Kamishna wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji mstaafu Thomas Mihayo amewasisitizia wasimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Ngorongoro, Chamwino na Nyang'ware kuvishirikisha vyama vya siasa na wadau wengine ili kuwarahisishia utekelezaji wamajukumu yao ya kujenga mahusiano mazuri.
Akizungumza katika mafunzo ya watendaji wa uchaguzi ngazi ya jimbo na kata yaliyofanyika mkoani Arusha leo Novemba 3, 2021 Jaji Mihayo amesema ni vyema wakahakikisha wanatambua na kuyafahamu vizuri maeneo ambapo chaguzi zitaendeshwa ikiwemo hali ya miundombinu ya kufika katika kata na vituo vya kupigia kura.
Jaji Mihayo amesitiza kuwa ni vyema utambuzi wa vituo vya kupigia kura ukafanywa mapema ili kubaini mahitaji maalumu ya maeneo husika kwa lengo la kuhakikisha mpangilio mzuri ambao utaruhusu uchaguzi kufanyika kwa utulivu na amani.
Amesema wasimamizi hao ni vyema wakazingatia kuwaajiri watendaji wa vituo wenye weledi wanaojiitambua na kuachana upendeleo.
Wasimamizi wa uchaguzi wameahidi kufanya kazi kwa uadilifu ili kuhakikisha uchaguzi unakwenda vizuri.
Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo la Ngorongoro, Jumaa Mhina amesema wamejipanga vizuri kuhakikisha kwamba uchaguzi huo unafanyika kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu na maelekezo pamoja na kuzingatia demokrasia hivyo ni vyema vyama vyote vya siasa kuchukua fomu za ubunge wa jimbo hilo katika ofisi ya msimamizi wa uchaguzi kuanzia Novemba 9 hadi 15 mwaka huu.
"Itakapofika Novemba 15 mwaka huu muda wa saa kumi kamili jioni watafanya zoezi la uteuzi la wagombea ubunge wa jimbo hili la Ngorongoro na mnamo Novemba 16 mwaka huu tutaanza rasmi kampeni na ifikapo Desemba 11 itakuwa siku ya kupiga kura ikiwa kampeni zitaisha Desema 10 ,2021,"amesema Mhina.