Baada ya mbio ndefu za uchaguzi mdogo wa ubunge katika majimbo matatu hatimaye matokeo yametoka ambapo Chama cha Mapinduzi (CCM) kimepata ushindi kwenye majimbo yote ya matatu ya Songea Mjini, Singida Kaskazini na Longido.
Akitangaza matokeo katika jimbo la Songea Mjini, msimamizi wa uchaguzi, Tina Sekambo amemtangaza Dkt Damas Ndumbaro kuwa mshindi kwa kupata kura 45,762 sawa na 97%.
Wagombea wengine ni Christina Thinangwa wa CUF amepata kura 608 huku Neema Tawete wa ADA-TADEA akipata kura 471 na kubainisha kuwa waliojiandikisha kupiga kura walikuwa 28,841.
Katika jimbo la Singida Kaskazini ambalo liliachwa wazi na Lazaro Nyalandu CCM imerudisha jimbo hilo,ambapo msimamizi wa uchaguzi, Rashid Mandoa amemtangaza mgombea Justine Monko (CCM) kuwa mshindi baada ya kupata kura 20,857 sawa na 93.5%.
Matokeo ya wagombea wengine ni Dalphine Mlewa wa CUF kura 974, Aloyce Nduguta wa Ada-Tadea kura 265, Omar Sombi wa AFP kura 116 na Mchungaji Yohana Labisu wa CCK kura 86.
Mandoa amesema kura zilizopigwa ni 22,298, waliojiandikisha kupigakura ni 91,518, watu 69,220 ambao ni zaidi ya asilimia 70 hawakujitokeza kupiga kura.
Na kwa upande wa jimbo la Longido msimamizi wa uchaguzi, Jumaa Mhina amemtangaza Dkt. Stephen Kiruswa kuwa mshindi baada ya kupata kura 41,258 sawa na 99.1% .
Hata hivyo kwenye uchaguzi huo wa marudio baadhi ya vyama vya upinzani vikiwemo CHADEMA, ACT Wazalendo, CHAUMA n.k vilisusia kushiriki kwenye uchaguzi huo.
Soma zaidi – ACT Wazalendo wasusia kushiriki uchaguzi mdogo wa majimbo matatu, waeleza sababu