Waziri wa Madini, Dotto Biteko amempa siku tatu mtendaji mkuu wa kampuni ya uchimbaji madini Tembo Nickel, Chris Showalter kutengeneza mpango kazi na kuuwakilisha wizarani ili waziri afanye mchakato wa kuwapatia leseni.
Waziri Biteko ameyasema hayo leo Jumatatu, Agosti 2, 2021 alipotembelea eneo la mgodi huo na kumtaka mtendaji huyo kumpatia taarifa ya shughuli zinazoendelea katika mgodi huo ambao mkataba wa uchimbaji ulisainiwa na hayati John Pombe Magufuli na kampuni hiyo mwanzoni mwa mwaka huu.
"Natoa siku tatu niwe nimepata taarifa ya shughuli zitakazofanywa na kampuni ya Kabanga Nickel maana tangu Januari 19, 2021 tulisaini mkataba wa kuchimba madini ya Nickel lakini hadi sasa hakuna kinachoendelea hii ni kuwadanganya wananchi walioshuhudia utiaji saini mkataba wa uchimbaji," amesema Waziri Biteko.
Aliongeza kwamba, anataka kuona kwenye mpango kazi wakieleza ni wananchi wangapi watapewa fidia, watapewa kiasi gani na watatumia muda gani na waeleze mpango kazi wa ujenzi wa barabara.
Aidha Mh.Bitekoameiagiza kampuni hiyo ianze kuajiri wafanyakazi wakati ikisubiri kupata leseni.
Kwa upande wake Mtendaji mkuu wa Mgodi huo,Showalter amesema kuwa uchimbaji huo utakapoanza Serikali itanufaika na kodi mbalimbali na itapata asilimia 16 katika uzalishaji wa madini na kampuni ya Kabanga itapata asilimia 84 na kuwa mapato yatakayopatikana Serikali itapata asilimia 50 na kampuni itapata asilimia 50 huku kwa upande wa ajira amesema kampuni hiyo itaajiri wafanyakazi zaidi ya 1,900.