Matumaini ya wadau wa siasa juu ya kukoma kwa utaratibu wa wakurugenzi wa halmashauri kusimamia uchaguzi yanaendelea kuyeyuka baada ya Serikali kuwasilisha bungeni muswada unaopigia msumari uhalali wa jambo hilo.
Hayo yanatokana na miswada mitatu ya Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Sheria ya Uchaguzi wa Wabunge, Madiwani na Rais pamoja na Sheria ya Vyama vya Siasa, iliyowasilishwa bungeni wiki iliyopita.
Kwa nyakati tofauti wadau hao walisema wakurugenzi kusimamia uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani pamoja na Rais kuwa na mamlaka ya kuteua Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kunafanya uchaguzi usiaminike.
Hata hivyo, Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria, Mary Makondo alisema jana kuwa Serikali imetoa nafasi ya kusikiliza maoni ya umma baada ya muswada huo kusomwa kwa mara ya kwanza bungeni.
Alisema hiyo ndiyo nafasi ya wananchi wa makundi mbalimbali kushauri kuhusu kilichomo.
“Tumetoa nafasi ya public hearing (maoni ya umma), ni fursa ya kutoa mapendekezo yao, baada ya muswada kusomwa bungeni,” alisema Mary.
Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Dk Eliezer Feleshi alisema utungaji wa sheria ni mchakato utakaoendelea kuwashirikisha wadau wote kwa mujibu wa sheria na kanuni za Bunge.
“Katika hatua hii mimi siwezi kujua nini kitajiri kwenye public hearing,” alisema Feleshi.
Kwa mujibu wa Ibara ya 74(14) ya Katiba ya Tanzania, ni marufuku kwa watu wanaohusika na uchaguzi kujiunga na chama chochote cha siasa, isipokuwa tu kila mmoja wao atakuwa na haki ya kupiga kura iliyotajwa katika Ibara ya 5 ya Katiba.
Lakini kifungu cha 6(1) cha muswada wa sheria ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani wa mwaka 2023 uliowasilishwa bungeni na kusomwa kwa mara ya kwanza wiki iliyopita, kimezidi kufifisha matumaini ya wao kutosimamia uchaguzi.
Kifungu hicho kinasema kila mkurugenzi wa jiji, manispaa, mji na wilaya atakuwa msimamizi wa uchaguzi kwa madhumuni ya kuendesha uchaguzi katika jimbo au kata na msimamizi huyo anaweza kusimamia jimbo zaidi ya moja.
Lakini kifungu kidogo cha (2) cha sheria kinasema NEC inaweza kuteua kwa kuzingatia nafasi aliyonayo mtu katika ofisi au kwa jina kutoka miongoni mwa watumishi wa umma mwenye sifa za mkurugenzi kuwa msimamizi wa uchaguzi.
Kifungu kidogo cha (5) kinasema msimamizi wa uchaguzi, kwa kuzingatia maelekezo ya mkurugenzi wa uchaguzi, anaweza kuteua watendaji kwa idadi inayohitajika, kwa dhumuni ya kuendesha uchaguzi katika jimbo au kata.
Ukiacha sheria hiyo, muswada wa Sheria ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi wa mwaka 2023 haujatoa suluhusho la muda mrefu la wadau wa uchaguzi, wanaotaka Rais na mwenyekiti wa CCM, asiteue mwenyekiti na makamu wa NEC.
Kifungu cha 5(1) kinasema NEC itakuwa na mwenyekiti, makamu na wajumbe wengine watano watakaoteuliwa na Rais, lakini hapohapo sheria inasema NEC itakuwa ni chombo huru, kinachojitegemea na uamuzi wake hautaingiliwa.
Sheria hiyo inasema wajumbe hao watano, watateuliwa baada ya majina yao kupatikana baada ya usaili utakaofanywa na kamati itakayofanya uchunguzi na kumshauri Rais, lakini muundo wa kamati hiyo nao unadaiwa kuwa na ukakasi.
Wajumbe hao ni jaji wa Mahakama ya Rufani atakayekuwa mwenyekiti, kamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, kamishna wa Sekretarieti ya maadili ya viongozi wa umma bara na yule wa Zanzibar.
Katika muundo huo, wamo pia wajumbe wawili wenye uzoefu wa masuala ya uchaguzi kutoka Tanzania Bara na mwingine kutoka Zanzibar na Rais atateua mjumbe mmoja kadiri atakavyoona inafaa lakini kwa kuzingatia jinsia.
Akizunguzia muswada huo, mwanasheria Dk Rugemeleza Nshallah alikifananisha kilichofanywa katika miswada ya sheria hizo na kejeli na mzaha dhidi ya watu waliokuwa wanadai mabadiliko hayo.
Alisema kejeli na mzaha huo, unatokana na kilichobadilika katika miswada hiyo kuwa ni lugha kutoka Kiingereza kuwa Kiswahili, lakini si muktadha uliotarajiwa.
“Kilichofanyika ni sawa na kujaza upepo kwenye tairi lenye pancha, mwisho wa siku hizi ni hadaa, kejeli na mzaha dhidi ya waliokuwa wanadai mabadiliko,” alisema Dk Nshalla ambaye pia ni mchambuzi wa masuala ya siasa.
Alisema licha ya ripoti ya kikosi kazi na vikao vya mapendekezo ya mabadiliko, hakuna kilichotiliwa maanani katika miswada hiyo.
Mhadhiri wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Mohamed Bakary alisema muswada huo una matobo mengi na haujatatua matatizo ya msingi.
Aliyataja baadhi ya matobo hayo ni hatua ya wakurugenzi kuendelea kusimamia uchaguzi, akifafanua kwa mfumo wa utawala wa Tanzania jambo hilo si sawa.
Aliufafanua mfumo huo wa utawala, akisema uteuzi wowote nchini unafanywa kwa kuangalia uelekeo wa kisiasa na kwamba wakurugenzi hao ni wanachama wa CCM, watatendaje haki kwa vyama vya upinzani.