotuminya ndivyo wanavyotukuza na tayari tumeshashusha tanga na kupandisha tanga na safari inaendelea,” amesema Maalim Seif huku akipigiwa makofi na wanachama wa chama hicho waliokusanyika kwa dharura.

Amesema kinachoitisha dola ni wananchi kuhudhuria mikutano kwa wingi wakati wanataka dunia iamini vyama vya upinzani havina wafuasi.

Amesema ACT Wazalendo ni chama kichanga lakini kimeonyesha mwelekeo na kwa mipango iliyopangwa hakuna wasiwasi Watanzania watakiunga mkono na ndiyo ugomvi uliopo baina yake na dola.

Related Content

“Dola ya sasa ipo katika kujilinda inataka ibaki madarakani hadi mwisho wa dunia na wamesahau kuwa atakayebaki ni Mwenyezi Mungu na si mwingine.”

 “Wanajua ACT Wazalendo ikipewa nafasi hawatakuwa salama huo ndiyo ugomvi mkubwa uliopo, lakini nataka niwakumbushe, hii ni nchi ya kidemokrasia katiba ya nchi inaruhusu vyama vingi na inatoa haki sawa kwa vyama vyote, inashangaza kuona vingine vinabaguliwa, ”amesema.

Amedai kuna ubaguzi ambapo kuna watu wanafanya shughuli za chama bila kubaguliwa huku wengine wakizuiwa.

“Niwakumbushe watawala kwamba ukimchukua paka ukamtia kwenye chumba ukafunga milango na madirisha atakuja kukurarua, watu wamevumilia wakija kusema watoe jazba zao hakuna polisi, hakuna chochote kitakachowazuia,” amesema.

Maalim Seif amedai Zanzibar amezuiliwa kwenda kwenye baadhi ya mikoa.

Kwa upande wake, mwenyekiti wa chama hicho, Kulwa Maganja amesema: “hata uwe na nguvu  kiasi gani kuupinga upinzani unapoteza muda wako kwa sababu haijawahi kutokea mtu yeyote akacheza na demokrasia akabaki salama.”

Naye makamu mwenyekiti wa chama hicho Bara,  Shabani Mambo amesema kuwa viongozi wanaoongoza taifa wasicheze na muda na wafahamu Watanzania wa mwaka 1961 wakati nchi inapata uhuru siyo wa leo.

 “Waangalie haki ya msingi ya kila Mtanzania na wampe haki, muda huu mchache kabla watu hawajafikiria kwenda kuichukua haki yao wawape zote za msingi waziache huru,” amesema Mambo.

Naye mwanachama wa chama hicho, Saweji Mketo amesema kuwa lililotokea jana limezidi kutengeneza hamasa zaidi.

Amesema chama hicho kinakwenda kuongoza nchi na kitakapopata nafasi mwaka 2020 apewe wizara ya mambo ya ndani awafanyie kazi polisi wakae vizuri ili wafanye kazi kwa jamii.

Kwa upande wa kiongozi wa chama hicho,  Zitto Kabwe amesema utaratibu wa kugawa kadi za chama hicho utaendelea kama kawaida.

Amewataka wanachama warudi kwenye matawi yao na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam wafanye utaratibu wa  kupita kwenye matawi kugawa kadi kwa wanachama.

"Tumeukwepa mtego wao, walidhani wakizuia mkutano sisi viongozi tutawalazimisha wanachama ufanyike ili waseme tumefanya fujo.

"Wanaokoteza makosa, lengo lao ni kukifuta chama kwa kila hali, tusiwape hiyo nafasi, "amesema Kabwe.

Amesema kuwa anakwenda kukutana na sekretarieti kwa ajili ya kujadili mwelekeo wao.



Chanzo: mwananchi.co.tz